Phina asaini dili la miaka minne na Ziiki Media

What you need to know:

Mwimbaji wa Bongofleva aliyesumbua mwaka uliopita na ngoma 'Upo Nyonyo' na nyinginezo, Sarah Michael Kitinga 'Phina' amejiunga rasmi na kampuni kubwa ya usambazaji muziki barani Africa, Ziiki Media.

Mwimbaji wa Bongofleva aliyesumbua mwaka uliopita na ngoma 'Upo Nyonyo' na nyinginezo, Sarah Michael Kitinga 'Phina' amejiunga rasmi na kampuni kubwa ya usambazaji muziki barani Africa, Ziiki Media.

Makubaliano hayo ya miaka minne yanalenga zaidi kuendeleza kipaji cha mwimbaji huyo, kukuza soko lake la muziki duniani kupitia usambazaji, pamoja na kukuza fursa mbalimbali za biashara ya muziki.

Ziiki Media ni kampuni inayoongoza kwenye biashara ya usambazaji wa kazi za muziki barani Afrika na India kwa ushirikiano na kampuni kubwa ya muziki duniani Warner Music Group, huku ikitoa huduma kama usimamizi na usambazaji wa kazi za muziki, promosheni na usimamizi wa wasanii


Kwenye uzinduzi rasmi uliofanyika jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini, Phina amesema ajisikia mwenye furaha na bahati kuwa miongoni mwa wasanii wa kike kutoka Tanzania kupata nafasi ya kipekee kufanya kazi na familia nzima ya Ziiki Media.


"Ushirikiano uliozaliwa hapa leo ni hatua kubwa sana kwangu kwani hizi ni aina za fursa ambazo nimekuwa nikizitamani kuzifanikisha kwa muda mrefu kwenye kazi yangu. Niko tayari kuiwakilisha Afrika kwenye jukwaa la muziki,  huku tukiendelea kuipeleka sanaa na muziki wa Tanzania na Afrika mbele” amesema Phina.


Katika kumkaribisha Phina Ziiki Media, Mkurugenzi wa kampuni hiyo,  Arun Nagar amesema kukutana na kipaji kama cha Phina ni nadra sana, uwezo wake wa sauti na kutawala jukwaa ni vitu vya kushangaza na kutamani kuona kwa wasanii wengi zaidi.


"Binafsi nina shauku ya kuona atafanya nini kwenye majukwaa makubwa ya muziki. Sina shaka na uwezo wake wa kimuziki na nina imani ushirikiano wetu utadhibitisha mengi zaidi ambayo bado hatujayashuhudia kutoka kwake,” amesema Arun Nagar.

Ikumbukwe Phina ni msanii wa muziki kutoka Tanzania ambaye ujio wake kwenye tasnia ya muziki ulitambulishwa rasmi mwaka 2018 aliposhinda tuzo ya mashindano makubwa ya kuvumbua vipaji nchini Bongo Star Search (BSS.


Mwaka 2021 Phina alifanikiwa kuachia rasmi kazi yake ya kwanza ya muziki ‘In Love’ iliyopokelewa vizuri na mashabiki aliokwisha wajenga tokea BSS na toka kipindi hicho safari yake ya muziki imekuwa ya mafanikio mengi ikiwemo kutazamwa kama miongoni mwa wasanii bora wanaokua kwa kasi.


Mwaka 2022 Phina alishinda tuzo mbili za Tanzania Music Awards (TMA) kama Msanii Bora Wa Kike Chipukizi pamoja na tuzo ya Mtumbuizaji Bora wa Kike.