Shafi Adam Shafi: Sikufikiria wazo la kitabu lingezaa filamu kubwa

Muktasari:

Vuta N’kuvute ndiyo filamu gumzo kwa sasa nchini na kwingineko baada ya filamu pekee nchini Tanzania iliyokidhi vigezo vya kuwasilishwa kwenye mchakato wa tuzo za 95 za Oscars katika kipengele cha filamu bora ya kimataifa (International Features Film) kati ya nne zilizowasilishwa kwenye kamati.

Vuta N’kuvute ndiyo filamu gumzo kwa sasa nchini na kwingineko baada ya filamu pekee nchini Tanzania iliyokidhi vigezo vya kuwasilishwa kwenye mchakato wa tuzo za 95 za Oscars katika kipengele cha filamu bora ya kimataifa (International Features Film) kati ya nne zilizowasilishwa kwenye kamati.

Vuta N’kuvute ambayo imetokana na kitabu ‘Vuta N’kuvute’ chake Shafi Adam Shafi, imetayarishwa na Kijiweni Production chini ya mwongozaji Amil Shivji, akishirikiana na Steven Markovitz ambaye ndiye mtayarishaji chini ya kampuni yake, Big World Cinema.

Akizungumza na gazeti hili Shafi Adam Shafi ambaye ndiyo chanzo cha wazo la filamu hiyo kupitia utunzi wa kitabu anasema hakuwahi kufikiria kuwa wazo lake lingekuja kuwa kubwa baadaye kwa kuingizwa kwenye filamu.

Anasema mafanikio hayo yamempa morali na ni hatua nzuri katika maendeleo ya filamu Tanzania kwani miaka ya nyuma walishakaa na kujadili namna ya kutoa simulizi za kwenye vitabu na kuziweka kwenye filamu.

“Kama miaka 10 iliyopita wakati wa tamasha la filamu Zanzibar tulikuwa na mkutano kati ya waandishi wa vitabu, wachapishaji na watengenezaji filamu.

“Tukakubaliana watengeneze filamu zilizotoholewa kutoka kwenye vitabu vya Watanzania wenyewe, nafikiri filamu hii ni katika mwitikio wa azimio hilo,” anasema.

Kuhusu msukumo wa kuandika kitabu cha Vuta N’kuvute?, Shafi anasema alilenga kuonyesha mapenzi baina ya watu wa jamii mbili tofauti, Wahindi na Waafrika.

“Kwa maisha yetu sisi watu wa Afrika Mashariki si kitu cha kawaida mwanamke wa Kihindi kupenda Mwafrika, kwa hiyo nilijaribu kuonyesha kwamba inawezekana, Muhindi akampenda Mwafrika na wakaishi vizuri.

“Na vile vile nilijaribu kuonyesha juhudi za vijana kuendeleza mapambano ya kupigania uhuru wa Zanzibar wakati ule” anasema Shafi Adam.

Ukiachana na Vuta N’kuvute, filamu nyingine zilizojitosa kwenye kunyang’anyiro hicho ni; ‘I Regret’, ‘Mungu Ndiyo Suluhisho’ na ‘Giza’ ambazo zote zimeandaliwa na Amoor Abbas.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati maalumu ya kuchagua filamu kutoka Tanzania itakayoshiriki Oscars, Dk Mona Mwakalinga anavitaja vigezo vilitumika kuifikisha hapo filamu hiyo kuwa ni

iwe imetayarishwa nje ya Marekani, iwe imeonyeshwa kwenye nchi husika kwa kipindi cha kuanzia Januari 1, 2022, hadi Novemba 30, 2022.

Anasema pia ionyeshwe angalau siku saba mfululizo katika kumbi za sinema za kibiashara kwa faida ya mtayarishaji na mwonyeshaji, ia iwe na urefu kuanzia dakika 40, iwe imetumia lugha nyingine mbali na Kingereza kwa zaidi ya asilimia 5, ikiwa na tafsiri (Subtitles) sahihi za Kiingereza, iwe katika muundo wa Digital Cinema Package (DCP) kwa ubora wa angalau 2040 kwa 1080 pixels(2k).

Anafafanua kuwa pia filamu iwe na sauti ya kipimo cha 5.1 au 7.1, au iwe yenye chaneli 3 za sauti (left, right & centre), isiwe katika PPV (Pay-Per-View) Video in Demand na filamu isiwe kwenye usambazaji wa DVD au kwenye intaneti.


Vigezo vya kushiriki

Akizungumza na Starehe, msimamizi wa ubunifu kutoka Kijiweni Production, Priscilla Mlay anasema kwao ni mafanikio makubwa na Watanzania kwa ujumla.

Anasema ni kitu kizuri kwa filamu inayoelezea historia ambayo inaakisi Utanzania kwa kipindi hicho cha miaka ya 1950 huko Zanzibar wakati wa utawala wa Uingereza.

Kwa mujibu wa Mlay, Vuta N’kuvute itakuwa ni filamu ya kwanza ambayo imepitia mgongo wa kitabu ambacho kimeandikwa na Mtanzania.

“Lengo letu lilikuwa ni kuweka sawa hii historia ili watu waione kama Watanzania, kwa sababu kilikuwa ni kitabu ambacho tulikipenda wengi tulikisoma tukiwa sekondari. Tuliona ni hadidhi na historia sahihi kwa sababu sanaa ya kuandika na sanaa ya filamu ni vitu ambavyo vinaendana.

