Paul wa P-Square augua Corona

Tuesday January 05 2021
corona pic
By Mwandishi Wetu

Nyota wa muziki kutoka kundi lililokuwa likiundwa na waimbaji mapacha kutoka Nigeria la P-Square, Paul Okoye maarufu Rude Boy ametangaza kukutwa na virusi vya Corona.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, staa huyo aliyetamba na nyimbo ya  'Take It' pamoja na 'Ifunanya' alizoimba na kaka yake ameandika ujumbe leo Januari 5 akielezea hali anayopitia sasa huku akiwaonya wanaodhani kuwa ugonjwa huo ni haupo watalipa gharama za ubishi wao kwa kuathirika pia.

"Aisee!! Covid ipo KWELI!!!" Ameanza kwa kuandika hivyo Paul na kuongeza,

"Nafahamu kama mwafrika wa kawaida ni ngumu sana kuamini mpaka yakukute. Sasa mimi yamenikuta na yameniganda kwa zaidi ya siku 10 sasa."

"Kwa hiki ninachokipitia, naweza kusema Covid ni ugonjwa mbaya kuliko wowote ule. Nashauri muwe makini jamani, ukitaka niamini, usipotaka usiniamini, lakini ujue kuwa utalipa gharama za ujinga wako." Ameandika Paul.

Hali anayopitia Paul ambaye ni pacha mdogo iliwahi kumkumba kaka yake pia mwaka jana mwezi Juni ambapo yeye, familia yake (mke na mtoto) pamoja na wafanyakazi wake wawili wa ndani waligundulika kuwa na Covid.

Advertisement

Hata hivyo kwa upande wa Paul hajaeleza kama Covid imeigusa pia familia yake au watu wake wa karibu kama ilivyokuwa kwa kaka yake.

Advertisement