Rayvanny afunika MTV EMA, rekodi zake zinatisha

Monday November 15 2021
rayvannpicc
By Peter Akaro

Dar es Salaam. Usiku wa kumkia leo mwimbaji wa Bongofleva, Rayvanny amefanikiwa kutumbuiza katika hafla ya utoaji wa tuzo za MTV Europe Music Awards  (MTV EMA) 2021 huko nchini Hungary.

Kwa matokeo hayo, Rayvanny anaandika rekodi ya kuwa msanii wa kwanza toka Afrika kutumbuiza katika tuzo hizo ikiwa ni mwendelezo wa kufanya mambo makubwa katika muziki wake. 

Rayvanny ametumbuiza na msanii toka Colombia, Maluma ambaye amemshirikisha katika wimbo wake mpya uitwao Mama Tetema ambayo ametayarishwa na Prodyuza S2kizzy toka Tanzania.

Maluma ni msanii mkubwa nchini Colombia, ana wafuasi zaidi ya milioni 27.9 kwenye mtandao wa YouTube, na wafuasi zaidi milioni 59.7 katika mtandao wa Instagram.

Diamond Platnumz ambaye ndiye amemtoa Rayvanny chini ya WCB Wasafi, amempongeza kwa hatua hiyo na kuwataka wasanii wengine kuwa na fadhila pamoja na nidhamu ili muziki wao ufike mbali na sio kuishia katika matumizi ya mihadarati.

Advertisement

Utakumbuka Diamond alikuwa anawania tuzo katika kipengele cha Best African Act ambacho ushindi umeenda kwa Wizkid wa Nigeria, huku Diamond mwenyewe, Tems, Amaarae na Focalistic wakiambulia patupu.


Je, ni lini na wapi Rayvanny alianza muziki?, hadi sasa amefanikiwa kufanya kipi na kipi katika kiwanda cha muziki?. Makala haya yanaenda kujibu maswali yote hayo. 


Mwanzoni Rayvanny alikuwa akifanya muziki wa Rap kabla ya kuanza kuimba, mwaka 2011 Rayvanny aliibuka mshindi katika mashindano ya Free Style pale Coco Beach. 


Wakati huo alijulikana kama Raymond, akatafuta nafasi ya kutoka kimuziki chini ya Tip Top Connection ambapo alifahamiana na Babu Tale, Meneja wa kundi hilo. Kufikia Aprili 2016 alisainiwa katika lebo ya WCB Wasafi na kutoa wimbo wake wa kwanza, Kwetu uliofanya vizuri na kufuatiwa na nyingine kali. 


Usiku wa Juni 25, 2017 katika ukumbi wa Microsoft Theater Centre, Los Angeles nchini Marekani, Rayvanny alipokabidhiwa tuzo ya  BET kupitia kipengele cha Viewer’s Choice Best New International Act na kuwa msanii wa kwanza na pekee kutokea Tanzania kushinda tuzo hiyo hadi sasa. 


Ikumbukwe Diamond amewania tuzo za BET zilizoanza kutolewa Juni 19, 2001 mara tatu bila ushindi wowote, alifanya hivyo mwaka 2014, 2016 na 2021. 


Hivyo, Rayvanny akawa msanii wa pili Afrika Mashariki kushinda tuzo hiyo baada ya Eddy Kenzo wa Uganda ambaye aliishinda mwaka 2015 na kuwa msanii wa kwanza kwa ukanda huo.


Ferbruari 2020 Rayvanny aliachia Extended Playlist (EP) yake ya kwanza, Flowers iliyofanya vizuri hadi kufanikiwa kuingia kwenye hatua ya kujadiliwa (Consideration) kwa ajili ya kuingia kuwania Tuzo za Grammy. 


Mwaka mmoja baadaye, yaani Februari 1, 2021 Rayvanny aliachia albamu yake ya kwanza, Sound From Africa ikiwa na nyimbo 23 alizowashirikisha wasanii 20 kutokea Tanzania na nchi nyingine za Afrika. 


Sound From Africa iliweza kuweka rekodi Afrika Mashariki kwa kufikisha wasikilizaji (streams) zaidi ya milioni 100 ndani ya wiki moja pekee tangu itoke.


Rayvanny akiwa chini WCB, Machi 2021 aliweza kuanza lebo yake, Next Level Music (NLM) akiwa ni msanii kwanza kufanya hivyo kwani Rich Mavoko na Harmonize alijiengua WCB ndipo wakaanzisha lebo zao, lakini Rayvanny hakufanya hivyo. 


Septemba 24, 2021 alimtoa msanii wa kwanza wa NLM, Mac Voice ambaye tayari alikuwa ameshasikika kwenye Bongofleva kwa kipindi cha nyuma ambapo alikuwa chini ya usimamizi wa Chege.


Mac Voice akaachia EP iitwayo My Voice EP yenye nyimbo tano ambapo amemshirikisha Rayvanny katika nyimbo mbili, nayo ilifanya vizuri hadi kufikisha wasikilizaji zaidi ya milioni 10 kwenye mitandao ya iTunes, Spotify, Audiomack na Boomplay na Play Music kwa kipindi cha mwenzi mmoja tu. 


Hivi karibuni Mac Voice kachaguliwa kuwania tuzo za African Entertainment Awards USA (AEAUSA) toka Marekani ambapo ametupwa kwenye kipengele cha Msanii Bora Chipukizi 2021. 


Wakati Mac Voice akiendelea kufanya vizuri, Oktoba 29, 2021 Rayvanny aliachia EP yake ya pili, New Chui yenye nyimbo Sita, huku akimshirikisha msanii mmoja tu ambaye ni Abby Chams. 


EP hiyo ilitoka wakati Rayvanny na Maluma wamesharekodi na kufanya video ya wimbo wao, Mama Tetema ambao ndio wameutumbuiza jana kwa mara ya kwanza kwenye jukwaa la MTV Europe Music Awards  (MTV EMA) 2021 na kuongeza thamani katika chapa Rayvanny.Advertisement