Simulizi za muxiki: Enzi zetu kulikuwa na Ma Yea Men, slimfit, Bell bottoms’ na afro

What you need to know:

Mwishoni mwa miaka ya 60, vijana wengi wa Kitanzania waliingia katika upenzi wa utamaduni wa Magharibi na hasa Wamarekani weusi. Vijana walijitahidi kuvaa,kuongea, kutembea kama Wamarekani weusi na waliobobea zaidi waliitwa ‘Ma Yea Men’.

Na Anko Kitime

Mwishoni mwa miaka ya 60, vijana wengi wa Kitanzania waliingia katika upenzi wa utamaduni wa Magharibi na hasa Wamarekani weusi. Vijana walijitahidi kuvaa,kuongea, kutembea kama Wamarekani weusi na waliobobea zaidi waliitwa ‘Ma Yea Men’. Walipewa sifa hiyo kwani kila walipokuwa wakizungumza walimalizia sentensi zao na neno ‘Yea man’. Wavulana na wasichana wa kundi hili wote walifuga nywele na kuzichana kwa mtindo ulioitwa Afro. Haikuwa kazi rahisi kutunza nywele hizi, kwani zililazimika kunyooshwa na kitana cha chuma kilichokuwa kimepashwa moto, wengi walikuwa na makovu ya moto kwenye masikio kutokana na shughuli hiyo. Aliwahi kutokea mwanamuziki aliyeitwa Isaac Hayes ‘Black Moses’, aliyekuwa ananyoa kipara na kuacha ndevu zake, jambo hilo likaanzisha utamaduni wa kunyoa kipara na kufuga madevu kumuiga mwanamuziki huyo.

Kwa upande wa mavazi, ‘ma Yea men’ walikuwa wakivaa mashati yenye kola kubwa na yenye kubana sana yaliyoitwa ‘slimfit’, huku chini wamevaa suruali zilizobana kiunoni na kwenye mapaja na kuwa pana kuanzia kwenye magoti, suruali hizi ziliitwa ‘Bell bottoms’.

Chini kabisa walivaa viatu vyenye visigino virefu, vilivyoitwa ‘platform shoes’. Urefu wa visigino ulilazimisha kuweko na miandoko ya aina yake wakati wa kutembea.

Filamu kama Shaft, Three the Hard way, Foxy Brown, Super fly, zikiwa na wasanii kama Richard Roundtree, Jim Brown, Fred Williamson, Pam Grier, zilifanya kumbi za filamu kufurika kila zilipoonyeshwa.

Gazeti maarufu la Ebony ndilo lilikuwa chanzo kikubwa cha kuangalia mishono ya nguo mbalimbali. Mafundi cherehani wajanja walikuwa na magazeti hayo na kila kijana alipofika na kitambaa chake kushonesha nguo mpya, alipewa magazeti haya achague aina ya mshono alioutaka.

Taasisi ya kimarekani ya United States Information Services (USIS) nayo ilifanya kazi kubwa ya kutangaza utamaduni wa huo kwa kuwaleta wanamuziki waliokuwa juu wakati ule kama Staple Singers na Buddy Guy ambao walifanya maonyesho bure katika viwanja vya Mnazi Mmoja.

Bendi nyingi za vijana zikawa zinajitahidi kuiga nyimbo kutoka Marekani na hata majina ya bendi zao yalitokana na majina ya bendi za huko. Baadhi ya bendi zilizokuweko ni Comets, Sparks, Groove makers, Flames, Jets, Dynamites na vingine vingi vilivyotapakaa nchi nzima. Tamko la kupiga marufuku muziki wa soul lililotolewa na Mkuu wa mkoa wa Pwani lilifuta asilimia kubwa ya vikundi hivi, ambavyo vingi vilikuwa vya wanafunzi wa shule za sekondari.

Kuna vikundi viwili bado vipo hai mpaka leo vilivyotokana na enzi hizo navyo ni The Tanzanites na Kilimanjaro Band. Tanzanites awali walikuwa wakiitwa Barkeys. Ilikuweko na bendi ndugu, iliyoitwa Barlocks.

