Rayvanny, S2kizzy wanashikiri Grammy sio kuwania tuzo!

Muktasari:

  • Ghafla majina ya Rayvanny na S2kizzy yanaibuka yakihusishwa na tuzo za Garmmy  na  wenyewe wakifurahia hatua hiyo, lakini ukitazama kwenye vipengele vyote 94 huwaoni. Je, wanawania au kushiriki tuzo hizo? Ukweli upo hivi...

Hivi karibuni waandaji wa tuzo za Grammy, Recording Academy wametangaza majina ya wasanii wanaowania tuzo hizo za 66, huku kukiwa hakuna jina la msanii hata mmoja wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Ghafla majina ya Rayvanny na S2kizzy yanaibuka yakihusishwa na tuzo hizo na wao wenyewe wakifurahia hatua hiyo, lakini ukitazama kwenye vipengele vyote 94 huwaoni. Je, wanawania au kushiriki tuzo hizo? Ukweli upo hivi...

Ukweli ni kwamba Rayvanny na S2kizzy wanashiriki na sio kuwania Grammy. Wanashiriki kupitia mgongo wa albamu ya Maluma, Don Juan (2023) ambaye anawania kipengele cha 'Best Latin Pop Album' 2024. 

Albamu hiyo ndio ina wimbo wa Maluma 'Mama Tetema' ambao amemshirikisha Rayvanny, huku S2kizzy akiwa ndiye Prodyuza wa wimbo huo ambao umesampo wimbo wa Rayvanny, Tetema (2019) akimshikirikisha Diamond Platnumz.

Ikiwa albamu hiyo itashinda tuzo ya Grammy, basi Rayvanny na S2kizzy watapatiwa cheti cha kutambulika kwa kushiriki katika kazi hiyo na hata isiposhinda kuna aina nyingine ya cheti watapatiwa na waandaji wa Grammy.

Utakumbuka Nandy aliwahi kupatiwa cheti hicho baada ya albamu, Pamoja (2021) ya Etana kutoka Jamaica kuwania Grammy kama 'Best Regggae Album', ambapo  Nandy alishirikishwa katika wimbo uitwao Melanin.

Wapo wanaodai kuwa Diamond naye alipatiwa cheti hicho baada ya kushiriki katika albamu ya Alicia Keys, ALICIA (2020) ambayo ilishinda Grammy kama 'Best Immersive Audio Album', huku Diamond akisikika katika wimbo, Wasted Energy.

Ila ukweli ni kwamba hakupata kwa sababu  tuzo katika kipengele hicho haiendi kwa msanii, bali  kwa Mhandisi wa albamu (The Engineer), Mhandisi Mkuu (Mastering Engineer) na Mtayarishaji (Producer), wasanii waliohusika watapokea iwapo tu walishiriki kama watayarishaji.

Na kama wimbo wa ‘Mama Tetetema’ ndio ungekuwa amechaguliwa, basi moja kwa moja Rayvanny naye angetajwa kama msanii anayewania na kama ukishinda angepatiwa tuzo, huku S2kizzy na wengine walihusika kama watunzi wakipatiwa cheti.

Ikumbukwe tuzo hizo zinatarajiwa kutolewa Februari 4, 2024 nchini Marekani, zinatajwa kuwa ni za juu zaidi katika muziki, zilianza kutolewa tangu Mei 4, 1959 wakati huo zikifahamika kama Gramophone Awards. Lengo lake kuu ni kutambua mafanikio katika tasnia ya muziki.