Ndani ya boksi: Masponsa na panyarodi wote kero mjini

Muktasari:

  • Mitihani mingi kwenye nafsi zetu. Kuna pisi naihusudu mpaka moyo wangu unapata shaka. Unashindwa kuelewa kati ya Vicky na Khadija yupi zaidi. Khadija nilimpenda, nampenda na nitampenda.

Mitihani mingi kwenye nafsi zetu. Kuna pisi naihusudu mpaka moyo wangu unapata shaka. Unashindwa kuelewa kati ya Vicky na Khadija yupi zaidi. Khadija nilimpenda, nampenda na nitampenda.

Sasa huyu Vicky sijui katokea wapi jamani. Nimetokea kumpenda na dalili zinaonyesha nitampenda sana tu. Yaani moyo naupa tabu hapa jinsi ya ‘kubalansi shobo’ zangu kwa hawa viumbe. Nyie niombeeni tu.

Nipo kwenye umri ambao kiwango cha tamaa ya utajiri ni kikubwa sana sawa na kiwango cha tamaa ya kuwa na familia. Ni kaumri kanakoleta mvi nyingi, kisukari na tezi dume badala ya pesa. Ogopa sana!

Ni umri ambao mabinti hawakutaki na ‘mashuga mami’ hayakutaki. Ni umri ambao bila umakini utakuwa rafiki wa mashuka mekundu ya waganga kuliko madhabahu. Umri wa liwalo na liwe potelea potee.

Wajanja tulishasoma gemu kitambo. Tulifahamu huu msala upo mbele yetu, tulijiandaa kisaikolojia. Kama kuna mandezi yanategemea masela ‘tudate’ na ‘laifu’ yatadata yenyewe. Sisi paka wewe!

Nimeachika tena. Nimeachika Mimi.

Hizi ndo kauli ‘zinazotrendi’ kwenye nyoyo za vijana wengi. Hakunaga mapenzi ya kugandana, hayo ni mambo ya kale. Karibu chama la bachela ukimpenda ni leo leo tu. Dunia imebadilika. Uhusiano ni kama fasheni. Leo na huyu kesho na yule. Wapo wa kuoana mchana na usiku wanaachana. Penzi la kugandana na kutimiza miaka 50 ya ndoa ‘nau deizi’ halipo tena.

Ni kawaida kabisa msichana mdogo kumiliki wanaume watatu na kuwaita bebizi. Kijana wa kiume kuteka nyoyo za wasichana hata sita au saba na kuwaita sweetie, siyo ajabu kabisa ndio maisha ya sasa!

Ukiuliza jibu lake ni; “Akiba, ukitemwa una sehemu ya kutolea machungu yako.” Dunia hii ya kidijitale kumpata muaminifu ni sawa sawa na kusaka bikira kwenye danguro la makahaba. Maisha yapo tenge.

Kuna vifo vingi hutokea kwa wivu wa mapenzi. Hakuna upendo wa dhati, wanasema mjini cha bure vumbi tu. Kama kapuku utaishia kuziita shemu totozi za mjini ama ukubaliane kuwa mpenzi mtazamaji. Na ukiwa na pesa utazipanga totozi kama abiria wa mwendokasi. Ndio maisha ya sasa. Siyo suala la wazi lakini ndio ukweli, kwamba dunia hii ya kileo penzi ni pesa. Mambo ya muonekano na mvuto peleka stejini.

‘Sponsa’ wana nguvu kuliko majanki. Wao ndiyo chanzo cha kuharibu uhusiano wa mapenzi kwa vijana wengi. Kwa tamaa zao za ngono, au tamaa za totozi kwa suala la maisha flani hivi mazuri na amazing.

‘Mabishoo’ nao wanataka mtelezo kwa ‘mashuga mamizi’. Hutumika kingono ili walelewe, wamegeuza ngono kama ajira rasmi. Ni kwamba vijana kwa wazee wengi wao ni ‘ziro breini’ kwa kipindi hiki. Wanaishi ishi tu kijuha.

Kwa namna hii ni vigumu kudumu penzini. Ndio maana mnatemena leo kesho yupo kwenye uhusiano mpya. Bro usistuke, unatakiwa utambue kuwa kabla hujamtema na yeye pia alikuwa na uhusiano mwingine wa chini ya kapeti.

