Sho Madjozi: Natamani kuiona Bongofleva ya zamani yenye biti za kisasa

Muktasari:

Sho Madjozi anafanya vizuri katika anga ya kimataifa na ngoma kama ‘Chale’, ‘John Cena’, ‘Huku’ na ‘Wakanda forever’, ameiambia Mwananchi kuwa anatamani kuona Bongofleva ya kitambo katika usasa.

Nakumbuka muziki wa kizazi kipya wa miaka ya 1999 mpaka 2000. Ilikuwa ni Bongofleva yenye ladha za Bongo hasa, tofauti an sasa ambapo umekuwa ukichanganywa na muziki kutoka kwenye mataifa mbalimbali.

Ngoma za wakali wa enzi hizo kama Marlaw, Jay Mo, Z Anto, Berry Black au Mb Dogg, ngoma zao mpaka leo ukizisikiliza unazipenda.

Lakini mabadiliko ya muziki yaliyopo sasa uamemuibua msanii kutoka Afrika Kusini, Maya Wegeref, maarufu Sho Madjozi anayesema kuwa ladha halisi ya Bongofleva imepotea.

Sho Madjozi anafanya vizuri katika anga ya kimataifa na ngoma kama ‘Chale’, ‘John Cena’, ‘Huku’ na ‘Wakanda forever’, ameiambia Mwananchi kuwa anatamani kuona Bongofleva ya kitambo katika usasa.

“Mimi nimekuja hapa mwaka 2008, kipindi ambacho Bongofleva ilikuwa ndio inapamba moto, kipindi hicho Alikiba alikuwa ametoa album yake, ulikuwa ndio muda wa Cinderella, Mac Muga, Kidato Kimoja, Anita, yaani ladha halisi ya miondoko kutoka Bongo Tanzania. Baada ya hapo, 2010 Diamond akaja na Mbagala, lakini sasa ni ngumu kupata wimbo mpya wenye ladha ile.

“Hata kabla ya Amapiano kuingia watu walianza kuchukua midundo, melodi na staili za Nigeria, mpaka ikafikia hatua unashindwa kujua kama ni nyimbo ya Kibongo kwa sababu mpaka matamshi wanaiga. Nafikiri kuchukua vitu sio vibaya ila ningependa kuona Watanzania wanakuja na nini, yaani staili yao wenyewe,” anasema Madjozi.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Madjozi anasema hali hiyo kidogo haifurahii. “Huwa nakuja huku mara kwa mara, kun wakati nakuja na washikaji tukienda klabu usiku mwingi wanashindwa kutofauti tukiwa Bondeni (Afrika Kusini), na Bongo Tanzania kwani ngoma zinazopigwa na kuchezwa ni Amapiano mwanzo mwisho.

“Natamani nikiwa huku nipate ladha tofauti ya muziki ule ninaoujua wa Bongofleva hata washikaji zangu waliwahi kuniuliza kuhusu hili, siku na majibu. Pengine mabadiliko ya soko lakini kulinda cha kwenu ni bora zaidi,”anasema.

Anasema anapenda sana lugha ya Kiswahili, “Mimi napenda kuimba kwa Kiswahili kwa sababu ni kitamu sana.

Anaeleza namna alivyoishi nchini akisema kuwa walihamia akiwa na umri wa miaka 16 baada ya baba yake kuhamishiwa kikazi. Anasema wazazi wake waliishi hapa nchini miaka saba, ila yeye alikaa miwili kisha nikaenda chuo. “Tanzania ni moja ya nchi nzuri sana, na Watanzania wanasahau kama wana nchi nzuri, kipindi hicho nipo na familia yangu ndiyo nilijifundisha Kiswahili na nilikipenda hivyo sikuwahi kukiacha.

“Huwezi kuamini nilijifundisha mtaani tu, sikuwa na mwalimu wala sikwenda shule kukisomea, nilikipenda nikajifunza nikajua kiasi,”anasema Sho Madjozi.

Kuna maneno mengi ya Kiswahili ambayo yanafanana na lugha ya kizulu, mfano neno ‘tunafanana’ kwa kizuru tunasema ‘siafana’.

Sh Madjozi ambaye ni mzaliwa wa Limpopo mwenye taaluma ya ‘Uandishi wa ubunifu na masomo ya Kiafrika’ kutoka katika chuo cha Mount Holyoke, Massachusetts, Marekani, anasema mashabiki wamempokea vizuri kwenye muziki hususani Watanzania.

”Nilipotoa albamu yangu ya kwanza ‘Limpopo Champions League’, ilikuwa ni kubwa sana, nakumbuka nyimbo ya ‘Huku’ ilikuwa kubwa mpaka ikapata nafasi ya kujulikana Tanzania,”anasema.

Anasema mpaka sasa ameshinda tuzo kadhaa za nyumbani huku ya nje kubwa ikiwa ya BET.

Kuhusu kupenda kuvaa mavazi ya kung’aa Madjozi anasema anatoka kwenye kabla la Tsonga hivyo yeye ni Vatsonga. “Hata safari yangu ya muziki nilianza kwa kufanya nyimbo za Tsonga na mitindo ya asili hiyo pia.

“Kabila letu sisi tunapenda sana rangi zinazong’aa ndio maana hata nywele, nguo zangu unaona zipo hivyo, yaani napenda sana rangi, bibi yangu huwa anasema mtu hajavaa akapendeza kama nguo inakosa rangi ya njano,”anasema Sh Madjozi huku anacheka.

Anasema aliamua kuchukua miondoko ya Tsonga ili kuja na kitu tofauti. “Kwa nini uingie kwenye muziki kufanya vitu ambavyo watu wengine wanafanya kila siku?

“Kwa hiyo niliamua kuja na staili hii ili kuwa tofauti, mfano niliamua kuja na staili ya kutumia nyimbo yenye biti za Afrika Kusini na kuimba kwa lugha ya Kiswahili, hii ni kutokana na watu wa Afrika Mashariki wanapenda sana muziki wetu kwa ajili ya kucheza ndio nikaamua kuileta kwa lugha yao,”anasema.

Madjozi anasema anapenda sana kusafiri na kujifunza vingi kutoka Afrika. “Napenda kuandika vitabu na kusuka nywele kwa sababu naelewa sana, siku zijazo nitaanzisha ‘brand’ yangu ya nywele, niandike vitabu na movie.

“Tayari nishaandika kitabu changu cha watoto ambacho kinaitwa ‘Shoma and the stars’ kinauzwa Afrika Kusini, ila mwakani nataka nikiweke kwa Kiswahili ili tuuze huku pia. Pia nataka kitabu hicho nikitayarishie filamu.

Anasema pia anataka kufanya filamu zinazohusu masuala ya haki za binadamu.