Ndani ya Boksi: Kuna ‘ushosti’ wa VPN na video za wasanii

Teknolojia inazidi kupata maarifa sambamba na watu wengi kwenye jamii wanavyopoteza busara vichwani. Ukitaka kujua hilo zama mitandaoni utazame upotevu wa fikra na busara kwa watu wengi vichwani kupitia maandishi yao.

Wanamuziki na watengenezaji wa video hivi sasa wengi wako vizuri. Ni ngumu kukutana na video mbovu kwa sasa.

Zamani nyimbo zilikuwa nzuri kuliko video, kitu ambacho wasanii waliamini kufanya video ni kuharibu wimbo wenyewe. Hatukuwa na vifaa vya kisasa na watengenezaji wenye elimu na kazi hiyo. Wengi walifanya kazi kwa mizuka siyo taaluma.

Leo ukileta video za kipaimara na komonio kama siyo ‘kicheni pati’, hutapata kazi za wasanii na vituo vya runinga haviichezi video yako. Muziki ni shamba lenye mavuno kuliko sanaa yoyote Bongo kwa sasa. Muziki una utajiri na ajira za kutosha kama migodi ya madini.

Shilole alishtuka mapema kabla ya jua la utosi kwenye filamu. Akapita kushoto akaliacha soko la filamu kulia kwake. Kwenye sanaa ya filamu hakupata anachopata kwenye muziki. Ni dhahiri kwa sasa muziki una malisho mazuri.

Soko la filamu limefifia. Hata mvuto kwa jamii siyo kivile. Ndiyo maana wasanii wengi wanapiga pesa kwa vitu vya nje ya sanaa. Jacquline Wolper utamsikia kwenye biashara za mishono ya nguo na dili nyingine nje ya filamu, wengine michongo yao kwenye siasa.

Katika mazingira haya ni ngumu Wema kufurahia kuitwa msanii wa filamu kama ambavyo Shilole anavyochekelea kuitwa muuza chakula. Kuna wasanii wameamua kushughulika na mambo mengine. Kajala taswira na umbo lake hulioni kwenye filamu.

Kuna kitu kipo katika muziki na kwenye filamu hakipo. Kuna kitu kimepwaya kwenye filamu kwenye muziki kimejaa. Tuache hayo. Biashara yoyote inapokubalika huwezi kuzuia ushindani wake. Katika muziki hali iko hivyo pia. Upo ushindani kwenye utunzi, shoo mpaka video.

Kutokana na hilo ndiyo maana wanamuziki hivi sasa wanapanda ndege kufuata ubora wa video Afrika Kusini na kwingineko. Lengo ni kuteka soko la kimataifa kwa video nzuri. Wachache wamefanikiwa. Safari ya Diamond kimataifa ilifunguliwa na video kali.

Achana na midundo. Puuzia sauti, ‘melodi’ na shairi. Video ya wimbo wa Number One ilikuwa ni ya kiwango cha juu. Kupitia ubora wa video kama ile ilikuwa rahisi kumshawishi Davido akaelewa. Ndicho kilichotokea kwa Iyanya na wengineo aliofanya nao kazi.

Mbali ya kufanya kazi na nyota wa Kinaijeria na kwingineko, pia mfereji wa kutiririsha tuzo za kimataifa ulizibuliwa na video hiyo. Yawezekana kulikuwa na mengi zaidi yaliyochangia kufanya nao kazi, lakini ubora wa video ile ulichangia kwa kiasi kikubwa.

Ila kama ilivyowahi kutokea katika Bongo Movie, kuna kitu kibaya kinaanza kushamiri kwa wasanii wengi wa Bongo Fleva. Zamani Bongo Movie waliposema filamu ya kimataifa, ilikuwa filamu ambayo huwezi kuangalia na wazazi au mtu unayeheshimiana naye.

Waliamini filamu ya kimataifa ni uzungu kuanzia matendo, mavazi, ‘kava’ la DVD, jina la filamu na viingereza vingi vya kunyapianyapia ndani. Ni kama leo katika Bongo Fleva. Video nyingi zinazoitwa za kimataifa basi ujue ndani kuna vimini na mikao ya ajabu na nguo za faragha.

Kutazama video zao hivi sasa lazima utazame kushoto na kulia ili ujihakikishie kuwa hakuna mtu unayeheshimiana naye. Ubunifu umekwisha au wanakurupuka bila kujua dhana ya video ya kimataifa. Wao wanaamini ni kuvaa utupu na matendo ya kingono.

Unaweza kuimba mtupu kama ulivyozaliwa na bado ukaonekana ‘loko’. Unaweza kuimba ukijifunika kanga na vitenge na ukaitwa wa kimataifa. Kuna uhusiano gani wa vichupi katika video na ukimataifa mnaoutaja? Miriam Makeba ni wa kimataifa, mbona hana video za utupu?

Msijitoe akili kwa kuacha tupu zenu wazi kwenye video mkidhani mtapaa na kuwa kama Rihanna. Mnajidanganya. Kuna kitu mnatakiwa kufikiri. Mmebeba maana na heshima ya Taifa. Nyimbo na video zenu zinatoa tafsiri bora nje ya mipaka ya taifa hili.

Tanzania ni Taifa linalosifika kwa maadili na heshima. Mnahitaji kubadilika katika fikra ili msifanye tukaonekana kama wote ni wale wale. Sisi wote wajinga, lakini sio wajinga wa kitu kimoja. Kupanuka kwa teknolojia lisiwe lango la kuondoa maadili kwenye jamii yetu.

Kwa siku kadhaa Waziri wa Habari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Nape Nnauye amekuwa akilia na VPN. Najiuliza VPN na video za wasanii wetu kipi kinaharibu maadili? Kimsingi kama kweli VPN inapigwa stop Bongo ili kulinda maadili, basi tuelewe kwamba VPN na kile kinachoendelea kwenye video za wanamuziki wetu ni kulwa na doto.