Kwanza siku hizi ni ushamba kuishi na mpenzi mmoja. Hata wale wa kwenye ndoa wana vidumu mitaani pengine kuliko wasio na ndoa. Ndio dunia ipo huko, uaminifu ulibaki karne ya 20. Hata pisi ‘haziinjoi’ kabisa kuishi na mwamba muaminifu. Mara zimekukuta upo baa na malaya. Yaani timbwili na vituko ndio wanataka. Wewe kariri kufa na kuzikana.

Yaani atoke kwao kuja kwako kwa ajili ya kufa na kuzikana? Warembo wa hivyo waliondoka na Azimio la Arusha. Leo wanakuja kuchuma mali na kusepa. Na wanatuzika na siyo kuzikana. Angalia idadi ya wajane ndiyo utaamini.

Kuna maisha nje ya mitandao. Na siku hizi simu zinatunza siri kuliko mke au mume. Ukitaka kujua hili jaribu kuchukua simu ya mkeo ama mumeo, uone kama patakalika hapo. Teknolojia inajenga na kuharibu zaidi.

Maendeleo yaende sawa na elimu ya afya ya akili. Ili tupunguze matukio ya ukatili kwenye uhusiano. Maumivu ya kuachwa na kutendwa yanayofanya watu wauane hayataisha. Kwani ni ngumu kuwabadilisha wote waishi kilokole.

Tunakoelekea mapenzi yanaweza kuwa hatari zaidi na chanzo kikuu cha vifo kuliko vita na ajali. Maana mpaka dakika hii mapenzi yanaua kwa magonjwa, wivu na ‘stresi’ za kimkurabita. Noma sana!

Mapenzi yanataka kuharibu amani yetu. Tangu na tangu, Tanzania ni nchi ya amani. Sauti za mitutu ya bunduki na mabomu ni jambo geni. Lakini leo watu wanachinjana na kupigana risasi kisa mapenzi.

Kwa nini amani ipotezwe kibwege tu na wahuni? Hata hawa Panyarodi ambao ni vijana wasiopenda amani. Wakiingilia kazi ya Mungu kukatisha uhai wa watu. Kukaba na kupora mali za watu. Ukizama ‘dipu’ chanzo kikuu ni mapenzi.

Wanatembea kwa makundi huku wakiwa na silaha. Wanapora mitaani na kuvamia watu majumbani. Kama makarani wa sensa walivyotembea mitaani nyumba kwa nyumba. Ndio wanavyofanya nao mtaa kwa mtaa.

Ni vijana wadogo, ambao walitakiwa kuwa mashuleni. Kwenye viwanja vya soka kama siyo ‘lokesheni’ kuandaa filamu. Wameamua kufanya dili la kishetani kuua na kukaba watu mitaani. Umri wao hauendani na matendo yao.

Unajiuliza kwa umri wao wanataka mali na pesa nyingi kwa ajili ya nini? Hawajengi nyumba, hawalipi ada za watoto wala pango la nyumba. Nini sasa? Ni kutaka pesa ya kula bata tu, na bata haliendi bila warembo.

Tumezoea kusikia wakazi wa mikoa mbalimbali wakitamani kufika Dar. Lakini tunakoelekea hata waliopo Dar wanatamani kuondoka. Kutokana na matukio ya ukatili mauaji, uporaji na kuumizana kimapenzi. Dar, kuna kero nyingi . Ukiachana na Panyarodi hata masponsa ni kero kwa vijana. Masponsa wengi ni watu wazima, wana nguvu ya kiuchumi kuliko vijana. Matokeo yake humiliki warembo wote wazuri. Sasa vijana wameamua kutafuta pesa kihalifu, ili wakaishi maisha ya kisponsa. Hawajui kuwa pesa na mali hupatikana kwa bidii, kujituma na ubunifu kwenye kazi za halali na siyo vinginevyo. Inasikitisha sana. Kabla ya kumfanyia unyama mtu na kumpora mali yake. Inapaswa kujua kuwa hata yeye anatafuta ili ajiokoe kimaisha. Maisha bora hayatafutwi kwa kukaba na kupora watu. Na Dar watu hushindana kwenye matumizi kuliko utafutaji. Pongezi kwa Jeshi la Polisi kuwadhibiti, ingawa hatuwezi kuiachia Serikali pekee kwa sababu chanzo ni jamii yetu. Tulibebe kama tatizo kuu kuanzia ngazi ya familia na jamii kwa ujumla.

Sponsa niachie beb’angu nisigeuka kuwa Panya Road.