Risasi zilivyokatisha uhai wa AKA

Muktasari:

  • Msanii AKA alipigwa risasi na watu wasiojulikana nje ya mgahawa aliokuwa anatarajiwa kutumbuiza usiku wa Februari 10 eneo la Florida, Afrika Kusini.

Dar es Salaam. Rapa Kiernan Forbes (35) maarufu kama AKA kutoka Afrika kusini ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana alipokuwa nje ya mgahawa mmoja jijini Durban alipokua akitarajiwa kutumbuiza.

Rapa huyo na timu yake walishambuliwa kwa risasi wakitoka mgahawani eneo la Florida Morningside jijini humo. Taarifa za kifo chake zimethibitishwa na polisi usiku wa Februari 10, 2023.

Katika tamko walilolitoa leo Februari 11, 2023, wazazi wa AKA, Tony & Lynn Forbes, wameeleza kuumizwa sana na kifo chake, huku wakiomba amani na utulivu katika kipindi cha maombolezo wakati familia ikijipanga.

Tamko lililotolewa na wazazi wake baada ya kifo chake.

Rapa huyo atakumbukwa na wasanii wengi duniani hususani wa Tanzania ambapo wakati wa uhai wake alishirikishwa katika nyimbo za wasanii wa Tanzania akiwemo Diamond kwenye wimbo wa "Make me sing" na "Don't bother" alioshirikishwa na Joh Makini.

Februari 21, 2021, AKA aliweka picha katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii Instagram akitangaza uchumba wake na mpenzi wake Nelli Tembe, lakini ilipofika Aprili 11 2021, Tembe alifariki dunia baada ya kuanguka kutoka gorofani katika hoteli moja mjini Cape Town.

Msanii huyo ameacha mtoto mmoja wa kike anayeitwa Kairo Owethu Forbes (7).