Muziki wa Jazz kuja na tamasha lake nchini

Linapokuja swala la muziki nchini, huwezi kuacha kutaja Bongo Fleva, Taarab, Hip-Hop, dansi na Afrobeat. Lakini umewahi kufahamu ya kwamba, kuna aina nyingine ya muziki ambayo inaweza kukubadilisha kutoka kwenye huzuni mpaka furaha?
Nauzungumzia muziki wa Jazz. Ni moja ya aina ya muziki ambao umekuwepo kwa takribani miaka 100 iliyopita. Muziki huu umekuwa ukiweka msingi katika aina zingine za muziki kama vile soul, rock-n-roll, metal, Hip-Hop, go-go, n.k. Ingawa mara nyingi aina ya muziki huu hupuuzwa.
Katika kuhakikisha kwamba wapenda muziki wanapata nafasi ya kufahamu aina hii ya muziki, Patrick Chilijila aliamua kuja na kitu kinaitwa ‘Evergreen Afro Jazz’, tamasha pekee ambalo litatoa nafasi kwa vizazi nchini kuufahamu muziki wa Jazz na kutoa nafasi kwa wapiga vyombo ambao wamekuwa nyuma ya waimbaji kwa muda mrefu.
Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa mradi huo, bwana Patrick Chilijila maarufu kama Steve DC, amesema ujio wa tamasha hili litabadilisha namna ambavyo watu wamekuwa wakiufahamu muziki wa Jazz na namna ambavyo wataweza kutoa nafasi kwa wapiga vyombo ambao wanatamani kuonesha vitu vikubwa.
“Jazz ni aina ya muziki ambao sio ngeni sana nchini kwetu, ila tumeamua kuutangaza kwa mara ya kwanza ili tuwe na walaji wa aina tofauti tofauti kwenye ulimwengu wa muziki hapa nchini kwetu. Tutakuwa tunachanganya ladha kutoka kwenye makabira mbalimbali nchini kissha tunatengeneza kitu ambacho kitakuwa cha utofauti kwa msikilizaji,”
Ameongeza kwa kusema kwamba, Kwa muda mrefu watu wanaopiga ala, wamekuwa nyumba ya wasanii kwa ajili ya kunogesha muziki, kupitia Evergreen Afro Jazz wameona kwamba ndio muda wa kuonesha uwezo ambao wapiga vyombo wanao.
“It’s time to come out na kuonesha kile ambacho tunaweza kukifanya kwa ukubwa na sio tu pale ambapo mtu anakuwa anaimba. Wapo ambao watakuwa wanapiga na kuimba, na wapo ambao watakuwa wanacheza ala hizi za Jazz kwa muda mrefu stejini,”
Tamasha hilo linatarajia kufanyika Julai 29, jumamosi katika viwanja vya kijiji vya makumbusho. Hii itakuwa ni kwa mara ya kwanza kuwepo na tamasha kuhusu muziki wa Jazz na litakuwa likifanywa kwa mwaka mara moja.