Nyimbo tano za Oscars kuimbwa kutokea juu ya paa

Wednesday April 21 2021
oscrapic

Wafanyakazi wakisafisha paa la jumba

By Mwandishi Wetu

Los Angeles, Marekani (AFP). Nyimbo tano zilizotajwa kuwania tuzo katika tamasha la 93 la kutuza wacheza filamu la Oscars, zitatumbuizwa kutokea juu ya paa la jumba la makumbusho lililo katika mji mdogo wa uvuvi wa Iceland, ikiwa ni harakati za watayarishaji kufanya mabadiliko kuendana na janga la virusi vya corona.

Tamasha hilo kubwa duniani katika filamu litafanyika Aprili 25, wakati jumba hilo la makumbusho la taasisi ya Academy of Motion Pictures Arts and Science inayoandaa tuzo za Oscars, litafunguliwa Septemba 30.

Nyota wa filamu ya "Hamilton", Leslie Odom Jr atakuwa mmoja wa watakaotumbuiza kutoka eneo hilo la wazi lililo juu ya jengo hilo lililoko Los Angeles.

Jumba hilo la makumbusho limejengwa kwa miaka minne, lakini uzinduzi wake umecheleweshwa kutokana na janga la corona.

Wimbo wake wa "Speak Now" ulio katika filamu yenye matukio ya harakati za haki za kijamii ya "One Night in Miami", utakuwa sehemu ya burudani maalum kabla ya tamasha hilo -- kama itakavyokuwa kwa wimbo wa mashairi ya mapenzi wa "Husavik" ulio katika filamu ya vitimbi ya Will Ferrell inayoitwa "Eurovision Song Contest: The Story of Fire Saga," iliyoigizwa katika bandari ya Iceland yenye jina kama hilo.

"Tumebuni matukio muhimu ya kabla na baada ya tamasha ili kuimarisha tukio letu kubwa," mshindi wa tuzo za Oscar, Steven Soderbergh na mtayarishaji mwenzake wa tamasha hilo, walisema katika taarifa yao wiki iliyopita.

Advertisement

"Tunachotaka ni ufungue (televisheni yako) uone tamasha lote, la sivyo utakosa kitu ambacho hukukitegemea na cha kufurahisha."

Jumba hilo lililobuniwa na Renzo Piano liko katika eneo la mita 28,000 za mraba nje kandokando ya jiji la Los Angeles na lina majengo mawili; Saban na The Sphere ambalo lina kumbi mbili za David Geffen, unaoweza kuchukua watu 1,000 waliokaa, na Dolby Terrace, ambalo linatoa taswira nzuri ya jiji la Baverly Hills katika kaunti ya Los Angeles, California.

Pia lina baraza kubwa juu ya paa ambalo litatumiwa na watumbuizaji wa nyimbo hizo tano zinazowania tuzo za Oscars.

Tukio la mwaka huu la Oscars linaenda kwa mpango wa "tamasha la utoaji tuzo kama filamu" na litafanyika kwa kuheshimu masharti ya kutokaribiana kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya corona ndani ya ukumbi wa Union Station ulio katikati ya jiji la Los Angeles.

Harrison Ford, Brad Pitt na Reese Witherspoon ni miongoni mwa wasanii wa kada ya juu watakaokabidhi zawadi, ikiwa ni mara ya kwanza kwa majina hayo makubwa ya Tinseltown kuwa pamoja katika zuria jekundu tangu mwaka jana.

Katika tamasha hilo pia kutakuwa na maeneo nchini Uingereza na Ufaransa kwa ajili ya wasanii waliotajwa kuwania tuzo ambao watashindwa kwenda Los Angeles.

Muziki utakaotumbuizwa kabla ya tamasha pia utajumuisha mshindi wa tuzo za muziki za Grammy, H.E.R. na Diane Warren, ambaye aneshatajwa mara 12 kuwania tuzo za Oscar.

Warren anapewa nafasi kubwa ya kushinda tuzo mwaka huu kutokana na filamu zake za "Judas and the Black Messiah" na "The Life Ahead," zilizotajwa kuwania tuzo.

Watayarishaji pia wametangaza mahojiano baada ya tamasha hilo waliyoyapachika jina la "Oscars: After Dark," ambayo yatahusisha washindi wa vipengele vikubwa wakiwa na tuzo zao.

Advertisement