Namna mshindi wa BET anavyopatikana

Wednesday June 02 2021
bet PC
By Mwandishi Wetu

Mwimbaji wa Bongofleva, Diamond Platnumz amechanguliwa kuwania tuzo za Black Entertainment Television (BET) 2021 katika kipengele cha ‘Best International Act’ ambazo zitatolewa Juni 28 mwaka huu.

Hii ni mara ya tatu kwa Diamond kutajwa kuwania tuzo hizo baada ya mwaka 2014 na 2016,  safari hii anachuana na wasanii kama Wizkid, Burna Boy, Emicida, Headie, Aya Nakamura, Youssoupha na Young T & Bugsey.

Kufuatia hilo mashabiki wamekuwa wakiuliza namna ya kupiga kura.

Ukweli ni kwamba BET hawana mfumo wa mashabiki kupiga kura (popular votes) ili kumpata mshindi, bali kura zinapigwa na akademi yao (BET Awards Voting Academy) yenye watu 500 ambayo tayari wanakuwa wamewachagua wenyewe.

Akademi hii inajumuisha watu mbalimbali wenye uelewa kutoka kwenye muziki, media, bloga, burudani na hata mashabiki ambao hupita katika mchakato maalumu kabla ya kutambulika.

BET kupitia tovuti yao hutoa taarifa kuwa wanahitaji wanachama wa kupiga kura, kisha wanaambatanisha na fomu ya maswali ambayo anayehitaji kuingia katika hiyo akademi atayajibu. Maswali yanalenga kupima uelewa wa mwombaji kuhusu burudani na wale watakaojibu vizuri ndio wanaingia katika akademi hii.

Advertisement

Hivyo hii akademi ya watu 500 iliyopo chini ya BET ndio inapiga kura ni nani awe mshindi, hivyo ushindi wa Diamond utategemea namna hawa watakavyomtazama na si nje ya hapo.

Hata hivyo kuna kipengele kimoja tu ambacho ndicho kinatoa nafasi kwa mashabiki kupiga kura, nacho ni kile cha Viewers Choice Awards ambacho kura zake zitaanza kupigwa Juni 7 mwaka huu.

Hadi sasa Tanzania ina msanii mmoja pekee ambaye amewahi kishinda tuzo hiyo ambaye  Rayvanny aliyeshinda BET 2017 katika kipengele cha 'Viewer’s Choice Best New International Act' baada ya kuwabwaga wasanii kama Dave (Uingereza), Amanda Black (Afrika Kusini), Changmo (Korea Kusini), Daniel Caesar, Remi na Skip Marley (Jamica).


 Ugumu na wepesi kwa Diamond

Ukweli ni kwamba tuzo karibia zote duniani zina siasa zake, waandaaji nao huwa wana matakwa yao na malengo yao kiashara jambo linaloweza kutoa mwanya wa upendeleo kwa msanii fulani.

Leo hii Beyoncé ana tuzo 28 za Grammy wakati Rihanna ana tisa pekee, lakini ukweli ni kwamba Rihanna katoa nyimbo nyingi maarufu (hits) duniani kote kuliko Beyoncé. Hizo ndio siasa zenyewe.

Mwaka 2016 Diamond alipewa nafasi kubwa ya kushinda BET baada ya Wizkid 'kususia' tuzo hizo kwa madai haziwapi heshima wasanii wa Afrika na UK. Hata hivyo ushindi ukaenda kwa Black Coffee, DJ wa Afrika Kusini ambaye alikuwa hapewi kabisa nafasi ya kushinda, wengi walitazamia asiposhinda Diamond, basi atashinda Yemi Alade, AKA au Cassper Nyovest.

Hata hivyo hakuna ubishi kuwa Diamond toka mwaka 2016 aliposhiriki BET kwa mara ya mwisho, amepiga hatua kubwa kimuziki kitu ambacho kinaweza kuwa chachu ya ushindi wake.

Mathalani mwaka jana Diamond alishirikishwa kwenye albamu ya Alicia Keys 'ALICIA' kutokea Marekani na kusikika kwenye wimbo uitwao Wasted Energy. Alicia ameshinda tuzo saba za BET, huku akichaguliwa kushiriki mara 15.

Albamu hiyo ilikufanikiwa kushika namba moja kwenye chati za Billboard upande wa 'Top R&B Albums' mara ya baada ya kufanya vizuri katika mauzo. Hili linaweza na ushiwishi kwa akademi ya BET na kumchagua Diamond.

Advertisement