Mwanzilishi wa Daz Nundaz alivyoteuliwa kuwa msaidizi wa Mtume Mwingira

Jana Mtume na kiongozi wa kiroho wa makanisa ya Efatha ulimwenguni, Noely Kapinga alieleza namna alivyojikita kwenye Bongofleva hadi kuanzisha kundi la Daz Nundaz lililotamba mwishoni mwa miaka ya 1990 hadi mwanzoni mwa 2000, wakati huo akijulikana kwa jina la Critic.

Katika mwendelezo wa makala hii, Mtume Noely anaeleza namna alivyokutana na Mtume na Nabii Mwingira na kuamua kumtumikia Mungu jumla.

Anasema siku ya kwanza ilikuwa ni Mwenge, kwenye kanisa la Efatha ambako alikwenda kusali, ingawa wakati huo alikuwa bado ana hisia tofauti kuhusu watumishi.

"Nilikuja Dar es Salaam, mwanzoni mwa mwaka 2011 nilikwenda kusali ili nionane naye kwa ajili ya kunirekebishia mambo yangu ya kiroho, alinipa mkono, nakumbuka neno la kwanza kutamka alisema Yesu, msamehe kijana huyu.

"Nilipotaka kuoa nikampeleka mke wangu ili amthibitishe, akaniambia mwanangu sawa, hiyo ilikuwa hata sijawa kiongozi kwenye kanisa la Songea nilipokuwa naishi,” anasema Noely.

Anasema, mwaka huohuo, Mtume na Nabii Mwingira alimpigia simu akamwambia anakwenda Songea anapeleka mchungaji, hivyo anaomba ushirikiano.

"Niliifanya kazi ya kanisa nikiwa kwenye ajira ya Serikali kama mkuu wa kituo cha kuzalisha vifaranga vya samaki.

"Baadaye nilihamishiwa Morogoro, nafasi ya katibu wa kanisa nilipoondoka Songea niliiacha nikawa muumini wa kawaida, baadaye nikateuliwa kuwa msimamizi wa kanisa.

"Katika kanisa kuna timu maalumu ya watafsiri, nikiwa Morogoro, Mtume na Nabii Mwingira alisali kanisani hapo na kuna wakati huwa anatumia lugha ya Kiingereza, siku hiyo katibu wa kanisa ambaye alikuwa mkalimani wake hakuwepo.

"Nilifungua ibada, ajabu siku hiyo hakuwa na mtafsiri, nikajikuta kipaza sauti kimebaki kwangu, alipoanza kuhubiri nikajikuta tu naanza kutafsri.

"Sikujua nini kilitokea, sio kwa sababu ya kufahamu Kiingereza, kwani unaweza kuwa unafahamu lugha lakini ukazungumza tofauti na ambacho mtume alikuwa akimaanisha, nilipata nguvu ya ajabu nikaifanya kazi ile kwa ubora, baba alifurahi na baada ya pale alinikaribisha kwenye kanisa lake kubwa la Mwenge ili nikamtafsirie," anasema.


Kuacha kazi

Noely anaeleza alivyoambiwa aache kazi aliyoifanya kwa miaka 11 ili ajikite kumtumikia Mungu, ambako hakuna mshahara.

"Aliniambia mwanangu nataka nikuachishe kazi, uje umtumikie Mungu moja kwa moja, hivyo nikazungumze na mke wangu kwanza kabla sijafanya uamuzi huo, ilinichukua wiki moja kutafakari na kufanya uamuzi," anasema.

"Nilijiuliza, kama niliweza kuacha muziki ambao ulikuwa unanipa pesa na umaarufu, na yule aliyenivuta niuache ndiye huyohuyo alinipa ajira ambayo niliipata nikiwa kanisa hili, na sasa anataka niache kazi nimtumikie, nikasema nafanya uamuzi mgumu.”