Mwanzo mwa miaka ya sabini kundi la vijana wa Kigoa wa mjini Tanga walianzisha bendi yao wakajiita The Love Bugs. Jina hili lilitokana na filamu moja maarufu wakati huo iliyoitwa The Love Bug, iliyokuwa ikiongelea hadithi iliyohusu gari aina ya Volkwagen. Baada ya muda kundi hili likawa na mchanganyiko wa vijana wa Kigoa na Kitanzania, akiwemo marehemu Mabruk Khamis Omari ‘Babu Njenje’ na Mohamed Mrisho, kundi hili lilikuwa likipiga nyimbo za wanamuziki hasa kutoka Ulaya na Marekani. Love Bugs likiwa na mwanamuziki mwingine mpiga kinanda Waziri Ally, likabadili jina na kujiita The Revolutions. Kundi likahamia Dar es Salaam na kujikita kupiga kwenye mahoteli makubwa ya wakati huo. Umahiri wa wanamuziki wake uliliwezesha kundi lao kuwa katika nafasi ya juu miongoni mwa bendi zilizokuwa zikipiga kwenye mahoteli jijini Arusha na Dar es Salaam.

Mwaka 1989 bendi iliamua kuhamia Uingereza katika jiji la London na ili itambulike kuwa imtoka Afrika tena Tanzania ikabadili jina na na kujiita Kilimanjaro Band na kutoa albamu yake ya kwanza iliyoitwa ‘Kata kata’ ikiwa na nyimbo zenye mchanganyiko wa mahadhi na lugha. Wimbo uliobeba jina la albamu , ulikuwa ni wa Kiingereza uliotungwa na mpiga kinanda Waziri Ally na walirekodi wimbo ulioitwa ‘Njenje’, ambao unapendwa hadi leo na pia kusababisha bendi hii kuitwa Wananjenje. Bendi hii inakaribia umri wa miaka 45, na mpaka leo yupo mwanamuziki mmoja alikuweko toka ikiitwa the Love Bugs naye ni mpiga gitaa Mohamed Mrisho maarufu kwa jina la Moddy.

Katika uhai wake, Kilimanjaro Band imekwisha piga muziki kwenye sherehe za harusi za watoto wa maraisi wa nchi wa kwanza wote wanne. Bendi imewahi kufanya maonyesho katika nchi mbalimbali ikwemo Japan, Korea Kusini, Uingereza, Oman, Kenya na kadhalika. Jambo la kufurahisha ni kuwa kuna vijana wameanza kupokea ujuzi kutoka kwa wakongwe waliopo ili kuendeleza historia ya bendi hii. Nyimbo kadhaa za bendi hii zimeanza kurudiwa na vijana wa muziki wa kizazi kipya na kushiriki kurekodi na wanamuziki vijana kama MwanaFA na Kassim Mganga na imeshafikisha albamu nne.

Nyimbo kama ‘Gere’, ‘Tupendane’, ‘Kinyaunyau’, ‘Boko’. ‘Kachiri’ bado zinachezwa katika vituo vya redio nchini japo zilirekodiwa zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Mei mwaka 2020, Kilimanjaro Band ilipata pigo kubwa baada ya mwanamuziki mwanzilishi Mabruk Khamis Omari ‘Babu Njenje’ kufariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu. Mabruk alipata kiharusi Disemba 9, 2013 akiwa anajitayarisha kwenda kwenye onyesho la bendi yake kusherehekea siku ya Uhuru, mwaka mmoja baadaye , Julai 2021 mwanamuziki kiongozi wa Kilimanjaro Band na mpiga kinanda Waziri Ally akafariki kwa matatizo ya moyo akiwa njiani anapelekwa katika Hospitali ya Mwananyamala. Kwa miezi kadhaa baada ya hapo bendi hii kongwe ikawa imepigwa na ganzi, lakini sasa imeanza mazoezi makali na Septemba 24 itafanya onyeso lake la kwanza jijini Dodoma, ikiwa pia na vijana wadogo ambao wanategemewa kuendeleza jahazi hili kongwe.