Serikali yafuta kodi ya wasanii Youtube

Tuesday April 20 2021
Tozo pc

Katibu mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbas

By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Kuanzia sasa wasanii wa muziki wanaoweka kazi zao kwenye akaunti zao binafsi za mtandao wa Youtube hawatolazimika kusajiliwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wala kulipia ada kama ilivyokuwa miaka michache iliyopita.

Wasanii hao wametakiwa kutumia taaluma zao vizuri katika kutangaza kazi zao badala ya kuchafuana kwenye mitandao ya kijamii kwani wanao ushawishi katika jamii.

Mabadiliko hayo yametangazwa leo, Aprili 19, na katibu mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbas kwenye mkutano wake na viongozi wa Shirikisho la Filamu Tanzania (Taff).

Dk Abbas amewakumbusha wasanii hao kuwa wote wameyaona yaliyokuwa yakiendelea kwenye mitandao ya kijamii siku za hivi karibuni na kueleza kuwa hiyo inaua sanaa na wasanii wenyewe.

"Leo hata kampuni zilizoanza kuwa na imani kibiashara na wasanii zimeanza kusita, heshimuni sanaa ni maisha ya wengi na hii itawajengea heshima badala ya kiki za kuchafuana” amesema Dk Abbas.

Kwa kutafuta kiki, katibu mkuu huyo amesema wanaondoa uaminifu kwa jamii ambao wameujenga kwa gharama kubwa na muda mrefu na kuwafikisha walipo.

Advertisement

Kuhusu tozo ya Sh1 milioni waliyokuwa wanalipia kwa kuweka nyimbo zao Youtube, Dk Abbas amesema wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na TCRA wamekubaliana kubadilisha Kanuni ili wasanii na wadau wengine wa maudhui yasiyohusisha habari waweze kuzirusha kazi zao bila kutozwa chochote.

Hatua hiyo, amesema imetokana na kuona umuhimu wa kuwaruhusu wasanii kutumia majukwaa haya kukuza sanaa nchini na kuwaongezea fursa za kujiingizia kipato.

“Tumezungumza na wenzetu kuhusu maudhui ya Tv  za mtandaoni, tumeona kuna tofauti kubwa sana kati ya habari na sanaa. Hivyo, tutaboresha kanuni, tumeona wasanii wanapaswa kufanya kazi zao bure. Nafurahi kuwaambia kuanzia sasa wasanii wawe wa muziki au filamu changamoto hii imefika mwisho," amesema Dk Abbas.

Kuhusu maslahi ya kazi za wasanii zinazorushwa kwenye vyombo vya habari, amesema wizara zinazosimamia wasanii ikishirikiana na TCRA wanaendelea kupitia na kuanzisha mfumo wa kuangalia namna ya kazi zao zinavyorushwa kwenye vyombo hivyo ili waweze kulipwa kwa jinsi zinavyorushwa.

“Wizara kupitia Taasisi ya Haki Miliki Tanzania (Cosota) na TCRA tunaendelea kukamilisha mfumo wa kuwanufaisha wasanii na tayari TV na redio nyingi wamekubaliana na jambo hili,” amesema.

Advertisement