Serikali yatoa onyo la mwisho kwa Rayvanny na Harmonize

Thursday April 15 2021
onyo pc
By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amewaonya wasanii wa Bongofleva, Harmonize na Rayvanny kutokana na wawili hao kurushiana shutuma mitandaoni.

Amesema wasanii hao waliofikia hadi hatua ya kutungiana nyimbo za kushutumiana huku picha za utupu zinazodaiwa kuwa za Harmonize zikisambaa mitandaoni,  wakiendelea atawachukulia hatua kali na hatakubali msamaha wao.

Waziri huyo ametoa onyo hilo leo Alhamisi Aprili 15, 2021 mkoani Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano wa wanawake waliopo katika sekta ya ubunifu ulioandaliwa na shirika la British Council na shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco).

Bashungwa amewataka wasanii kujenga umoja na mshikamano na kwamba yanayoendelea mitandaoni ni ya kitoto.

"Vitu hivyo vya kitoto vinavyoendelea wala havinifurahishi, niliwaelekeza Basata (Baraza la Sanaa la Taifa) watoe onyo nami nimerudia tena, sasa wakiendelea na tukianza kuchukua hatua asitokee mtu ananiambia waziri msamehe fulani maana mnaona wenyewe kinachoendelea.”

"Natoa wito kwa wasanii wote kuendelea kuzingatia maadili na tamaduni zetu, narudia haya  yanayoendelea huko mtaani kiukweli yananichefua, nikitoa adhabu kali asitokee mtu wa kusema fulani asamehewe," amesema Bashungwa.

Advertisement
Advertisement