Siku 730 tangu Vee Money aitose Bongofleva

Sunday July 24 2022
vmoneypic
By Peter Akaro

Ni zaidi miaka miwili yenye takribani siku 730 bila sauti ya Vanessa Mdee kusikika kwenye Bongofleva tangu kutangaza kuachana na muziki hapo Julai 2020 katika Podcast yake, kwa kile alichodai ulimuingiza katika maisha yasiyofaa kama ulevi wa kupindukia na msongo wa mawazo.

Kwa sasa Vee Money anaishia Georgia, Marekani na mchumba wake Rotimi ambaye kwa mara ya kwanza walikutana Julai 2019 kwenye Tamasha la Essance nchini Marekani, ambapo wote walitumbuiza. Ameshinda tuzo za KTMA, AFRIMA na AFRIMMA, huku akianzisha lebo yake, Mdee Music iliyokuja kuwasanii wasanii Mimi Mars na Brian Simba.

Mwaka 2017 alikutana na Rais wa Gabon, Ali Bongo walipokuwa wakirekodi project ya ‘The African Queens’ ya Rais huyo pamoja na msanii mkongwe nchini humo, Frederic Gassita. Albamu yake ya pili alieleza angeitoa chini ya Universal Music Group (UMG) baada ya kusaini nayo mkataba Desemba 2017 akiwa ni msanii wa pili Tanzania, baada ya Diamond Platnumz lakini haikuwa hivyo.

Novemba 2020 Vee alionekano kwenye video ya wimbo wa mchumba wake, Rotimi, ‘Love Somebody’ na kuibua uwezekano wa Staa huyo kurejea kwenye muziki lakini hadi sasa hajafanya hivyo.

Vanessa kwa sasa ni mama wa mtoto mmoja, Seven aliyezaliwa Septemba 2021 na kubadili mfumo mzima wa maisha ya staa huyo, na kupitia mitandao ya kijamii tayari amegusia mpango wa kumpatia Seven mdogo wake.

Kabla ya muziki mwanamama huyu alikuwa mtangazaji wa Redio na TV, na kufanikiwa kufanya mahojiano na wasanii wakubwa duniani kama Kelly Rowland, Rick Ross, Ludacris na wengineo.

Advertisement

Hiyo ilikuwa ni kati ya mwaka 2007 na 2011 ambapo alifanya kazi na MTV na Choice FM.

Advertisement