Nandy azungumzia alivyomlipa Rayvanny Show ya Songea

Saturday August 06 2022
nanda pic
By Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Wakati sakata la msanii Raymond Mwakyusa ’Rayvanny’ kutakiwa kulipa Sh50 milioni baada ya kupanda jukwaa la tamasha la Nandy Festival, Songea Mkoa wa Ruvuma likiwa bado halijapoa, Nandy amesema alimlipa msanii huyo katika show hiyo.

 Jana Ijumaa, Agosti 5, 2022 uongozi wa WCB kupitia meneja wa wasanii , Rikado Momo, alikiri kutaka Rayvanny kulipa fedha hizo.

Akihojiwa na Milard Ayo, kuhusu sakata hilo na namna gani alivyoweza kumshawishi kushiriki tamasha lake, Nandy amesema alipitia hatua zote za kimkataba kufanya naye kazi hiyo ikiwemo kumlipa.

“Kama ilivyo kwa wasanii wengine ninaofanya nao kazi, tulikaa na menejimenti yangu kumuhitaji Rayvanny,” amesema.

Hata hivyo, alisema awali aliongea kama kwa kumtania na kumuuliza..’Ray kwa nini usije Nandy Festival, ambaye naye kama aliipotezea fulani kwa kumjibu aaaa! Hayo mambo gani tutaongea...”

Lakini mchumba wake, Billnass baadaye alimshauri wafanye kweli kuongea naye ila wasitangaze iwe ni ya kushtukiza mashabiki, jambo ambalo lilifanikiwa baada ya kuzungumza naye na kumuhidi atakwenda na timu yake.

Advertisement

“Mwisho tulikubalijna na menejimenti, vigezo na masharti vikazingatiwa na akafika,” amesema

Alipoulizwa kama alifanya bure, kishkaji au alilipwa, Nandy alijibu, “hii ni biashara, alikuwa na timu ya watu 13 wameendesha gari hadi Songea, kwa hiyo nikaelewa biashara tuliyoongea ilipaswa iwe hivyo.”

Hata hivyo, alipoulizwa Rayvanny hajawahi kumwambia kutokana na bado kuwa WCB, labda na vitu hakutakiwa kuvifanya, Nandy alisema hapana na alizungumza naye yeye kama yeye na kama angemwambia hivyo basi angezungumza na uongozi wa WCB.

Wakati namna alivyopokea baada ya kusikia Rayvanny anapaswa kulipa WCB kutokana na kutumbukiza kwake kwenye tamasha hilo, amesema alijisikia vibaya na kuona kwamba amemuingiza gharama licha ya kuwa mpaka sasa hajamuuliza chochote kuhusu suala hilo.

 “Hata hivyo ilinipa moyo zaidi msanii huyo alipoandika kwenye Instastory yake kwamba yeye ni msanii huru na mtu yoyote anaweza akawasiliana naye kwa ajili ya kufanya kazi, jambo lililonipa ahueni,” amesema

Advertisement