Anasema wengi hawakumuelewa, mwaka 2021 alipoondoka kwenye ajira wizarani na kupewa kazi ya kuwa kiongozi wa masuala ya kiroho akisimamia makanisa zaidi ya 670 duniani, wachungaji zaidi ya 700 na mitume 12 wa kanisa hilo yenye matawi wilaya zote nchini. Pia wapo nchi za Denmark, Uingereza, Marekani, DR Congo, Zambia, Malawi, Msumbiji, Kenya na mataifa mengine yakiongozwa na Mtume na Nabii, Mwingira.

"Napokea maelekezo kutoka kwa baba, pia katika kanisa kuna bodi ya mitume, nikiingia huko naenda kutoa maelekezo kutoka kwa baba na kile chombo kinanisimamia mimi, baba (Mtume na Nabii Mwingira) ndiye kiongozi mkuu, kisha kuna katibu mkuu, mhazini mkuu kisha kiongozi wa kiroho ambaye ni mimi na kiongozi wa masuala ya kiutawala (Mtumishi Vivian).


Matukio ya kiroho ambayo hawezi kuyasahau

"Upande wa kiroho yupo Mungu na yupo shetani, kila mmoja ana mambo yake, tunaona maadili yanavyoporomoka, hii ni changamoto ya watumishi wa Mungu, kazi yetu kubwa ni kuifundisha jamii na kuhakikisha mafundisho yetu yanarejesha maadili.”

Anakumbuka akiwa mwanamuziki, walipaswa kwenda Kigoma kufanya shoo, treni ilijaa wakakosa tiketi, hivyo wakalazimika kwenda hadi Dodoma ndipo wapande treni kuanzia pale.

"Treni iliyokuwa tupande tukakosa nafasi, ndiyo ilipata ajali Dodoma, na kuuwa watu wengi, na sisi tulikuwa kwenye ile safari, kukosa kwetu tiketi ndiyo ilikuwa pona yetu, lile tukio lilianza kunionyesha Mungu yupo upande wetu, tumefika Dodoma tunapanda treni nyingine kuna mabehewa mengine yana miili ya watu waliopoteza maisha kwenye treni ambayo sisi hatukuipanda.

"Kwenye utumishi, kitu ambacho sitokisahau ni kukubali kuacha kazi serikalini na kuja kwa Mungu, ilikuwa kipindi kigumu na kizito, si jambo rahisi kuacha mshahara, marupurupu, cheo na kila kitu.


Anavyomzungumzia Mtume na Nabii Mwingira

"Kufanya kazi na mtu mkubwa kama baba yetu, kwangu naona ni neema tu na kuwa na sikio la kusikia, kufanya kile anachotaka.

"Kwangu naona Mungu aliruhusu nipitie kwenye maisha ya kidunia, kisha Serikali hadi kufika huku, hakuna jambo kubwa kama kufanya kazi na mtumishi wa Mungu, ukiishi naye kwa mazoea unapata laana, wapo ambao wanafanya kazi kwa mazoea, ndiyo sababu kuna watu wanaasi.”

Akitoa historia ya kanisa hilo, anasema lilianza miaka ya 1994/95, baada ya Mtume na Nabii Mwingira kutokewa na roho mtakatifu na kumwambia anataka amtumie.


Atoboa siri ya jina la Critic

Japo sasa hapendi kulitumia, anasema lilitokana na tabia yake ya kutokubali jambo hadi alifikirie kwa kina, hakupenda kukurupuka, hivyo wenzake wakawa wanamuona anapinga sana, ndipo akaitwa jina hilo.

"Hata hivyo pinga yangu ilikuwa ni kwa manufaa, nikitaka kujiridhisha kwanza kabla ya kufanya kitu, ndiyo sababu hata kabla ya kundi kuvunjika, niliwaambia tutoe abamu ya pili ndipo kila mmoja aende kivyake wakakataa, nikawaambia uhai wa kundi unakwenda kuwa shakani, na kweli ndicho kilitokea," anasema Noely, ambaye ndiye alidizaini logo ya kundi hilo.