NDANI YA BOKSI: Acha lopo lopo... weka pesa mezani upate penzi la moyoni

Sunday July 17 2022
NDANI YA BOKSI PIC
By Dk Levy

Alikuwa mzuri. Ndiyo! Itoshe kusema Khadija alikuwa mzuri. Yap! Mchukue Hamisa ndio kimo chake. Rangi yake haihitaji ‘filta’ au ‘editingi’ wala ‘snap’. Sifa nyingine ni zake peke yake.

Kwa hapa Bongo hakuna pisi wa mfano wake. Niamini mimi!

Natamani ‘Vieiara’ ziwepo hata katika maisha yetu ya kila siku. Ili tukio la kumtokea Khadija lijirudie mara kwa mara. Kwa faida ya matomaso wa kizazi hiki, ambao ukiwaambia lolote la zamani hawaamini kwa na uzuzu wao.

Naweza kuongea maneno mengi ya uongo. Lakini pindi linapokuja suala la Khadija, nanyoosha maelezo na sidanganyi wala kusahau kitu juu yake. Nilimpenda kinoma kabla hata hajanikubalia rasmi. Nikamuweka moyoni na akilini jumla jumla.

Wakati namuona mara ya kwanza, tayari mie nikawa nimetenga bajeti yake. Kuanzia kula, kulala, kuvaa na matumizi ya kawaida. Nikajivisha jukumu la ulezi kibwege tu na wala sikujali. Hizo ndo zangu nikiielewa pisi kali. Nikabaki nasubiri utekelezaji wa ahadi, endapo akikubali upumbavu wangu wa hisia kali juu yake. Kama zali, mtoto nilipomuimbisha akatoa ahadi ya kunipa jibu wikiendi ijayo. Tayari nikaanza kujenga picha juu yake hapo hapo na mkeka wa penzi lake ukitiki tu, Jumamosi natimba naye Twanga Pepeta kula vyombo! Chimbo la mjini lilikuwa ni Mango Garden Kino au Makumbusho kila Jumamosi. Jumapili ni Leaders Club, Msasani na pale TCC Chang’ombe.

Kote huko ni mwendo wa ‘laivu bendi’ tu. Twanga Pepeta na Fm Academia ndo zilikuwa ‘Supa brandi’. Maeneo hayo ndiko ambako ungekutana na pisi za mjini. Nyakati zinapita! Ujue kuna watu hujiona wao ndio kila kitu na wamemaliza dunia. Nikawa miongoni mwao, kitendo cha Khadija kuahidi tukutane wikiendi tu. Hapo hapo nikaanza kuvimba sana mjini kama fisadi la EPA.

Advertisement

Watu wengine ambao hujisikia kama nilivyokuwa najisikia. Ni wanaojua kuzungumza Kiingereza hata kama ni ‘brokeni’ na wamiliki wa toleo mbalimbali za simu za ‘aifoni’. Na waliochukua masomo ya sayansi sekondari na vyuoni.

Wanaosomea kozi mbalimbali za uhandisi. Hawa hata ukiwakuta huku mtaani bila ajira, hujihisi tayari wao wamepatia maisha. Wahitimu vijana wa UDSM. Na wale walioishi sana Marekani au Uingereza na kurudi Bongo.

Wenye ndinga hasa hizi ‘krauni’ na kupanga nyumba nzima, Mikocheni, Sinza au Mbezi. Waliokuwa wanavaa tumiwani kipindi hicho skonga. Na wanaoishi Dar halafu wakaenda zao mikoani, nao hujikutaga sijui ni kina nani vile.

Kuna ‘stafu’ wa bandarini, airport na TRA. Utadhani ndo wenye mamlaka kuliko Rais Samia. Kuna wale ndezi pori wa kujiita wazee wa ‘koneksheni’. Wakiwa na video ya ngono ya supastaa yeyote. Hujiona wao ndo wamepatia maisha kuliko Mo.

Daslama washamba bado wapo wa kumwaga tu. Vitu kibao vimetoweka mjini, lakini washamba wameweka makazi ya kudumu hapa. Unadhani kwa wakazi wa Dar, mara ya mwisho kuona kipepeo au panzi, kunguru wenye doa jeupe shingoni lini? Lakini washamba wamejaa tele.

