Miss World 2023 kufanyika India

Dar es Salaam. Hatimaye Waandaaji wa shindano la ulimbwende la dunia (Miss World), wamebainisha kuwa, fainali za mwaka huu zitafanyika Desemba 9 nchini India.
Tanzania itawakilishwa na Miss Tanzania 2022, Halima Kopwe; ambaye katika moja ya mahojiano na Mwananchi, alieleza namna alivyojipanga kufanya vizuri, na hasa kwenye kinyang'anyiro cha mataji madogo madogo katika fainali hizo.
"Naendelea kufanya project yangu ambayo nitakwenda nayo kwenye Miss World, sijajua ni lini na wapi zitafanyika, lakini niko vizuri ninaamini nitafanya vizuri zaidi kwenye yale mataji madogo madogo, ambayo yatanisogeza kwenye nafasi ya kufanya vizuri,” alisema Halima kwenye mahojiano na gazeti hili hivi karibuni.
Tayari Kamati ya Miss World imetegua kutendawili cha lini na wapi zitafanyika fainali hizo kwa kulitaja Jiji la New Delhi, India kuwa mwenyeji.
Kamati ya Miss Tanzania imeeleza kupokea taarifa ya fainali hizo na warembo wote wataingia kambini mwezi mmoja kabla mashindano.
"Tunamtakia kila la heri Miss Tanzania katika kutuwakilisha kwenye mashindano ya dunia," imesema taarifa ya Kamati ya Miss Tanzania.
Wakati huo huo, fainali za Miss Tanzania mwaka huu zitafanyika kesho kwenye ukumbi wa Super Dom, Dar es Salaam.
Mrembo wa mwaka huu ataondoka na gari aina ya mercedes Benz.