Sarafina, zao la BSS linalonogesha bongofleva

Muktasari:

  • Ni mwaka 2018 alivyoonyesha kipaji chake mbele ya umma wa Watanzania.Hii ni baada ya kushiriki shindano la kusaka vipaji (BSS).

Ni mwaka 2018 alivyoonyesha kipaji chake mbele ya umma wa Watanzania.Hii ni baada ya kushiriki shindano la kusaka vipaji (BSS).

Kipindi hicho ndio shidano hilo lilirejea baada ya kutofanyika miaka miwili ikiwemo 2016 na 2017.

Huyu sio mwingine ni Sarafina Michael au Phina ambapo amekuwa moto wa kuotea mbali na ni kati ya wasanii watano wa kike wanaokimbiza katika soko la muziki wa bongofleva.

Tangu alipoachia kibao chake cha kwanza “Sio Kitoto’ na baadaye ‘Sitaki Tena’, ‘Kushki’, ‘Pekecha’, ‘wamerudiana’ na ‘Upo Nyonyo’ ambao unafanya vizuri huko kwenye mitandao ya kijamii kuliko nyimbo zake zote kwa kutazamwa mara milioni 4 kwenye mtandao wa YouTube mpaka sasa.

Ukiachia kutoa vibao vikali Sarafina amefanya kolabo na wasanii wakubwa akiwemo Ruby , Stamina, Chege, Christian Bella, Barnaba na wiki hii amechia kibao kinachokwenda kwa jina la ‘Super Woman’ alichomshirikisha msanii mkubwa kutoka nchini Kenya, Otile Brown.

Mafanikio mengine ya Sarafina

Saraphina pia anafanya kazi katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye jukwaa la Tamasha la Sanaa na Utamaduni, Bagamoyo lililofanyika Oktoba mwaka jana.

Pia mwaka huu alikuwa miongoni mwa wasanii wachanga waliopata mgao wa mirabaha, ambapo aliondoka na kitita cha Sh1.8 milioni.

Mirabaha hiyo ilikusanywa kuanzia Julai hadi Novemba mwaka jana ambapo Sh312.2 milioni zilikusanywa kwa kazi 5924 huku wasanii 1123 wakinufaika na fedha hizo.

Kama haitoshi katika tuzo za muziki Tanzania(TMA) zilizotolewa mwaka huu alishinda kipengele cha mtumbuizaji bora wa kike na aliteuliwa na Serikali kutumbuzia wiki ya nchi ya Tanzania katika maonyesho ya biashara ya kimataifa ya Dubai ‘Dubai Expo2022’.

Akizungumza na gazeti hili kuhusu mafanikio ya nyota huyo, Mkurugenzi wa BSS, Rita Paulsen anasema anajivunia kuwa na msanii anayejituma kama Saraphina na kueleza kuwa hapo bado hajaonyesha vizuri kipaji alichonacho.

“Sisi tulimuona Saraphina tangu ameingia kushiriki mshindano ya BSS akiwa anatokea mkoani Mwanza, na tuliona kabisa ushindi akiwa anaenda kuuchukua yeye,tunashukuru hatukufanya makosa na leo ni kati ya wasanii bora wa kike wanaotajwa Tanzania,”anasema Rita.

Anasema mafanikio ya Sarafina yatawaaminisha wengine wanaotaka kushiriki BSS kuwa ni sehemu salama kwao kwenda kuonyesha kipaji na kueleza inazidi kumpa moyo kuendelea kuvumbua vipaji vingine huko mbele ya safari.

Rita anawasihi Watanzania wanaoweza kuwasimamia wasanii kujitokeza kufanya hivyo wanapotoka kwenye mashindano hayo ili kukuza vipaji vyao na kupunguza tatizo la ajira nchini, kwani watakuwa wamepata shughuli ya kuwaingizia kipato.

“Siyo lazima kuwashika mkono walioshinda pekee, wapo wanaoshiriki shindano na wana kipaji, ila si rahisi wote kushinda, hivyo hao nao wakishikwa mkono watafanya vizuri,”anasema Rita.

Baadhi ya wasanii walioshiriki BSS, lakini hawakushinda na kuendeleza vipaji vyao ni pamoja na Peter Msechu, Menina, Kala Jeremiah, Baby Madaha na Frida Amani ambaye mwaka huu katajwa kuwania tuzo za Afrimma.

Akizungumzia suala la mameneja kutowapokea wasanii hawa kama ilivyotarajiwa,Yusufu Chabuso aliyekuwa meneja wa msanii Aslay, anasema ni kutokana na mfumo mzima wa uendeshaji biashara ya muziki kubadlika.

“Zamani tulikuwa mameneja tunafanya kazi kama msaada kwa wasanii ikiwemo kuwagharamia kila kitu, lakini sasa hivi muziki umekuwa biashara kila mmoja anataka ajue akiwekeza atafaidikaje.

“Kwani siku hizi sio ajabu kuona msanii mchanga anafanya vizuri huko mitandoni hata kabla ya kuwa na meneja, hivyo nasi inatupasa tuendane na mabadiliko haya,”anasema Chambuso ambaye pia aliwahi kusimamia bendi ya Yamoto.


Waliowahi kushinda BSS

Kwa upande waliowahi kushinda na mwaka walioshinda kwenye shindano hilo yupo Jumanne Idd ambaye ndio mshindi wa kwanza wakati shindano hilo limeanzishwa mwaka 2006/2007.

Wengine ni Misoji Nkwabi (2007/2008), Pascal Cassin(2009), Mariam Mohamed(2010), Haji Ramadhani(2011), Walter Chilambo(2012),Emmanuel Msuya(2013),Kayumba Juma(2015), na 2016 na 2017 halikufanyika mpaka 2018 ambapo Sarafina kuibuka kidedea.