Nandy na Zuchu kuonyeshana ubabe kimataifa

Sunday October 17 2021
Nandy pc
By Peter Akaro

Utakuwa ni mwaka mwingine ambao utaenda kubadili mtazamo wa wale mashabiki ambao wamekuwa wakiwapambanisha Nandy na Zuchu ndani ya muziki wa Bongofleva kutokana na wote wawili kufanya vizuri.

Mashabiki hao watapata jawabu baada ya ushindani wa mstaa hao wa Bongofleva sasa unapimwa katika ngazi ya kimataifa kufuatia wote kutajwa kuwania tuzo mbili kubwa na kuwekwa katika vipengele viwili tofauti pamoja.

Katika tuzo za All Africa Music Awards (Afrima) 2021 ambazo zinatarajiwa kutolewa kati ya Novemba 19 na 21, 2021 Lagos, Nigeria, Nandy na Zuchu wapo katika kipengele kimoja cha msanii bora wa kike Afrika Mashariki.

Hata hivyo, Nandy alishawahi kushinda tuzo hiyo katika kipengele hicho mwaka 2017, hivyo Zuchu anaweza kupindua meza au Nandy akaendeleza ubabe. Lakini pia wanaweza kukosa wote maana kuna washindani wengine wakiwamo Rosa Ree, Spice Diana kutoka Uganda na Karun kutoka Kenya.

Wiki hii wawili wao wametajwa tena kuwania tuzo za African Muzik Magazine Awards (Afrimma) 2021 ambazo hutolewa nchini Marekani, na wamewekwa tena kipengele kimoja cha msanii bora wa kike Afrika Mashariki. Hata hivyo wanatarajia kupata ushindani mkubwa kwa wasanii kutoka Kenya, Tanasha Donna na Nadia Mukami.

Nandy pcc
Advertisement

Ushindani wa mashabiki wao unaanzia hapa, wasanii hao wawili mwaka jana walishinda tuzo hiyo, Nandy akishinda katika kipengele cha msanii bora Afrika Mashariki, huku Zuchu akishinda kama msanii bora anayechipukia.

Utakumbuka Zuchu amekuwa akifanya vizuri kwenye muziki tangu Aprili mwaka jana alipotangazwa kuwa chini ya WCB Wasafi, huku Nandy aking’aa tangu mwaka 2016 baada kufanya vizuri katika shindano la Tecno Own The Stage nchini Nigeria.

Maeneo 12 ulipo ushindani wa Nandy na Zuchu


1. Zuchu ndiye msanii wa kike wa kwanza kufikisha watazamaji milioni 100 katika mtandao wa YouTube Tanzania na Afrika Mashariki ambapo sasa wamefikia milioni 240.3, baada ya mwezi mmoja, Nandy naye akafanya hivyo na sasa amefikisha milioni 130.2.


2. Nandy alifanya vizuri katika shindano la kwanza la karaoke barani Afrika, Tecno Own The Stage nchini Nigeria, aliposhika nafasi ya pili na kuondoka na Sh36 milioni, huku Zuchu akishindwa kufua dafu kwenye shindano hilo.


3. Zuchu ndiye msanii wa kike anayeongoza kwa wafuatiliaji katika mtandao wa YouTube Tanzania akiwa nao milioni 1.5, Nandy anashika nafasi ya pili akiwa nao 914,000.


4. Hadi sasa Nandy tayari ana albamu mmoja, ‘The African Princess’ iliyotoka Novemba 2018, pia ana Extended Playlist (EP) mbili, ‘Wanibariki’ (2020) na ‘Taste’ (2021), ilihali Zuchu hana albamu ila na EP moja, ‘I Am Zuchu’ iliyotoka Aprili 2020.


5. Mama mzazi wa Zuchu ni Khadija Kopa ambaye ni malkia wa muziki wa taarabu nchini, huku baba mzazi wa Nandy, Charles Mfinanga amewahi kuwa DJ.


6. Zuchu ni shabiki wa timu ya Simba na mwaka jana alitumbuiza kwenye tamasha la timu hiyo ‘Simba Day’ huku Nandy akiwa ni shabiki wa timu ya Yanga na mwaka huu ametumbuiza kwenye tamasha lao ‘Siku ya Mwananchi’.


7. Nandy anajisimamia mwenyewe kimuziki chini ya chapa yake, The African Princess huku Zuchu akisimamiwa na WCB Wasafi ambayo ni lebo ya Diamond Platnumz.


8. Mwaka huu Nandy kafanya tamasha lake ‘Nandy Festival’ katika mikoa ya Kigoma, Mwanza, Dodoma, Arusha, Dar es Salaam na visiwani Zanzibar, huku Zuchu akifanya shoo yake kubwa ‘Home Coming’ nyumbani kwao, Zanzibar.


9. Wasanii wa kimataifa waliofanya kolabo na Nandy ni Willy Paul (Kenya,) Joeboy (Nigeria) na Koffi Olomide (DR Congo), Zuchu akiwa na Joeboy (Nigeria), Olakira (Nigeria) na Spice Diana (Uganda).


10. Hadi sasa hawa ndio wasanii waliobahatika kupigiwa simu na Rais Samia Suluhu Hassan wakiwa katika shoo zao. Nandy aliipokea simu ya Rais akiwa Dodoma katika tamasha lake la ‘Nandy Festival’, huku Zuchu akiipokea akiwa Zanzibar katika tamasha lake pia la ‘Home Coming Show’.


11. Baada ya Zuchu kumzidi namba upande wa YouTube, Nandy naye kaja kupindua meza upande wa Instagram na Facebook, ana wafuasi milioni 5.6 Instagram, Facebook milioni 2.1, huku Zuchu akiwa na milioni 3.5 Instagram na Facebook milioni 1.2.


12. Nandy ana tuzo nne kubwa katika maisha yake ya muziki, mbili kutoka Afrima (2017 & 2020) - Nigeria, nyingine toka Afrimma (2020) - Marekani, na Maranatha Awards (2018) - Kenya, huku Zuchu akiwa na moja tu, Afrimma (2020) - Marekani.

Matokeo ya tuzo wanazowania yataondoa sintofahamu ya mashabiki wao kujua nani mkali zaidi ya mwenzake.

Advertisement