Rema, Ayra Starr 'watishia' ufalme wa Diamond YouTube

KWA sasa rekodi ya Diamond Platnumz kama msanii aliyetazamwa zaidi YouTube Kusini mwa Jangwa la Sahara sio kitu cha kujivunia sana licha kuwa bado anaongoza, hii ni kutokana na ukweli kwamba namba zinamkataa yeye binafsi!
YouTube ni mtandao wa kucheza video ulioanzishwa Februari 14, 2005, huko San Mateo, California nchini Marekani na kwa miaka sasa umekuwa ukiwalipa wasanii wa muziki kama wanavyofanya kwa wazalishaji maudhui wengine.  

Tangu Diamond amejiunga YouTube Juni 12, 2011 amekusanya 'views' bilioni 2.1 na kuongoza ukanda huo lakini sasa rekodi yake inaanza kupoteza mvuto barani Afrika, hiyo ni ishara kuwa atakuja kuipoteza miaka michache tu ijayo.  

Kwa mfano ukitazama rekodi za wasanii waliokuja hivi karibuni kama Rema na Ayra Starr wote kutokea Nigeria, utabaini Diamond kuna sehemu amekwama licha ya hesabu za jumla kumbeba kwa miaka zaidi ya miwili.

Hadi leo hakuna video ya wimbo ambao Diamond kafanya pekee yake (solo) iliyofikisha walau 'views' milioni 100, zote ambazo zimefanya hivyo kawashirikisha wasanii wengine tena wakubwa kwake kimuziki au kwa wakati huo walikuwa wanafanya vizuri.

Diamond ana nyimbo tatu zilizofikisha views milioni 100+ ambazo ni Yope Remix akishirikiana na Innoss'B, Inama akimshirikisha Fally Ipupa na Waah! akimshirikisha Koffi Olomide, wasanii wote aliowashirikisha ni kutokea DR Congo.

Video za nyimbo ambazo Diamond kafanya pekee yake na kufanya vizuri YouTube kwa kiasi chake ni Jeje (mil. 80) na Sikomi (mil. 61), hivyo tunaweza kusema Diamond amekuwa akibebwa zaidi na kolabo anazofanya na wasanii wengine.

Hata hivyo, Rema kupitia video ya wimbo wake, Calm Down iliyotoka Februari 11, 2022 tayari imegonga 'views' milioni 412 ikiwa ni mwaka mmoja tu tangu kutoka kwake.

Ikumbukwe hata video za Diamond ambazo zimefikisha 'views' milioni 100, hakuna iliyofanya hivyo ndani ya mwaka mmoja ila Rema kafanya hivyo mara nne yake tena kwa miezi 12 tu. Rema ndiye msanii wa kwanza Afrika kufanya hivyo wakati rekodi ya Diamond ni Kusini mwa Jangwa la Sahara tu.

Remix ya wimbo huo ambayo Rema kamshirikisha Selena Gomez, video yake iliachiwa Septemba 7, 2022 na ndani ya miezi saba sasa tayari imefikisha 'views' milioni 358. Kwa mwaka 2022 Rema alikuwa ndiye mwanamuziki aliyefanya vizuri zaidi YouTube Afrika wakati Diamond hakuwa hata ndani ya 10 bora!.

Rema ndiye alichukua nafasi ya kwanza na ya pili katika orodha ya video 10 zilizotazamwa zaidi YouTube Afrika 2022, video nyingine ni Last Last ya Burna Boy (mil. 140), Buga ya Kizz Daniel (mil. 108) na For My Hand ya Burna Boy (mil. 70).

Nyingine ni Finesse ya Pheelz (mil. 61), Emiliana ya Ckay (mil. 57), Ku Lo Sa ya Oxlade (mil. 54), No Wahala Remix ya 1da Banton (mil. 53) na Rush ya Ayra Starr (mil. 52).

Hata hivyo, kwa Diamond mambo yalikuwa tofauti kabisa, video yake iliyofanya vizuri zaidi ni ya wimbo 'Mtasubiri' akimshirikisha Zuchu iliyomaliza mwaka 2022 na views milioni 22 tu.

Rema ambaye alijiunga YouTube Aprili 7, 2019 ikiwa ni miaka minane baada ya Diamond, amefikisha jumla ya 'views' milioni 991 ndani ya miaka minne tu ikiwa ni karibia nusu ya 'views' za Diamond alizokusanya kwa miaka 12.
Kwa upande wake AyraStar ambaye ni msanii chipukizi Nigeria, hivi karibuni video ya wimbo wake 'Rush' iliyotoka Septemba 26, 2022 tayari imefikisha 'views' milioni 117 YouTube ikiwa ni miezi mitano tangu kuachiwa, hizi ni rekodi za solo ambazo Diamond hana!

Ikumbukwe mwaka 2019 Yemi Alade aliandika rekodi kama mwimbaji wa kwanza wa kike Afrika kufikisha 'views' milioni 100 YouTube, ni kupitia video ya wimbo wake, Johnny iliyotoka Machi 3, 2014.

Katika orodha ya video 10 za muziki zilizotazamwa zaidi YouTube Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa muda wote, hakuna video hata moja ya Diamond, mwanzo ilikuwepo Yope Remix ila kwa sasa imetupwa nje, hivyo rekodi yake ya ujumla inazidi kukosa mvuto kabisa!

Na hizi ni nyimbo ambazo video zake zimetazamwa zaidi YouTube Kusini mwa Jangwa la Sahara; Jerusalema ya Master KG (mil. 555), Magic in the Air ya Magic System (mil. 415), Love Nwantiti ya Ckay (mil. 371), Calm Down ya Rema (mil. 358), On The Low ya Burna Boy (mil. 323), Baby On Fire ya Die Antwoord (mil. 267), Fall ya Davido (mil. 259), Ye ya Burna Boy (mil. 227), Way Maker ya Sinachi (mil. 224) na Joro ya Wizkid (mil. 220).