Rayvanny, WCB ngoma bado nzito, wamkamua Sh50 milioni show ya Nandy

Friday August 05 2022
rayvan pic
By Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Rayvanny, WCB ngoma bado nzito. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya sakata lake la kutaka kuachana na WCB kutokamilika na kuendelea kumkamua hela.

 Julai 27, 2022 Rayvanny pamoja na uongozi wa WCB, akiwemo Mkurugenzi wa lebo hiyo, Naseeb Abdul maarufu ’Diamond Platnumz’, Meneja wake Sallam Sharaff na Said Fella ’Mkubwa Fella’ walionekana kwenye ofisi za Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).

Sababu za kuonekana kwao zikielezwa ni mvutano uliopo wa fedha wanayoitaka WCB walipwe kutokana na msanii huyo kuvunja mkataba ambayo ni Sh800 milioni pamoja na mgao wa fedha zinazopatikana kutokana na kinachoingia katika mitandao mbalimbali ya kuuza muziki.

Habari za ndani ambazo Mwananchi imezipata ni kwamba katika kikao kile pande mbili hizi bado zinatakiwa kurudi tena Basata kwa kikao kingine kwa ajili ya kumalizana na suala hilo.

Wakati kuhusu tetesi za kuwa ametozwa Sh50 milioni kutokana na kupanda kwenye jukwaa la Nandy Festival mkoani Songea, Meneja wa timu ya wasanii wa WCB, Rekado Momo, amekiri jambo hilo ni la kweli.

Akihojiwa katika kipindi cha Mashasham jana katika kituo cha redio Wasafi, Momo amesema hiyo imetokana na Rayvanny bado kutambulika kama ni msanii wa WCB hadi sasa na wamemkata fedha hiyo kutokana na mkataba wake unavyosema akienda mkoa gani anapaswa kulipwa Shilingi ngapi ambapo nje ya Dar es Salaam ndio hiyo Sh50 milioni.

Advertisement
Advertisement