Siri nyuma ya majina ya mastaa bongo

Sunday September 12 2021
majina pc
By Peter Akaro

Umekuwa ni mtindo wa kawaida sasa kwa wasanii wa Bongofleva kujipachika majina ya wanyama wakali na wababe mwituni kwa lengo la kudhihirisha ukubwa na umaarufu wa muziki wao.

Hata hivyo si wote hutumia majina ya wanyama wakali, mathalani Mr. Blue anatumia jina la nyani mzee, akiwa na maana ya kuwa amekwepa mishale mingi ndani ya Bongofleva hadi kufikia alipo sasa. Huku Young Lunya akijiita mbuzi, Fid Q anajiita mzee mbuzi, yaani (G.O.A.T) akimaanisha the Greatest of All Time.

Baadhi ya wasanii wanaotumia majina ya wanyama wakali ni Diamond Platnumz (simba), Harmonize (tembo), Rayvany (chui), Country (fisi), Dubu Baya (mamba) na Afande Sele (simba) ambaye ndiye alianza kutamba na mtindo huo.

majina pcc

Utamaduni huo unazidi kushamiri kwa kizazi cha sasa ukilinganisha na wakongwe ambao walipenda zaidi kutumia vyeo kama Komando, Inspector, Professor, Doctor n.k.

Kutokana na majina ya wanyama wakali kuwa machache, kumekuwa na ushindani na unyang’anyi wa majina hayo, mfano jina la Simba alianza kulitumia Afande Sele, akafuata Mr. Blue na sasa lipo kwa Diamond, jina Tembo alilitumia Alikiba kwa kipindi kifupi alipokuwa balozi wa kukomesha ujangilili chini ya WildAid, na sasa jina hilo lipo kwa Harmonize.

Advertisement

Mwimbaji Nurdin Ali Bilal, maarufu Shetta ambaye alianza kutumia jina la Mamba, alijikuta akiambulia vitisho kutoka kwa Dudu Baya aliyedai msanii huyo hana sifa wala mamlaka ya kujipachika jina hilo analotamba kuwa ni lake kwa miaka mingi.

Lakini wasanii wa kike hawaonekani sana katika hilo, mrembo Nai aliyetambulika kama video vixen na sasa anafanya muziki, anajita Chui Jike, ameliambia gazeti hili amefanya hivyo kutokana na mapenzi yake kwa mnyama huyo tu.

“Nampenda Chui kwa sababu ni mnyama mzuri kimuonekano, anavutia, sio kwamba inaongeza kitu kwenye chapa yangu bali ni kama mrembo tu. Kuna mwingine anaweza kujiita ‘sweet baby’ lakini sisi hatuwezi hayo, si unajua sisi ni wanyamwezi, ndio nikaona Chui linanifaa zaidi,” anasema Nai.

Kwa upande wake, Queen Darleen anasema ameshindwa kujipa jina la mnyama kutokana yale makubwa na yanayosifika yameshachukuliwa na kama kutakuwa na ulazima wa yeye kufanya hivyo, basi atatumia jina la Nungunungu au Karunguyeye.

“Unajua kila anachofanya msanii ana lengo lake, kuna shabiki muda mwigine hajisikii kukuita Queen Darleen, anataka tu kukuita Nungunungu, kwa hiyo inaleta ladha fulani,” anasema Darleen.

Hata hivyo, msanii Bonge la Nyau anasema aliamua kujiita jina hilo wakati anaanza muziki wala hakufikiria hayo majina ya wanyama.

“Nilikuwa nafikiria nitoke vipi kimuziki ili niwe tofauti na wengine, likaja wazo la jina tofauti pia,” anasema Bonge la Nyau na kuongeza:

“Haya majina mwisho wa siku ni kuchangamsha tu muziki, ila haina athari yoyote kama una wimbo mbaya, haisaidii,” anasema.

Bonge la Nyau anaongeza kuwa: “Unajua chapa ya msanii inakuzwa na kazi zako na matukio yako, ila jina jipya linakuwa linachangamsha, ukitoa wimbo unajipa jina jipya ndio maana Profesa Jay ana majina hata 15”.

Akizungumzia suala hilo na gazeti hili, Country Boy kutoka Konde Music Worldwide ambaye anajiita Fisi, anasema ametumia jina hilo kutokana na tabia za mnyama huyo ambazo zinashabihiana na mwenendo wake katika muziki.

majina pccc

“Ni tafsiri ya kile ambacho unakifanya kwenye muziki, mimi nimejiita Fisi kwa sababu ni mnyama anakwenda polepole na mpole, lakini ana njaa na haachi kitu, anakula hadi mifupa. Hivyo mimi nina njaa ya muziki wangu, nafanya chochote kile, naweza kubadilika kila wakati, ndiyo sababu ya kujipa jina hilo,” anasema Fisi, maarufu Country Boy na kufafanua:

“Haiongezi chochote, ni kujitengenezea tu usikivu kutoka kwa mashabiki, unajua kuna mtu akijisikia umejiita Fisi atataka kufuatilia muziki wako ajithibitishie kwa nini amejiita hivyo. Haina athari yoyote, hata ukijipa majina zaidi ya 10, hapa ni muziki mzuri kwanza halafu majina ndiye yanafuata baadaye,” Country Boy ameliambia gazeti hili.

Advertisement