Wadudu waliojazana kila kona ya jiji hili ni mbu, inzi, sisimizi, mijusi au mende. Hii ni ishara kuwa jiji limetawaliwa na uchafu kila kona na kila nyumba. Hata uwezo wa kunguru weusi kama koti la jambazi wa Bongo movie, ni ishara ya uchafu mwingi. Maana mchongo wao mkubwa ni kutafuna mizoga na kuiba vitoweo. Kila kitu mjini hapa hutoweka na tunaletewa vitu vya ajabu.

Zamani kila baada ya mtaa kulikuwa na wazee wanaocheza bao na kunywa kahawa.

Hivi sasa kila baada ya mtaa kuna ‘gesti’ na wazee hao hao ndo huingia na vibinti vidogo vidogo. Hata minazi imekuwa adimu, michongoma pia inatoweka taratiibu. Hivi leo mitaani kumejaa makopo yaliyotumika kwa vinywaji vya kuongeza nguvu. Mbao siyo kwa vitanda, kabati na jeneza tu, sasa hujengea vibanda vya kuuzia pombe. Zamani ukitembea kila mtaa kuna mama muuza bagia, vitumbua au visheti. Leo hii kila mtaa kuna mama ana kiduka cha kuuzia pombe. Zamani kila nyumba ilikuwa na kibaraza na ungewakuta kina dada wakisukana. Leo hii kila kibaraza cha nyumba kimegeuzwa fremu ya duka. Vijiwe vya mafundi saa, viatu na wachonga funguo na mihuri, sasa ni stendi za bodaboda.

Magenge ya bamia na pilipili hoho, yamegeuka vibanda vya miamala ya pesa. Zamani ungehaha kusaka namba ya totozi, leo unapata popote iwe njiani au kwenye daladala. Maendeleo ni kama mafuriko, huja na vitu vingi na huondoka na vitu vingi. Daslaama ya zamani siyo sawa na ya sasa. Ukifika jitahidi kuishi sehemu ambayo ukipanda basi moja unafika kazini kwako. Siyo unaenda kuishi Goba, wakati kazini kwako ni Temeke, utajuta kuijua Dar kijana.

Mikoani utatembea kwa miguu sehemu moja mpaka nyingine freshi tu. Dar hii ukitembea utaingia kwa nani wakati unamwaga jasho mwili mzima? Ogopa bro! Mkoani utachuma mboga mboga bustanini kwa jirani yako yeyote. Safi tu! Dar hii nyumba zimebanana kama miguu ya jongoo, utalimia wapi? Ujue Dar wapangaji ni wengi kuliko wenye nyumba, utamuomba nani ukalale kwake? Hakuna!

Vijana wanashinda kwenye ‘betingi’ za soka kutwa nzima. Mikeka ndo inaendesha maisha yao. Hukatazwi ukitaka wewe jiongeze njoo, utajua namna watu wanavyoishi. Dar hapa watu hawalali njaa, bali wanachelewa kula. Niamini bro!

Na totozi za Dar hazieleweki zinataka nini au zinataka mwanamume wa aina gani. Mara anataka wa ‘siksi paksi’, mara mrefu, sijui ‘jentlomani’ mara sijui manini. Ni uongo mtupu tu na kuchelewesha hukumu ya hakimu mkazi. Ni pesa!

Enyi wageni tunawatangazieni rasmi, kwamba simamieni kwenye suala moja la pesa tu. Pesa ndio msingi wa penzi penzini, mahaba habani, huba hubani na ulaazizi. Hakunaga penzi la kweli, ila pesa ndio huwapa hisia za kweli. Ukileta uinjilisti inakula kwako. Yaani meseji ya muamala huvutia zaidi kuliko ahadi ya ndoa na tukio la kuvishwa pete. Ndio maana vizee vya mjini hapa huitwa ‘bebi’ kila kona, na vinajidekeza na makunyazi yao usoni. Vinamiliki totozi kali zaidi ya mabishoo.

Ndiyo! Kwa sababu havina mkono wa birika. Sasa wewe njoo Daslama hii ulambelambe lipsi na kujivimbisha kifua. Utaishia kuwa baunsa wa kina Konde Boy. Warembo huvutiwa na sauti za ATM kuliko kupeleka barua ya posa kwao.

Hivi mnaolalamika kuombwa pesa, ni kwa mpenzi wako mmoja mmoja au kwa lundo la totozi zako? Msichana mmoja anaweza kuomba pesa kiasi cha kuwa kero kiasi hicho? Au ni harakati zenu za kipimbi ndio zinafanya mpigwe vizinga? Kama unao wanne wote wakiishiwa gesi, hapo ni laki mbili na ushee lazima zitakutoka. Upo mjomba?

Advertisement