Nyuma ya pazia Hamisa Mobetto kuimba singeli

Sunday July 18 2021
Hamisa pc
By Peter Akaro

Mwamitindo Hamisa Mobetto, ambaye aliamua kutupa karata yake pia kwenye muziki wa Bongofleva, amewakosha wengi mara baada ya kuibukia kwenye miondoko ya singeli na kuachia remix ya wimbo ‘Ex Wangu’ akishirikiana na Seneta Kilaka.

Hamisa anakuwa msanii wa tatu wa kike Bongo ndani ya wiki mbili kuachia wimbo wa singeli, alianza Zuchu na wimbo ‘Nyumba Ndogo’, kisha akafuata Menina aliyeibuka kupitia Bongo Star Search (BSS), na wimbo wake, ‘Nyumba Kubwa’.

Mwendelezo wa wasanii wa Bongofleva kufanya singeli umetajwa na wadau kama ishara ya kuendelea kukua kwa muziki huo. hasa upande wa biashara yake.

Akizungumza na gazeti hili, Seneta Kilaka amesema Hamisa alimtafuta kwenye mtandao wa Instagram baada ya kuupenda wimbo huo na kumpa namba ya meneja wake kisha wakakutana, baada ya makubaliano ya kibiashara kwa pande zote mbili ndipo wakaingia studio na kurekodi remix ya wimbo huo.

“Huu ni mwaka wangu wa nne nipo kwenye muziki, nilishafanya kolabo na Dulla Makabila kwenye singeli, katika Bongofleva nilifanya na Gigy Money na bado sikutoka. Ila nyota yangu inaonekana alikuwa nayo Hamisa, tumefanya tu remix ya huu wimbo kila mmoja sasa ananitambua na muziki wangu,” anajinasibu Seneta.

Video ya wimbo huu imepata watazamaji zaidi ya milioni 1 kwenye mtandao wa YouTube ndani siku tatu na kuwa miongoni mwa video chache za singeli zilizopata mapokezi makubwa ndani ya kipindi kifupi.

Advertisement


Ugumu wa kufanya na Hamisa

Seneta anasema kufanya kazi na Hamisa kulikuwa na changamoto mbili kubwa, kwanza ni wakati wa kushuti video, pili walipokuwa wanarekodi Hamisa ilimbidi kujitoa zaidi ya hapo awali.

“Kwenye kufanya video ilikuwa ngumu kwa sababu kuna sehemu kama mbili nilitakiwa kucheza na Hamisa, nimshike kiuno, mara nimbambie, ilikuwa ni ngumu kwa sababu yule ni dada yangu na ni shemeji yetu. Ila aliniambia mdogo wangu usiogope wala usiwe na aibu tupo kazini, fanya chochote kinachohitajika,” anasema huku anacheka na kugonga mikono yake kwa pamoja.

“Wakati tunarekodi nilimwelekeza kwa sababu muziki wa singeli unahitaji pumzi, maneno yako uyatoe kwa hali ya mkazo, japokuwa ilikuwa ni ngumu kwake lakini tulirekodi na unaona umetoka vizuri,” anasema Seneta.

Utakumbuka Agosti 2018 ndipo Hamisa aliachia wimbo wake wa kwanza unaokwenda kwa jina la ‘Madam Hero’. Wimbo huu umeandikwa na msanii Foby na Prodyuza C 9. Pia kwa mara ya kwanza Januari Mosi 2019 Hamisa alitumbuiza jukwaani baada ya kuachia wimbo huo na mwingine uitwao ‘Tunaendana’ ambao video yake ilifanyika Marekani.


Wadau wafunguka

Mtangazaji wa E FM Radio, Fido ambaye anatangaza kipindi cha Genge kinachocheza muziki wa singeli pekee, anasema hiyo ni ishara kuwa muziki huo umezidi kukua na anategemea kuona wasanii wengi wa Bongofleva kuungana nao.

“Imeshakuwa biashara na mtaani ndio unahitajika sana, hivyo wasanii wa Bongofleva wanalazimika kufanya hivyo ili kuifikia mitaa, pia wanaona kwenye shoo jinsi wasanii wa miondoko hiyo wanavyoamsha. Kwa hiyo na wao wanajikuta hakuna namna zaidi ya kufanya muziki wa singeli, na ndio changamoto kubwa iliyoukumba muziki wa Bongofleva sasa,” anasema Fido.

Kuhusu wasanii wa kike kutoka kwenye Bongofleva kuonyesha mwitiko zaidi upande wa singeli kwa kipindi cha hivi karibuni, Fido anasema hiyo ni kutokana na muziki huo kutoa fursa ya mipasho, kitu ambacho wanawake wengi wanakipenda.

“Unajua singeli ni muziki wa Uswahilini, wanawake wengi wamehamasika kufanya kwa sababu unashabihiana na mipasho, ni kama version mpya ya taarabu. Ndio maana wameupenda, unajua tena watoto wa kike wanapenda kuchambana, na unawapendeza sana wanapoufanya” anasema.

Kwa upande wa Prodyuza wa muziki, Mocco Genius ambaye ametengeneza wimbo wa Menina ‘Nyumba Kubwa’ wenye mahadhi ya singeli pia, anasema miondoko hiyo ni utambulisho wa muziki wa Kitanzania na ndio sababu unazidi kushika kasi na pia kila muziki una wakati wake.

“Kuna kipindi wasanii walikuwa wanashauriwa kuupa nguvu muziki wa singeli kwa sababu ndio unaibeba asili yetu na ukisikiliza hamna nchi yoyote ambayo inaupiga,” anasema Mocco.

Ameendelea kwa kusema: “Sasa wakitoka wasanii wa Bongofleva wakafanya singeli ni kwamba wanafanya muziki ambao unaweza kusikilizwa na mtu yeyote kutoka Taifa lolote, kwa hiyo kwangu ni kitu kizuri na waendelee kuufanya”.

Ikumbukwe hadi sasa majina makubwa kwenye muziki kama Professa Jay, Lava Lava, Mr. Blue, Harmonize, Ben Pol, Ruby, Snura, Rayvanny, Ibraah na wengine wameachia nyimbo zenye mahadhi ya singeli na zimefanya vizuri.

Advertisement