Ndani ya boksi: Nasimama na Ommy Dimpoz "Pozi kwa Pozi'

Sunday September 18 2022
omy pic
By Dk Levy

Aboubakar Shaaban Katwila muite ‘Q Chief. Unamkumbuka huyu mwamba wakati anaibuka kisanii? Alikuwa juu kama nyota. Juu kama theluji pale kwenye kilele cha Kili na mawenzi. Ogopa sana.

Alitamaniwa na totozi za ushuani na uswahilini. Alihusudiwa na ‘mashuga mami’ na mashangazi ya ‘tauni’. Na zaidi masela walimpenda na kuvutia kamera za wana habari. Q Chief yule siyo Chillah huyu.

Sauti yake ilitikisa spika za mageto ya masela na masista duu. Kwenye mataa ya ‘Salenda’ na Morocco au Magomeni. Ungeziona pisi kali za wakati ule zikitisa vichwa kwenye mikoko yao na ngoma na Q Chief.

Wakati ule madem wenye magari, walihesabika kama nywele kwenye kichwa cha January Makamba. Hata mabishoo waliopushi ndinga pia nao walikuwa wachache. Lakini maisha yalikuwa rahisi sana. Ukiacha sauti, uwezo wa kuimba na uso wenye ubora kabla haijaguswa na vilevi vya vya mjini. Mtoko wake ulisindikizwa zaidi na stori nyuma yake iliyogusa sana mioyo ya watu. Q Chief alitupa burudani yenye hisia za maumivu.

Alitulilia kuwa alitelekezwa na mshua wake. Na akatulilia kuwa alimpoteza Bi Mdanga kwa sababu ya mimba yake. Mimba iliyofanya mama yake atimuliwe kwao baada ya kutimuliwa skonga.

Yaani Bi Mkubwa alitoswa na mshua wa Chillah. Akatimuliwa na shuleni na zaidi nyumbani pia wakamtema. Mimba iliyomzaa Aboubakar Shaban Katwila Q Chief. Presha na mawazo yakaondoa uhai wa mama yake.

Advertisement

Hii stori kila mtu ilimgusa kwa nafasi yake. Hata mie, licha ya kufahamiana kitambo toka enzi za ‘Zero Brain’ pale Posta Mpya. Enzi za Mzimuni Family na goma la Mpiga debe. Lakini pindi alipotoa “Ulinikataa”. Nilidata!

Abdul Naseeb ‘Daimond Platinumz’. Achana na ‘Nenda Kamwambie’, weka kando penzi lake na Wema. Stori za kuwahi kutelekezwa na baba yake, ni kitu kilichofanya atuame midomoni mwa watu mpaka hapa juzi kati.

Stori za masela hawa kutemwa na washua wao. Na kwamba mama zao ndio walikomaa mpaka wanapata maisha. Mosi, ziliwapa nguvu, kina dada wengi kuendelea kukomaa na malezi ya watoto bila baba zao.

Pili, ziliwashtua washua kibao walio kata ringi. Na kukumbuka umuhimu wa kutoa mahitaji kwa watoto wao ili kesho yasiyewakute yaliyowakuta wenzao. Na zaidi taasisi zetu kama Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) zikatolea macho zaidi.

Kuna wasanii wengi Afrika na Ulaya, ambao walilia kutemwa na washua. Na zaidi katika dunia ya sasa vijana wengi hulelewa na upande mmoja wa mama kwa sababu nyingi tu. Siyo tu kutelekezwa na mshua.

Kuna dada ambao umri umesogea sana bila ndoa. Huamua tu kuzaa na yeyote hata mume wa mtu. Na kuna ambao wakiwa na elimu nzuri ama ajira tamu, mshahara huwa bora zaidi kuliko joto la mwanaume.

Wanaamua kwa makusudi kuchagua wa kuzaa naye na siyo kuolewa naye. Wakati wanaume tunavyopata pesa nyingi ndivyo tunavyoongeza totozi nyingi zaidi. Kina dada kwao ni tofauti kabisa. Mwanamke anapopata pesa nyingi zaidi, ndivyo ambavyo huwakataa wanaume wengi zaidi. Yaani hutaka kuishi kivyao. Kifupi umaskini wao kwa kiasi kikubwa huchangia madem kuingia kwenye ndoa.

Na kutokana na uchache wa masela wenye uwezo wa kutunza familia. Kina dada wengi huamua kujiingiza kwenye ngono zembe na waume za watu. Akiamini kuwa hata akimzalia atatunza mtoto.

Hizi ni mojawapo ya sababu nyingi za watoto kulelewa na pande moja ya kina mama zaidi. Ingawa wale wa kutelekezwa na wanaume ni wengi zaidi kuliko wanaozaa kwa kupenda kulea kivyao. Dunia ipo hivi.

Kwa sasa ongezeko la kina mama wanaolea watoto kivyao ni kubwa. Tumewapa na jina la ‘Singo Maza’. Maisha yao ni liwake jua au inyeshe mvua wao wapo mtaani, ili tu wapate chakula na watoto wao.

Kuna sababu nyingi mitaani hutetea wanaume wenye tabia hizi. Wengi husema ukorofi wa wanawake na kelele majumbani ni chanzo. Wapo wanaodai ugumu wa maisha pia na ufinyu wa ajira ndio chanzo. Ukweli ni kwamba huwezi kukimbia familia kwa sababu ya kelele za mke, ugumu wa maisha. Kama wewe mtu mzima unaona maisha ni magumu, vipi kwa hao watoto wako unaowatelekeza?

Jamii haipaswi kuacha hili liendelee kuota mizizi. Watoto huhitaji penzi la baba na mama. Wazazi wanaweza kutengana kivyao, lakini huwezi kutengana na watoto wako. Masela tutafute pesa kinguvu tule na watoto wetu.

Achana na mke wako, lakini usiache kuhudumia watoto. Kutotoa huduma kwa watoto ni kuwapa uchungu kina mama. Na huwapelekea kupandikiza chuki kwa watoto juu ya baba zao. Hii ni mbaya zaidi na hasara kubwa uzeeni.

Siyo ajabu leo mtoto kumkana baba. Ni pandikizo la chuki za maisha ya taabu na dhiki wakiwa na mama zao pekee. Achana na kelele za juu ya baba yake Ommy Dimpoz, ambazo zimeteka mtandaoni.

Yote chanzo ni makosa ya washua kwa watoto wetu. Tunatemana na mama zao na kuwasusa na wao pia. Mtoto anapata akili anaona mama tu ndio anampa kila kitu. Kuanzia nguo, kula mpaka nauli. Unategemea nini? Hao ni baadhi ya mastaa wa muziki waliokutana na maisha hayo. Kuna wanasoka na wanasiasa pia. Ajabu wazee hujitokeza pindi watoto wakifanikiwa kimaisha. Na hao ni wachache ambao hujitokeza kutaka msaada. Kuna vijana wengi ambao bado ni malofa, wazee wanaendelea kuwapotezea. Jambo la msingi ni kwamba, ugomvi wa wazazi isiwe fimbo kwa watoto.

Kabla kumtazama kwa jicho lako hilo Ommy Dimpoz, itazame jamii yako inayokuzunguka. Ni kama vile sasa tumerasimisha wanaume kutelekeza familia. Huku wakiwaachia kina mama wahangaike na watoto.

Nasimama na Ommy Dompoz...

Advertisement