Queen Elizabeth katika ulimwengu wa muziki

What you need to know:

  • Utawala wake ulianza Februari 6, 1952, Malkia Elizabeth II, sio tu Mfalme aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi nchini Uingereza, bali ndiye Mfalme pekee ambaye tumekuwa naye kabla muziki wa Rock na Pop hujashika kasi duniani.

Utawala wake ulianza Februari 6, 1952, Malkia Elizabeth II, sio tu Mfalme aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi nchini Uingereza, bali ndiye Mfalme pekee ambaye tumekuwa naye kabla muziki wa Rock na Pop hujashika kasi duniani.

Ikumbukwe muziki wa Rock ulianza nchini Marekani mwishoni mwa miaka ya 1940 na mapema miaka ya 1950, uliendelea kuwa na aina mbalimbali za mitindo, katikati ya miaka ya 1960 ulivuma zaidi Marekani kisha Uingereza, huku Pop ikianza katikati ya miaka 1950 huko Marekani na Uingereza.

Malkia Elizabeth II alizaliwa Aprili 21, 1926 huko Mayfair, London nchini Uingereza, alifariki Ahamisi, Septemba 8, 2022 akiwa na umri wa miaka 96, baada ya kutawala kwa miaka 70.

Alikuwepo kwenye kiti cha enzi kabla ya ‘The Beatles’, ‘Elvis’, hata kabla Big Mama Thornton hajarekodi toleo la kwanza la ngoma yake maarufu ‘Hound Dog’.

Watu wengi walipata kufahamu nyimbo ambazo alizipenda Malkia Elizabeth II wakati anasherekea miaka 90 ya kuzaliwa, kupitia dokumentari, ‘Our Queen: 90 Musical Years’. Binamu yake wa kwanza, Lady Elizabeth Shakerley alitaja nyimbo hizo ni;. Oklahoma!’ – ‘Howard Keel’, ‘Anything You Can Do’ (I Can Do Better) – Dolores Gray and Bill Johnson, Sing – Gary Barlow and the Commonwealth Band featuring the Military Wives, Cheek to Cheek – Fred Astaire, The White Cliffs Of Dover – Vera Lynn.

Nyingine ni; Leaning on a Lamp-post – George Formby, Praise, My Soul na The King Of Heaven’(hymn) - Alan Gray and John Gos, The Lord is My Shepherd’ (hymn), Lester Lanin Medley na Regimental March Milanollo.

Kwa mujibu wa Lady Elizabeth Shakerley, Malkia Elizabeth II, alizipenda zaidi nyimbo kama kama “Oklahoma!” na “Annie Get Your Gun,” ambazo ziliimbwa kwenye harusi yake na Philip Mountbatten Novemba 20, 1947 huko Westminster Abbey, London.

Mwimbaji wa Uingereza, Soprano Alexandra Stevenson aliimba nyimbo zote mbili katika “The Queen’s Chapel of the Savoy” mnamo Februari 2022 kuadhimisha Platinum Jubilee ya Malkia.

Malkia Elizabeth II pia alikuwa shabiki wa msanii wa Pop, Cliff Richard, mwaka 2012 mwimbaji wa Uingereza, Gary Barlow alipewa jukumu la kuandaa tamasha la mwaka huo la Diamond Jubilee, na Malkia alikuwa na ombi moja maalumu.

“Ilinibidi nimuulize Malkia angependa tamasha hili liwe na kitu gani cha pekee, alichoomba ni uwepo wa Cliff Richard. Kwa hiyo nilikutana naye (Cliff) kwenye hilo, sikumwambia kwamba lilikuwa ombi, bali alikuja na kufanya hivyo na alikuwa na neema sana,,” Gary Barlow aliambia gazeti la The Sun.

Katika Golden Jubilee mwaka 2002 na Diamond Jubilee miaka kumi baadaye, zilisherehekewa kwa maonyesho na wasanii kadhaa wa Pop kutumbuiza ingawa ni vigumu kujua ni muziki wa kina nani aliupenda au ni upi ulikuwa kwa ajili ya kuwafurahisha raia wake.

Siku chache baadaye sherehe ya watu wote wa Pop ilifanyika katika Ikulu Juni 3, 2002, ilifunguliwa na Brian May na Roger Taylor wakiimba wimbo wa Taifa, ‘God Save The Queen’, huku Brian akipiga gitaa ndani ya Buckingham Palace.

Naye Cliff Richard alikuwepo, aliimba na Bendi wimbo, ‘Living Doll’, kisha wimbo wake maarufu ‘Move It’ wa mwaka 1958 akishirikiana na S Club 7 na Brian May. Paul McCartney ndiye alifunga sherehe hiyo kwa kuimba nyimbo zake kama; ‘Magical Mystery Tour’, ‘All My Loving’, ‘Let It Be’, ‘Live and Let Die’ na ‘Ob-La-Di, Ob-La-Da’.

Kwa ujumla Malkia Elizabeth II alikaribisha nyuso nyingi maarufu upande wa burudani katika kasri lake, kila mara alipeana mikono kwa heshima alipopokea watu mashuhuri kwenye matamasha mbalimbali na sherehe.

Baada ya kutangazwa kifo cha Malkia Elizabeth II, wasanii wa kundi la The Spice Girls kutoka nchini Uingereza liloundwa mwaka 1994, walienda kwenye mitandao ya kijamii kuomboleza kifo cha malkia huyo.

“Leo (alhamisi) ni siku ya huzuni sana si kwa nchi yetu tu bali kwa ulimwengu mzima. Nimehuzunishwa sana na kifo cha Mfalme wetu mpendwa, Her Majesty The Queen,” aliandika Victoria Beckham, maarufu kama Posh Spice.

Naye Melanie Brown ‘Scary Spice’ alishapisha mtandaoni picha akiwa na Malkia Elizabeth II na kusema;

“Leo ni siku ya huzuni zaidi. Tumempoteza mwanamke wa ajabu ambaye sisi sote tulikua pamoja naye na tulikuwa na heshima kubwa kwake”.

Melanie Brown amesema anakumbuka na kushukuru alivyotunukiwa nishani (MBE) na Malkia Elizabeth II kwa kutambua kazi yake kama mtetezi wa waathiriwa wa unyanyasaji majumbani.

Malkia Elizabeth II pia mara nyingi alikuwa akisimamia utendaji wa Royal Variety, kipindi cha televisheni kinachoonyeshwa kila mwaka Uingereza ili kuchangisha fedha kwa ajili ya “Royal Variety Charity” ,ambayo imewahi kuwaleta pamoja wasanii kama Spice Girls, Lady Gaga, Bette Midler, Kylie Minogue, Alicia Keys na Michael Buble.

Royal Variety Charity ni shirika la misaada la Uingereza lililopo Twickenham jijini London, linatoa msaada kwa wale ambao wametumikia tasnia ya burudani na kujikuta katika magonjwa, umaskini au uzee.

Shirikaka hilo la hisani lilianzishwa mwaka 1908 likijulikana kama Variety Artistes’ Benevolent Fund, kisha mwaka wa 1971 likaitwa Entertainment Artistes’ Benevolent Fund, na baadaye Juni 2015 likaaza kutumia jina la Royal Variety Charity.