Serikali yamaliza utata tamasha la ‘Nyege Nyege’

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Uganda, Robina Nabbanja amelikingia kifua tamasha hilo na kuahidi kwamba, litafanyika Septemba 15 hadi 18, 2022 chini ya uangalizi mkali kudhibiti vitendo viovu.

Kampala, Uganda. Tamasha maarufu la kitamaduni nchini Uganda, ‘Nyege Nyege’ sasa litafanyika baada ya awali Bunge la nchi hiyo kutaka kusitishwa kwa madai ya kuruhusu vitendo vya uasherati.
Kwa mwaka huu tamasha hilo linatarajiwa kufanyika Septemba 15 hadi 18 mjini Jinja, ambapo tangu mwaka 2015 limekuwa likifanyika na kushirikisha wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Waziri Mkuu wa Uganda, Robina Nabbanja amesema tamasha hilo ambalo lilisimama kwa miaka miwili, sasa litafanyika kama ilivyopangwa.

Hata hivyo, Nabbanja amesema kuwa safari hii litafanyika chini ya miongozo ya Serikali ili kuhakikisha kile kinacholalamikiwa hakifanyiki tena.
"Tamasha litaendelea lakini chini ya miongozo madhubuti ya Serikali, tunafahamu kuwa linavutia maelfu ya wageni hivyo, hatuwezi kuikosa fursa hiyo wakati huu nchi yetu ikiendelea na juhudi za kujikwamua kutoka kwenye athari za Uviko-19," amesema Nabbanja.
Sekeseke la kuwepo au kutokuwepo kwa tamasha hilo liliibuliwa na Jumaane, Septemba 6, 2022 na Mbunge wa Tororo, Sarah Opendi baada ya kutoa  hoja ya kufutwa kwa tamasha hilo kwa madai ya kuingiza tamaduni zisizo za Kiafrika nchini Uganda.
"Watu kutoka duniani kote watakuja hapa na kuleta kila aina ya vitendo ambavyo si vya Kiafrika na visivyo vya jumuiya ya watu wa Uganda," amesema Sarah.
Hata hivyo, Waziri wa Utalii, Martin Mugarra ametetea tamasha hilo akisema wageni 8,000 tayari wamekamilisha taratibu za safari kuja Uganda kushiriki tamasha hilo.

Lakini, Spika wa Bunge la Uganda, Anitah Among akapigilia msumari wa moto akipinga kauli ya waziri huyo na kutangaza kwamba, tamasha hilo halitafanyika.
"Hatutaruhusu shughuli hiyo kufanyika, unauzaje tiketi kwa gharama za watoto wa watu? Unakuza vitendo visivyofaa nchini Uganda," amesema Spika Anitah.
Waziri wa Maadili, Rose Lilly Akello akasimama na kulieleza Bunge kuwa, wizara yake imekutana na waandaaji wa tamasha hilo na kuwapa masharti ikiwamo kutoruhusu watoto wenye miaka chini ya miaka 18 kuhudhuria.

“Tutaangalia hadi mavazi kwa watakaoshiriki kama kuna atakayevaa bila kuzingatia heshima hataruhusiwa kuingia na wale watakaohalalisha  vitendo vyovyote vya uasherati hawatakuwa na nafasi ya kufanya hilo,” amesema Akello.