Serikali:Tunarudisha tuzo,hatutaangalia ‘wanaotrendi’, kuendekeza ‘kiki’ na matusi

Wednesday August 25 2021
tuzopic
By Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Serikali imetangaza kurudisha tuzo za muziki na kuonya kuwa hawataangalia nyimbo iliyotrendi siku nne, kuendekeza kiki na kuimba matusi.

Hayo yamesemwa leo na Katibu wa Wizara ya Habari,Sanaa,Utamaduni na Michezo,Dk Hassan Abbas kwenye  mkutano wa wasanii kuhitimisha mapendekezo ya kanuni ya leseni ya utangazaji na maonyesho kwa umma ya mwaka 2021.

Dk Abbas amesema maandalizi ya tuzo hizo yameanza kufanyika  ambapo  kwa kuanzia kutakuwa na tuzo za muziki na filamu.

Hata hivyo akitahadharisha kuwa katika tuzo hizo hakutakuwa na kuangalia nyimbo zilizotrendi siku nne,msanii mwenye kiki na anayeimba matusi kwenye nyimbo zake.

"Tuzo hizi zinakwenda kuwaheshimisha wasanii,hivyo kutakuwa na wataalamu katika eneo la sanaa kuangalia vigezo vinavyopaswa haswa kumpa muhusika tuzo, wale wanaoimba mashairi ya matusi,sijui nyimbo kaitoa leo inatrendi siku nne,mara kaja na kiki hii,wazisahau," amesema Katibu huyo.

Katika hatua nyingine amesema Serikali ipo tayari kuwapa ushirikiano wadau wenye nia ya kuandaa tuzo nyingine zenye mlengo huo.

Advertisement

Kuhusu ulipaji wa mirabaha kwa vyombo vinavyotumia kazi za wasanii Dk Abbas amesema wasanii watumie kama fursa katika kutengeneza kazi zilizo bora.

"Katika hili la mirabaha wasanii msiende kubweteka mkadhani sasa mifuko yenu itajaa fedha bila kuandaa kazi zilizo bora.

" Pia wananchi waelewe hii sio tozo bali ni haki ya msanii inakusanywa kwa niaba ya Serikali ikiwa ni matunda ya msanii aliyewaza na kuwazua kwa kulipeleka wazo kwenye utendaji,"amesema Katibu huyo.

Advertisement