Rihanna awapiku Madonna, Beyonce kwa utajiri

Thursday August 05 2021
riyamapic

Mwimbaji na mfanyabiashara Rihanna

By Mwandishi Wetu

Los Angeles, Marekani (AFP). Mwimbaji na mfanyabiashara Rihanna ana thamani ya dola 1.7 bilioni za Kimarekani (sawa na Sh3.94 trilioni za Kitanzania), kwa mujibu wa jarida la Forbes la jana Jumatano Agosti 4, 2021  kitu kinachomfanya kuwa ni mwanamuziki wa kike tajiri kuliko wote duniani.

Mwimbaji huyo wa muziki wa R&B aliongeza mafanikio yake katika chati za nyimbo kwa kuanzisha biashara kubwa ya vipodozi na fasheni, akipata mapato makubwa yanayozidi mapato ya wanamuziki wengine nyota duniani kama Madonna na Beyonce.

Mzaliwa huyo wa Barbados ambaye jina lake halisi ni Robyn Rihanna Fenty, alichomoza katika anga za muziki mwaka 2005, na kutoa nyimbo zilizotamba duniani kama "We Found Love" na "Umbrella", akishirikiana na Jay-Z.

Lakini, wakati upakuaji wa nyimbo zake na mauzo ya tiketi za maonyesho yake umechangia utajiri wake, ni ufahamu wake wa biashara ambao umemfanya apae na kuingia katika orodha ya matajiri.

Forbes, ambalo mara kwa mara hukusanya orodha ya watu matajiri, jana lilisema kuwa limekadiria takriban dola 1.4 bilioni za utajiri wake zinatoka katika thamani ya mapato ya kampuni yake ya vipodozi ya Fenty Beauty, ambayo anashirikiana na kampuni ya mavazi ya Ufaransa ya LVMH.

Fenty Beauty, ambayo ilianzishwa mwaka 2017 kw alengo la kukuza upekee, huzalisha vipodozi vinavyoendana na rangi tofauti za ngozi.

Advertisement

Kampuni ya Rihanna ya kutengeneza vikuku ya Savage x Fenty, pia imechangia katika utajiri wake, Forbes imesema, ikikadiria mchango huo kufikia dola 270 milioni.

Ingawa hajatoa albamu tangu mwaka 2016, Rihanna bado ana mashabiki wengi, huku akiwa na wafuasi milioni 100 katika Instagram na Twitter.

Advertisement