Suala la Zuchu kulalamika kudhalilishwa, lipo hivi kisheria!

Muktasari:

Kwa muda sasa uzalilishaji, unyanyasaji na ukatili wa kijinsia sio jambo ngeni katika mitandao ya kijamii, mara kadhaa watu maarufu kama wasanii wa muziki na filamu wamekuwa wakilengwa sana kwa sababu anayefanya hivyo anaamini kuna faida za kimtandao atakazozipa au kushusha chapa ya muhusika.

Kwa muda sasa uzalilishaji, unyanyasaji na ukatili wa kijinsia sio jambo ngeni katika mitandao ya kijamii, mara kadhaa watu maarufu kama wasanii wa muziki na filamu wamekuwa wakilengwa sana kwa sababu anayefanya hivyo anaamini kuna faida za kimtandao atakazozipa au kushusha chapa ya muhusika.

Juni 2021 chini ya Baraza la Usawa la Umoja wa Mataifa, wanawake 200 wenye hadhi ya juu duniani walisaini barua ya wazi kutaka hatua kali kuchukuliwa mara moja katika mitandao kama Google, TikTok, Facebook na Twitter kukabiliana na vitendo hivyo.

Miongoni mwa waliotia saini ni Waziri Mkuu wa zamani wa Austaralia, Julia Gillard, waigizaji filamu wa Uingereza, Thandiwe Newton na Emma Watson pamoja mcheza tenisi mstaafu wa Marekani, Billie Jean King.

Watendaji wa mitandao huyo walielekezwa kutoa kipaumbele kwa usalama wa wanawake ambao uchunguzi wa mwaka 2020 uliojumuisha wanawake 4,000 ulibaini asilimia 38 kati yao katika nchi 51 wamekumbwa na madhila hayo.

Wiki hii mwimbaji wa Bongofleva kutoka WCB Wasafi, Zuchu alilalamikia kitendo cha yeye na mama yake mzazi, Khadija Kopa kudhalilisha mtandaoni kwa kutolewa maneno yasiyofaa.

“Mimi ni binti mwenye ndugu, marafiki na familia inayonizunguka lakini pengine pia ni kioo kwa watu kadhaa, mama yangu mzazi ni nguli aliyeipa tasnia hii heshima, kashiriki kampeni toka za Mwalimu Nyerere mpaka Rais wetu wa sasa mpendwa, Mama Samia, hajawahi mdhihaki mtu na si mgomvi.

“Nipo kwenye mazungumzo na taasisi zinazojihusisha na haki za wanawake, bado natafuta muongozo sahihi kama mpo naomba ushiriakiano wenu. Mimi si mkamilifu kweli lakini kuongelea maumbile yangu na ya mzazi wangu na kutudhalilisha kwa lengo la kujipatia faida ya kimitandao, sidhani kama ni sahihi, TCRA naomba muongozo,” aliandika Zuchu kwenye mtandao wa Instagram, baada ya mtumiaji mmoja wa mtandao huo kueleza maumbile ya mama yake katika lugha isiyofaa.

Hata nchini kuna sheria ya makosa ya kimtandao (cyber cribe act) 2015 na ile ya maudhui mitandaoni (online content regulation) 2020, zote zimejielekeza kulinda na kuzuia ukatili wa kijinsia mtandaoni. Na kwa kulichambua hilo, Starehe imefanya mahojiano na baadhi ya watu;


Kisheria

Wakili Emmanuel Sosthenes ambaye ni Mwanasheria na Mtetezi wa Haki za Binadamu amesema katika malalamiko aliyoyatoa Zuchu kuna jinai na madai, lakini kwa sababu amemdhalilisha, yanaegemea zaidi upande wa madai kwa sababu ameshakuwa ni msanii mkubwa, kwa hiyo maneno kama hayo yanamshushia heshima yake kwa jamii.

Anasema kisheria Zuchu anaweza kuomba fidia ya udhalilishaji mahakamani, kwa shauri la madai la kawaida kwamba picha au chapa yake imeharibiwa kutokana na maneno yaliyotolewa dhidi yake.

“Mahakama ikipitia madai na kuthibitisha kuna ushahidi, kama amedai mabilioni ya fedha, mdaiwa atatakiwa kutekeleza amri ya Mahakama kulipa hiyo fedha,” anasema.

