Rayvanny anarudia makosa yaleyale kwa Paula!

Friday September 10 2021
rayvannpic
By Peter Akaro

Dar es Salaam. Msanii wa Bongofleva kutoka WCB na Next Level Music (NLM), Rayvanny amendelezea utamaduni wake wa kutumia warembo anaokuwa nao katika mahusiano kwenye video za nyimbo zake, kitu ambacho sio dalili nzuri.

Hii leo Septemba 10, 2021 Rayvanny ameachia video ya wimbo wake mpya 'Wanaweweseka' ambayo ndani yake mpenzi wake wa sasa, Paula ndiye ametokea kama 'video vixen' ikiwa ndio mara ya kwanza kwa mrembo huyo kufanya hiyo.

Utakumbuka kabla ya Rayvanny hajaachana na mzazi mwenziye, Fahyma ambaye wamejaliwa kupata mtoto mmoja, alimtumia pia  kwenye video za nyimbo zake tatu ambazo ni ‘Kwetu’, ‘Natafuta Kiki’ na ‘Siri’, kisha wakatengana.

Hata hivyo, Rayvanny sio msanii wa kwanza ndani ya Bongofleva kufanya kitu kama hicho, kwani Diamond Platnumz, Harmonize, Jux, Ben Pol na wengineo wamefanya,  lakini mwisho wao katika mahusiano, haukuwa mzuri.

1. Diamond

Mwimbaji huyu wa WCB karibu warembo wote ambao wamewahi kuwa nao katika mahusiano ameshafanya nao video za nyimbo zake, alianza na Miss Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu ambaye alitokea kwenye video ya wimbo uitwao ‘Moyo Wangu’.

Advertisement

Kisha akafuata Zari The Bosslady aliyeonekana kwenye video ya wimbo 'Utanipenda' uliyotoka Desemba 2015, pamoja na ‘Iyena’ iliyoachiwa Mei 2018. Pia mzazi mwenziye Hamisa Mobetto naye aliinogekesha vizuri video ya wimbo ‘Salome’.

2. Harmonize

Wakati penzi la Harmonize na Jacqueline Wolper lipo katika kilele cha mafanikio yake, walisafiri hadi Afrika Kusini kufanya video ya wimbo 'Niambie', hiyo ni baada ya bibie kutokea kwenye video kadhaa Bongo ikiwemo ‘Pesa’ ya Mr. Blue.

Baadaye Konde Boy alianzisha mahusiano na mrembo kutokea Italia, Sarah ambaye walisafiri wote hadi Ngorongoro na kufanya video ya wimbo 'My Boo' ambao alishirikiana na Q Chief pia. Utakumbuka Harmoize na Sarah walifunga ndoa lakini ikivunjika ndani ya kipindi kifupi.

3. Jux

Kipindi cha penzi lao Vanessa Mdee alionekana kwenye video ya wimbo wa Jux 'Sisiki' iliyotoka mwaka 2014, pia walikuja kutoa nyimbo mbili pamoja ambazo ni ‘Juu’ na ‘Sumaku’.


Baada ya kuachana na Vanessa, Jux aliamua kubadili mapishi ndipo akafunga safari hadi Bangkok nchini Thailand na kukutana na mrembo Nayika ambaye amejiachia naye kwenye video ya wimbo wake uitwao ‘Unaniweza’.

4. Ben Pol

Mkali huyu wa RnB ambaye kila mahusiano yake yanayokuwa kwenye vyombo vya habari lazima yawe na drama nyingi, wakati wa penzi lake Ebitoke, aliamua kumtumia kwenye video ya wimbo wake uitwao ‘Natuliza Boli’

Mwishoni mwaka mwaka jana alichia wimbo 'Kidani' ambao katika video yake amejiachia na aliyekuwa mkewe kutokea Kenya, Anerlisa ambaye inadaiwa walikuja kupelekana mahakamani kudaiana talaka.

Ukiachana na hao, kuna Barnaba na mzazi mwenziye, Mama Steven (Zuu) katika video ya wimbo 'Wahalade', pia yupo Rapa Mabeste na aliyekuwa mke wake, Lisa Fickenscher katika video ya wimbo uitwao ‘Usiwe Bubu’.

Ukitazama wasanii hao zaidi  ya watano ambao walifanya video hizo, kwa sasa ndoa na mahusiano yao yamevunjika, kumbukumbu ya penzi lao imesalia kwenye video tu. Kwa muktadha huo, ni wazi Rayvanny wanarudia makosa yaleyale kwa Paula ambayo yamewakuta wenzao,  isitoshe ishamtokea Rayvanny katika mahusiano yake na Fahyma

Advertisement