“Tuliamua kutumia kitabu kwa sababu alichoandika Shafi ni kama yeye mwenyewe alikuwa anaunda picha kabisa, Kiswahili kilichotumika, mandhari ambayo alikuwa anayazungumzia, historia ambayo alikuwa anazungumzia kwa kweli ni mambo ambayo tuliona kupitia filamu itawafikia watu wengi zaidi,” anasema Mlay.

Je, ubora upande wa uzalishaji umechangia kwa kiasi gani kwa filamu hiyo kupata nafasi hiyo?, Mlay anasema wao wamekuwa wakitengeneza filamu hapa nyumbani kwa muda sasa, tangu walipoanza na hizo filamu fupi kama ‘Shoeshine’ na ‘Samaki Mchangani’, hivyo wamekuwa tukijijenga hata kwa hatua.

Baada ya mafanikio ya kazi zao nyingi wakaona bado kuna nafasi ya kuleta kitu kingine kikubwa zaidi, ndipo wakaamua kushirikiana na Steven Markovitz na kampuni yake ya Big World Cinema.

Anasema Markovitz ni mtu ambaye alikuwa ameshafanya filamu nyingi za Kiafrika na zimefanikiwa, hivyo alikuwa anakuja na ujuzi wake jinsi filamu za Kiafrika zinaweza kufanikiwa lakini wao walikuwa na ujuzi wa hapa nyumbani, hivyo ujuzi wa hizo pande zote mbili umesaidia kuandaa kitu chenye viwango vya Oscars.

Kwa upande wake Gudrun Mwanyika ambaye amechezaji filamu ya Vuta N’kuvute akitumia jina la ‘Denge’ , anasema kwa vigezo vilivyokuwepo moja kwa moja alitegemea wangepata nafasi hiyo.

“Kwa mwaka huu sidhani kama kuna filamu inatimiza vile vigezo, kwa hiyo ni habari njema ambayo niliitegemea kwa sababu mchakato mzima nilikuwa naufuatilia.

“Kiukweli tasnia yetu inakuwa sasa kwa sababu ni mwaka wa 21 tangu kupata hiyo nafasi ya kuweza kuwasilisha filamu, kwa hiyo naona tunarudi kwenye ramani kama tasnia. Hatutengenezi filamu tu, bali tunatengeneza tasnia ,” anasema.


Zifahamu Tuzo za Oscars

Tuzo za Oscars zimekuwa zikitolewa nchini Marekani tangu Mei 16, 1929 zinatajwa kama tuzo za juu zaidi upande wa filamu duniani, husimamiwa na AMPAS (Academy of Motion Picture Arts and Sciences).

Katika tuzo hizi hakuna fedha zozote zinazotolewa kwa washindi, lakini kuna faida kubwa kwa njia nyingine, waigizaji wanaoshinda tuzo ya Oscar hutengeneza fedha zaidi pale filamu zao zinapotafutwa na watazamaji wengi baada ya kutajwa kuwania au kushinda.

Kwa mujibu wa tovuti ya Oscars, tuzo hizo zimetengenezwa kwa dhahabu halisi yenye uzito wa karati 24 na ni kosa kisheria kuiuza.

Oscars katika academy yao wana vipengele vitano vikuu “Big Five” hivi ni vile vya; Picha Bora (Best Picture), Muongozaji Bora (Best Director), Muigizaji Bora (Best Actor), Mwigizaji Bora wa Kike (Best Actress) na Mswaada Bora wa Filamu (Best Screenplay).

Hadi kufikia tuzo za 94 za Oscars (2021) jumla ya filamu 43 zimeteuliwa katika vipengele vyote vitano vya tuzo hizi, lakini ni filamu tatu pekee ambazo zimeshinda tuzo zote tano kuu:

Filamu hizo ni ‘It Happened One Night’ (1934), ‘One Flew Over the Cuckoo’s Nest’ (1975) na ‘The Silence of the Lambs’ (1991), huku filamu nane zikishindwa kushinda tuzo yoyote katika vipengele hivyo vikuu baada ya kuteuliwa katika kila kipengele.

Miongoni mwa wasanii wa Afrika waliowahi kushinda tuzo ya Oscars ni Lupita Nyong’o kutokea Kenya, Tsotsi wa Afrika Kusini na Daniel Kaluuya toka Uingereza mwenye asili ya Uganda.

Hattie McDaniel anashikilia rekodi kama Mwafrika na mtu mweusi wa kwanza kushinda Oscars hapo mwaka 1940, huyu alikuwa mwigizai, mwandishi na mchekeshaji huko Marekani. Alizaliwa Juni 10, 1893 na kufariki Oktoba 26, 1952 akiwa amecheza filamu zaidi ya 300.

Kwa mujibu wa Jarida la Essence, takribani watu weusi 20 ndio wamefanikiwa kushinda tuzo za Oscar ukiachana na na Hattie McDaniel, wengine ni Will Smith, Ariana DeBose, Ahmir “Questlove” Thompson, Samuel L. Jackson, Tyler Perry, H.E.R, Travon Free, Jon Batiste, Matthew A. Cherry & Karen Rupert Toliver.

Wengine ni Spike Lee, Regina King, Mahershala Ali, Kobe Bryant, Jordan Peele, Tarell Alvin McCraney & Barry Jenkins, Viola Davis, Common & John Legend na Steve McQueen, hawa wote wana asili ya Marekani, kisha kuna Daniel Kaluuy na Lupita Nyong’o.