“Kama hana mpeleka shauri ana njia nyingine za kimahakama za kufanya ikiwemo kukazia hukumu, kuomba kifungo cha madai au kukamata mali yoyote ya mlalamikiwa ambayo inakaribiana na thamani ya hicho kiwango cha fedha,” anasema Sosthenes.

Hata hivyo, anasema anaweza kumpa nia kutaka kufungua shauri (demand notice), kumuomba yule mtu aidha aombe radhi, au anampa siku kadhaa aombe radhi au atoe fidia fulani kwa muda fulani. Hiyo ni nje ya Mahakama.

“Lakini pia maneno aliyotoa huyu bwana inaweza kuwa ukatili wa kijinsia, yale maneno yamemuathiri kisaikolojia, kwa hiyo anaweza kwenda kufungua shauri la jinai polisi,” anasema.

Anaongeza jinai utaratibu wake ni tofauti kidogo, shauri ni lazima likafunguliwe polisi ambapo kutafanyika uchunguzi kama kosa limetendeka na ushahidi upo, utapelekwa mahakamani. Adhabu inaweza kuwa ni kifungo, faini au vyote kwa pamoja.


Kisaikolojia

Mwanasaikolojia Modesta Kimonga anasema iwapo mwathiriwa wa vitendo hivyo hatapata washauri wazuri hali ya kuweza kujikubali inaweza ikashuka kwa sababu yeye ni kioo cha jamii na watu wengi wanamuamini.

“Athari hazitokei kwake pekee yake, hata watu waliokuwa wanamchukulia kama mfano wao, pia wataachana na hilo wazo. Watu hao wanaweza wakapoteza mwelekeo kwa sababu yule mtu ambaye wanamuona kama kioo chao anapata maoni hasi, inaweza kuwaathiri na kuacha kumzingatia,” anasema Modesta.

Kuhusu matukio ya kuvuja video za faragha za wasanii mtandaoni na baadhi ya watu kushabikia, Modesta anasema hilo linaathari kubwa kwao kutokana intaneti haisahau. Na kusema wao ndio wanazivujisha, inaweza kuwa ni kweli au sio ila hilo pia linaweza kuwa tatizo la kuathirika kisaikolojia kunakotokana na umaarufu.

“Upande wa saikolojia tunaamini kuna ule umri wa kujitafakari (appreciate and regret), kama vitu vizuri ulifanya anaweza kujipongeza kweli hapa kuna alama niliacha, kama utakuwa kwenye hali ya kujutia utapata kujitafakari ni watu wangapi walikuamini na ukawaangusha,” anasema.


Basata wanena

Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Taifa (Basata), Dk Kedmon Mapana ameliambia Starehe udhalilishaji na ukatili wa kijinsia katika mitandao ni jambo ambalo linapaswa kukemea na kila mtu kuanzia majumbani.

“Ni kosa la jinai ambalo kila mtu anatakiwa kulikemea, mimi wewe na kila Mtanzania, kwa hiyo unyanyasaji wa kijinsia sio suala la kulifumbia macho, na hili suala sio Basata tu, ni kila mtu anatakiwa kulikemea,” anasema Dk Mapana.

Alipoulizwa kuhusu video za faragha za wasanii kuvujishwa kwenye mitandao mara kwa mara kama Basata walishakaa na wasanii kuwapa elimu, Dk Mapana anasema hilo ni suala pana, linaanzia nyumbani kwa kila mtu na ni jukumu la wote kulikemea na sio Basata pekee yao.


Wasanii wafunguka

Baada ya Zuchu kutoa malalamiko yake mtandaoni, baadhi ya wasanii wamekuwa na maoni tofauti ya kulaani tukio hilo na kutaka hatua za kisheria kuchukuliwa. Haya ni baadhi ya maoni hayo;


Rosa Ree

Haya ni makosa sana! mbali na kuwa mtu mwenye chuki nyingi na asiyependa wanawake, anamkosea vipi heshima hivyo mama mtu, inasikitisha jinsi watu watakavyoweka ushabiki kwenye hilo, achukuliwe hatua huyu!. Zuchu wewe ni mrembo na mama yako ni malkia.


Miriam Odemba

Hapana kwani yeye ni nani anaishi wapi ? mbona anatabia mbaya sana, kwa nini atusi watu ambao hata hujawahi kuwashika mkono, sio poa kabisa, imetosha sasa. Hizi kiki sasa sitawatokea puani sio vyema kumsema mama na mtoto, hapana sijapenda kabisa kabisa. Huyu tunaomba aombe msamaha.