Mwanasheria amtetea R Kelly vitendo vya uzinzi

Friday September 24 2021
rkellypic
By Mwandishi Wetu

New York, Marekani (AFP). Timu ya utetezi ya R. Kelly jana Alhamisi Septemba 23, 2021 ilimpachika nyota huyo wa R&B jina la "sex symbol (alama ya ngono)" ambaye aliishi maisha ya kupenda mahusiano ya kimapenzi.

Wakili huyo alisema hayo  wakati ikifanya majumuisho ya hoja zake katika kesi inayomkabili msanii huyo ya tuhuma za kuongoza genge la uhalifu wa kingono kwa takriban miongo mitatu.

R.Kelly aliyejipatia umaarufu mkubwa duniani kutokana na nyimbo zake za miondoko ya R&B katika miaka ya tisini ukiwemo wa "I Believe I Can Fly", anakabiliwa na mashtaka ya kuwafanyia wanawake sita na wanaume wawili uhalifu wa kingono na kupiga picha za video za ngono za watoto.

Soma zaidi: Ushahidi wamuweka pabaya R Kelly

Jana (Alhamisi), wakili Deveraux Cannick aliwaelezea watu wanaodai kuathiriwa na vitendo vya R.Kelly -- ambao tuhuma zao zinajumuisha ubakaji, kuwekwa kizuizini, picha za ngono kwa watoto pamoja na kunyanyaswa kimwili na kiakili -- kuwa ni watu wenye uchu wa fedha.

Wakili Cannick alisema serikali inajitahidi kugeuza tabia ambayo ni ya kawaida miongoni mwa watu maarufu kimataifa, kuwa ni uhalifu.

Advertisement

"Kampuni yake ya muziki ilianza kumtangaza (R.Kelly) kama alama ya ngono na mpenda mahusiano ya kimapenzi, kwa hiyo alianza kuishi maisha ya namna hiyo," mwanasheria huyo aliiambia mahakama.

"Wapi kuna kosa katika hilo?"

Majumuisho hayo ya upande wa utetezi yamekuja saa sita baada ya hoja kali za upande wa mashtaka, ambazo zilimuelezea nyota huyo wa muziki kama bosi wa uhalifu ambaye aliongoza vitedo hivyo dhidi ya wanawake na watoto wadogo kwa msaada wa wafanyakazi na washirika wake.

Baada ya kumaliza, mwanasheria msaidizi wa serikali, Nadia Shihata alianza kutoa hoja kinzani, akielezea utetezi huo kuwa "hauna mashiko" na "wa aibu".

"Usiwaruhusu wakupoteze," alisema, akiongeza kuwa utetezi huo unalenga kupotosha kwamba "wanawake wote hawa na wasichana walikuwa wakipenda na walistahili walichofanyiwa."

Katioka majumuisho yake, Cannick alitumia sauti ya dhihaka alipokuwa akirejea ushahidi wa waathirika -- ambao tisa ni wanawake na wanaume wawili ambao walisema Kelly aliwatendea isivyostahili -- akihoji uaminifu wao na kusema walikuwa wakitafuta fedha.

"Watu wengi wanaishi kwa mgongo wa R. Kelly," alisema, wakitengeneza makala kwa jina la "Surviving R. Kelly" ambazo ziliamsha mtazamo wa muda mrefu wa tuhuma dhidi ya mwanamuziki huyo.

Mwanzoni mwa majumuisho ya aina yake, Cannick alianza hoja zake kwa kukumbushia enzi za mwanaharakati wa Marekani, Martin Luther King Jr., akisema Kelly alikuwa akijaribu tu kupinga ukiukwaji wa haki kama alivyokuwa akifanya kiongozi huyo wa kupigania haki za kiraia.

Aliiambia mahakama kuwa "si kosa, mapenzi ya nguvu (kinky sex)" na kwamba "baadhi ya watu wanapenda" uhusiano baina ya mwanamume mwenye umri mkubwa na "msichana mdogo."

"Mmesikia kuhusu mtu aliyewachukulia wanawake hawa kama dhahabu," alisema Cannick. "Aliwanunulia mikoba na magari ya thamani."

Kelly, ambaye jina lake la kuzaliwa ni Robert Sylvester Kelly, anakabiliwa na kosa moja la unyang'anyi na makosa nane ya kuvunja sheria ya mwaka 1910 ambayo ilipiga marufuku usafirishaji wa mwanamke au msichana kwa sababu za kingono kwenda majimbo ya Marekani.

Advertisement