Rais Ramaphosa akataa mazishi ya AKA kufanyika kitaifa

Muktasari:

  • Ramaphosa amekataa ombi la Waziri wake Mkuu Gauteng Panyaza Lesufi mazishi ya rapa AKA kufanyika kitaifa ikiwa ni jeneza lifunikwe bendera ya taifa na bendera kupeperushwa nusu mlingoti.

Cape Town. Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amekataa ombi la Waziri Mkuu wa Gauteng, Panyaza Lesufi mazishi ya rapa Kiernan Forbes maarufu AKA kufanyika kitaifa, waziri huyo aliomba jeneza lifunikwe bendera ya taifa na bendera kupeperushwa nusu mlingoti kwa heshima ya rapa huyo.

Kwa mujibu wa kituo cha habari ‘BBC’ wameeleza kwamba ombi hilo limekataliwa na Rais Ramaphosa baada ya kuandikiwa barua na Waziri Mkuu Gauteng Panyaza Lesufi, kuomba kupata ruhusa kwa ajili ya mazishi hayo kufanyika kitaifa.

Alhamisi ya Februari 16, 2023 Waziri Lesufi alisema ombi lake lilikataliwa alisema, hakuomba fedha za Serikali kwa ajili ya mazishi, bali jeneza lifunikwe bendera ya taifa na bendera kupeperushwa nusu mlingoti kwa heshima ya AKA.

"Tulihisi kwamba mtu wa hadhi yake ya kimataifa, mtu wa hadhi ya kitaifa, lazima kuwe na aina fulani ya heshima, na tunataka kufafanua sio mchango wa kifedha," alinukuliwa akisema Waziri Lesufi.

Rapa AKA na timu yake walishambuliwa kwa risasi Jumamosi Februari 10, 2023 wakitoka mgahawani eneo la Florida Morningside jijini humo.

AKA aliyeacha mtoto mmoja wa kike anatarajiwa kuzikwa siku ya Jumamosi Februari 18.