Nandy atangaza ziara ya kimuziki Marekani

Wednesday October 13 2021
nandpic
By Peter Akaro

Mwimbaji wa Bongofleva, Nandy ameweka wazi kuwa ataanza ziara ya kimuziki nchini Marekani, Machi hadi Aprili 2022 baada ya kuiahirisha kwa mwaka mmoja.

Hatua hiyo ya Nandy inakuja kipindi ambacho wasanii wengine wa Bongofleva akiwamo  Diamond Platnumz, Harmonize na Ibraah wakiendelea kufanya shoo za nchini humo.

Mapema mwaka jana mwimbaji  huyo alitangaza ziara yake aliyoipa jina la ‘Nandy USA Tour 2020’ iliyopangwa kuanza Mei 22 hadi Juni 20, 2020, lakini akalazimika kuifuta kufuatia mlipuko wa Uviko-19.

Si Nandy pekee aliyeahirisha ziara mwaka jana, Diamond naye alizifutilia mbali shoo zake alizopanga kuzifanya nchini humo kuanzia Agosti 21 hadi Septemba 21, 2020.

Kwa sasa wasanii wengine wakubwa Afrika wakiwamo  Wizkid, Burna Boy, Yemi Alade, Tiwa Savage, Tems wanaendelea kufanya shoo zao nchini Marekani ambapo baadhi walianza mwanzoni mwa Septemba mwaka huu. 


Advertisement
Advertisement