NDANI YA BOKSI: Nyie, hawa wasanii wanaonewa sana

Sunday June 12 2022
NYIEE PICHAA
By Dk Levy

Utasikia Diamond siku hizi hawezi kuandika mashairi kama zamani. Sawa, lakini wapo wanaoandika kama yule Diamond wa zamani? Kwenye akaunti ya muziki wako ‘homu’ au kwenye simu, umejaza nyimbo za nani? Za Mondi au hao wengine?

Utasikia Harmonize anabebwa sana na ‘kiki’ kuliko kufanya muziki wa kweli. Sawa, lakini wapo wasanii wanaofanya muziki kimya kimya bila ‘kiki’? Kwenye ‘grupu’ zenu za ‘wasapu’, vijiweni hata maofisini huwa mnajadili nini? Kiki za Konde Boy au hao wengine?

Haina tofauti na kusema hupendi siasa wala wanasiasa. Lakini, kutwa kuchwa unalia na kulalamikia vitu ambavyo ni matokeo ya siasa na wanasiasa. Kama ‘tozo’, mfumuko wa bei, nauli, kuswaga wamachinga kwenye mitaa ya majiji na miji. Na kila kitu kinachohusu maisha yetu.

Mdomoni unatoa maneno ya kuelewa na kupenda kazi za Lady Jaydee. Ukidai mwanadada huyu anafanya muziki wa kweli. Na wala hana ujinga wa ‘kiki’ na drama za kindezi. Lakini ukifungua insta cha kwanza kutazama ni ‘drama’ za hao wa mjini ambao kutwa ni ‘drama’ tupu kwao.

Unaongoza kulalamikia sana uvaaji wa wasanii wa kike kwenye video na hata majukwaani. Lakini, unaongoza kwa kushangilia na kupiga miluzi, ‘pisi’ kali kitaa zikipita zile zenye ‘Neema za Alah’, kwa sauti ya Sheikh Kipoozeo. Na zaidi unaziimbisha ovyo ovyo pisi kali huko mitaani.

Unalalamika kwamba wasanii wa WCB nyimbo zao zimejaa matusi sana. Sawa, wao wanatumia lugha ya kiuficho, lakini wewe unaongoza kwa kutenda matusi mitaani huku. Yaani unakemea asiimbe kile unachofanya au? Anzia ‘homu’, kwa daladala hadi ofisini. Kuna lugha gani?

Advertisement

Watu tunaponda kile tunachofanya kila siku kwa kificho au kwa uwazi. Yaani tumekuwa mabingwa wa kuziponda lugha za mashairi ya wasanii. Huku sisi tukiwa mabingwa wa ‘kusagia kunguni’ video na uvaaji wa wasanii wetu.

Lakini huku mtaani kwetu kukoje? Hawa wasanii wanatumia lugha toka mataifa ya nje? Uvaaji wao ni wa mataifa ya nje? Mitaani huku tunatumia lugha gani? Na tunavaa mavazi gani na kwenye simu tumehifadhi video za aina gani? Maana tusiponde tunachokiishi.

Serikali imefungia mitandao yenye kuonesha video za ngono. Ni jambo jema sana, lakini kile kilichofungiwa huwa kinatazamwa na walevi ngono tu. Vipi ngono zinazofanyika kwa vitendo mitaani kwetu? Kwa ‘pub’ na ‘grosari’ za upenuni mwa nyumba zetu?

Kwa sasa ukahaba unatrendi kinoma mitaa ya Daslama, sijui kwa baadhi ya mikoa. Ukweli ni kwamba imekuwa biashara kubwa ambayo ‘dadaz’ hufanya bila ya kificho. Kama hujui hivi sasa wamefikia ‘levo’ za kukufata mpaka magetoni kwako.

Dada zetu hujiuza kupitia mitandao ya badoo, tinder, tagged na telegram. Tena telegram ndo uozo mtupu, wengi ni wadogo umri. Wake za watu na baadhi ya mastaa wa nchi hii, mitandaoni huko kumeoza mno. Sheria zetu zipo maalumu ili zivunjwe.

Lakini hao wauzaji na wanunuzi pindi wakiwa kwenye mishe zingine mchana ndio vinara wakubwa wa kuponda video na mashairi ya kina Mondi na wenzake kuwa zina matusi sana.

Hatutaki waimbe tunachokiishi? Na ukifanya uchunguzi wa fasta fasta, binadamu wanaoishi kimatusi mijini ni wengi kuliko wenye maisha yao ya hofu ya Mungu. Wengi wanaishi kimatusi kuliko video na mashairi yenye matusi.

Madanguro mitaa ya Sinza, Tabata, Kino, Temeke, Mwananyamala na kwingine ni mengi kuliko maduka ya dawa na saluni. Wapo ambao wanakodi nyumba hata kadhaa mtaa mmoja na kugeuza madanguro ya biashara yao.

Baadhi ya sehemu za ‘masaji’ huko ndo kumeoza. Ukweli ni kwamba kuna ofisi za ‘masaji’ kupewa vibali na serikali ni kuruhusu kushamiri kwa michongo ya ukahaba. Asilimia kubwa ya watoaji wa huduma hiyo, hutoa huduma mbadala ya kimwili.

Ukitaka kuthibitisha tembelea sehemu yoyote yenye ‘dili’ la ‘masaji’. Wakutajie huduma zao zote, mpaka ‘bode tu bode masaji’. Yaani mnakuwa kama Adam na Hawa kule bustanini. Unafanyiwa hiyo ‘bode tu bode’. Na ukitaka zaidi ni dau lako tu.

Halafu hao kengepori na ‘bode tu bode’ zao, utawakuta wanaponda ngoma za wasanii kuwa zina mitusi mingi. Jamii kubwa tunaishi kimatusi kuliko tungo za kina Konde Boy.

Unaweza kusoma haya lakini ukaona kama hayakuhusu na ukweli ni kwamba yanakuhusu, kama sio dada yako basi jua ni dada wa mshikaji wako.

‘Ukicheki’ mitandaoni utagundua kuwa kila siku kuna maelfu ya video ambazo hurushwa na dada zetu kwa ajili ya hao wateja wao ambao wengi ni Wabongo. Kifupi tutarajie uwepo wa video nyingi za ngono za kibongo siku zijazo kuliko za wazungu. Hapa ni lazima Serikali na jamii tuanze kuwa wakali sana, vinginevyo vizazi vyetu vijavyo vitakuwa kwenye hatari kubwa ya kuharibikiwa. Mambo yanayofanyika kwa sasa huko mtaani hayafai. Kwa mfano wakazi wa Sinza wamefikia mahali pa kuhama mijengo yao, kwani wakifungua geti tu usiku wanakutana na wadada wamejipanga foleni kama wako kwenye duka la kaya. Tuache kuwanyooshea vidole wasanii wetu kwa kulalamikia tungo na video zao wakati jamii nzima inaishi kimatusi. Msanii hufanya kazi ambayo itagusa jamii inayomzunguka. Kama wanaimba matusi na video za utupu basi kuna shida kwenye jamii ambayo inazipokea. Kabla ya kuwaponda na kuwalalamikia ikiwa pamoja na kufungia ngoma zao, sasa tuiangalie jamii kwa upana wake.

Advertisement