Panda shuka ya taarabu

Sunday November 14 2021
kopapic
By Nasra Abdallah

Unakumbuka wimbo wa ‘Mambo ipo huku’, Nyama ya bata, Utalijua Jiji, Njiwa na Tx Mpenzi au ile ya Mwanamke hulka. Achana na hizo, vipi kuhusu Sanamu la Michelini, Kinyago cha mpapure, Njiwa peleka salamu na nyingine kibao ambazo ziliufanya muziki wa taarabu kuwa juu zaidi.

Wakati huo si kwamba taarabu ilikuwa juu pekee, bali hata wasanii wake walikuwa hawashikiki kwa umaarufu na hata vipato vyao vilikuwa vya uhakika. Khadija Kopa, Nasma Hamis walikuwa moto, huku TOT na Muungano zikitamba na kuteka kundi kubwa la mashabiki ndani ya nje ya mipaka.

Kipindi hicho unaambiwa ilikuwa ni bandika bandua, msanii huyu au kundi hili likiachia wimbo basi ndani ya siku ama saa chache mwingine kashusha kitu na kinatoka na moto wake na kuteka soko.

Hata hivyo, ilipoingia taarabu ya kisasa kundi kubwa la wasanii kama wakina Mzee Yusufu, Isha Mashauzi, Joha Kassim, Hadija Yusufu na Leila Rashid wakaichukua taarabu na kuipeleka juu zaidi.

Hapa ndipo tuliposikia nyimbo kama VIP, My Valentine, Two in One zilizoimbwa na kundi la Jahazi ambazo zilitingisha.

Akaja Isha Mashauzi na ngoma zake za ‘Nani kama Mama’, Mapenzi hayana dhamana, Sudi sudini, Una mapungufu na nyingine nyingi.

Advertisement

Wapenzi wa muziki huo ilikuwa wakisikilizia mwezi huu kibao gani kimeachiwa na ndio kipindi watu walitoka kwenye kutumia kaseti na kutumia CD.

Ukiacha kusikiliza tu, kumbi mbalimbali, hususan siku ya kuanzia Alhamisi hadi Jumapili watu walikuwa wakipigana vikumbo kupata burudani ya muziki wa taarabu.

Hata hivyo, muziki huo sasa hivi umekumbwa na gharika la kushuka ambapo, wakongwe wa muziki huo wameeleza sababu mbalimbali zinazochangia kushusha muziki huo.

Afua Suleiman, mwimbaji wa wimbo wa ‘Utalijua Jiji’ ameeleza kuwa moja ya sababu zinazochangia kushusha muziki wa taarabu ni kutokuwepo kwa viingilio kwenye shoo nyingi.

“Thamani ya taarabu imeshuka na sababu ni kuondolewa kwa viingilio, yaani sasa hivi ukinunua kinywaji unaangalia shoo. Hata thamani ya wasanii wenyewe imeshuka,” anasema Afua.

Alisema wakati wa kipindi chao taarabu ilikuwa juu na mashabiki walikuwa wakilipa viingilio vikubwa kupata burudani, huku wasanii wenyewe wakilipwa mishahara mikubwa na posho za uhakika.

Lakini, kwa sasa makundi mengi yamekuwa wakitegemea kufanya shoo na kugawana viingilio vilivyopatikana kama posho za kujikimu, huku uuzaji wa kasri ukidorora kwa kasi kutokana na teknolojia.

Lakini, kwa Patricia Hillary anasema kuwa kitendo cha baadhi ya wasanii kurudia nyimbo za wasanii wa zamani, zimewafanya hata wale wenye vipaji kushindwa kuonekana na kuendeleza muziki huo.

Hata hivyo, alishauri kuwa wasanii wa taarabu wanapaswa kubadilika na kwenda na wakati, kwa kuwa muziki ni biashara, hivyo wasing’ang’ane kufanya kazi zao kizamani.

“Kuliingia taarabu ya Taradance, ambapo msanii anapanda na wanenguaji wake jukwaani na kuuchangamsha muziki huo, hawa wasilaumiwe kwa kuwa wapo kibiashara zaidi na siyo tu kutoa burudani kama tulivyokuwa tunafanya sisi huko zamani, hivyo wasanii wenzangu tubadilike,” alisema Patricia.

Khadija Kopa, ukipenda muite Malkia wa Mipasho alisema anachokiona kwa sasa ni kila wakati na jambo lake, hivyo sasa ni zamu ya BongoFleva kushika hatamu.

“Hakuna asiyekumbuka kuna wakati ulingia muziki wa taarabu ukawa huwaambii watu kitu kisha ikaingia dansi na mambo yakawa ni moto, sasa ni Bongofleva kutamba.

“Tunachotakiwa kufanya sisi wa taarabu ni kuangalia upepo unavyovuma ili twende nao, ndio sababu unaniona nimeimba na wasanii wengi wa Bongofleva ambao ni miongoni mwa wanaonifanya niendelee kusikika licha ya kipaji alichonijalia Mungu,” anasema mwimbaji huyo, akiwashauri wasanii wa taarabu kuacha kutegemea kutungiwa nyimbo.

Kwa upande wake Mzee Yusufu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Waimba Taarabu Tanzania (TTA), anakiri wasanii wenyewe wamechangia kushusha muziki huo kwa kuwa hawatengenezi kazi nzuri zenye kuwashawishi mashabiki kusikiliza. Mzee Yusufu ametamba vilivyo akiwa na kundi lake la Jahazi Modern Taarabu.

Advertisement