Mwanamuziki Sinead o'Connor aliyefariki dunia katufunza nini?

Wapo wanamuziki wa aina mbalimbali ulimwenguni. Wanaotuchezesha tukarukaruka kama Diamond Platnumz, Kofi Olomide; marehemu Fela Kuti (Nigeria) na James Brown (Marekani).

Wanaotuliwaza tukawapenda bila kuelewa lugha zao ni Salif Kaita (Mali), Youssou Ndour na Mbaaba Mal (Senegal), Bonga (Angola) au Oum Kulthum (“Sauti ya Misri” aliyefariki 1975). Mazishi yake Umm au Umi (mama kwa Kiarabu); yalihudhuriwa na watu milioni nne na Miriam Makeba (Malkia wa Afrika aliyefariki dunia jukwaani 2008).

Pia, magwiji wetu Afrika Mashariki: Salum Abdala (1965), Fundi Konde (Kenya), Marijani Rajabu (1994), Frank na dada zake.

Tusiwasahau wana Taarab: Shakila na Asmahani.

Je leo? Nani wa kizazi kipya anayetugusa kwa melodi? Kinadharia muziki ni vipengele vitatu: melodi, ridhimu (mapigo) na mpangilio (harmony).

Nani hutugusa bila hata kumwelewa anachokisema (melodi)?

Tunao wanamuziki wasioimba. Wanaopiga muziki wa ala, wanamuziki wa Jazz, mathalan, kama Abdala Ibrahim, mwana piano (kinanda) wa Afrika Kusini.

Vile vile wanaojulikana kwa ufundi tu wa vyombo, (maana muziki si tu “kuimba!”). Wanawake “wapiga vyombo” bendi ya Beyonce, -Suga Mamas - ni hatari.

Mwanamuziki Mmarekani, Prince aliyefariki mwaka 2016, alipiga vyombo zaidi ya 20, aliimba, alicheza na kutunga pia.

Wapo wanamuziki tunaowapenda kwa elimu na maudhui. Kama mpiga Reggae, Bob Marley (Jamaica), aliyefariki dunia mwaka 1981 au Bob Dylan (Marekani) aliyepewa tuzo mashuhuri ya Nobel mwaka 2016, kwa “kuendeleza mila ya uandishi wa nyimbo za Kimarekani.”

Au Caetano Veloso na mwenzake Gilberto Gil – Wabrazili waliowekwa jela, kisha wakakimbilia London, miaka ya Sitini.

Leo muziki wao unasujudiwa ulimwenguni kote, ingawa huimbwa Kireno.

Na hapa katika msimamo imara wa kimaudhui ndipo aliposimama Sinead O’ Connor, mada yetu leo. Sinead O'Connor (aliyesilimu na kuitwa Shuhada Sadaqat) alifariki dunia London, wiki mbili zilizopita.

Alizaliwa mwaka 1966, Dublin, Ireland. Anadai katika wasifu wa maisha yake, aliteswa utotoni na mama yake mzazi. Kuanzia hapo maisha yake yalitota vituko na tafrani.

Aliolewa mara nne na kuachana na waume aliowazalia, watoto wanne. Alifahamika kama mtetezi wa haki za watoto, wanawake na mafukara.

Vipaji vyake mseto vilichanganya utunzi, sauti safi, uandishi na upigaji gitaa. Albam yake mosi, 1987, “The Lion and The Cobra” (Simba na Nyoka) Zaburi 91:

“Utawakanyaga simba na nyoka wakali, simba mkubwa na nyoka utawaponda kwa miguu.”


Alisifiwa sana kwa kazi hii.

Kutokana na wanahabari kumsakama “kuwa mrembo” alifanya mapinduzi makubwa kwa kunyoa kipara. Kitendo hiki kilimpa utofauti uliosisitiza kuwa yeye si msanii wa kuchezewa chezewa.

Mwaka 1990 alifahamika dunia nzima baada ya kuurekodi wimbo ulioandikwa na nguli Prince – Nothing Compares 2 U. Ubeti wa tatu:

“Upweke umeshadidi toka uondoke

Kama ndege bila wimbo

Hakuna kitakachomudu kusitisha machozi ya kipweke kutiririka...”

Nothing Compares 2 U, ulitisha. Alizawadiwa tuzo mashuhuri ya Grammy. Akaikataa akisema ni biashara isiyo na utu. Mwaka 1992 akaalikwa kuimba Idhaa ya NBC kipindi mashuhuri cha Jumamosi “Saturday Live.”

Badala ya kuchekacheka, akaimba wimbo maarufu wa Bob Marley (War) kutathmini unyanyasaji (na ulawiti wa watoto).

Miaka ya baadaye aliitwa shujaa wa utetezi wa wanyonge, msanii wa kipekee, aliyechangia ubunifu katika muziki duniani.