Tamasha la muziki kukusanya wasanii Dar, Bagamoyo

Tuesday October 05 2021
tamasha pc

Mwakilishi wa Barza la Sanaa Tanzania (Basata), Ibrahim Ibengwe akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.

By Elias Msuya

Dar es Salaam. Wanamuziki wapatao 180 wa kimataifa kutoka kwenye makundi 16 wanatarajiwa kufanya tamasha la muziki la siku nne la Marafiki (Music Festival) jijini Dar es Salaam na Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani Oktoba 7 hadi 9 mwaka huu.


Akizungumzia tamasha hilo leo Oktoba 5, Mkurugenzi wa Marafiki Music festival, Isack Abeneko amesema awali walipokea maombi ya makundi 180 lakini waliyachuja hadi kufikia 16 wakilenga kupata wanamuziki mahiri zaidi.


Amesema tamasha hilo litakalofanyika kuanzia Oktoba 7 hadi 9 litakuwa pia na warsha kwa wanamuziki Watanzania na wa mataifa mengine ya jinsi ya kufanya biashara ya muziki.


“Muziki ni biashara, lakini ukiwauliza baadhi ya wanamuziki kama wanafaidika, hawana majibu ya kuridhisha. Kwa hiyo tutawafundisha wanamuziki jinsi ya kufanya biashara na jinsi ya kujiunga na majukwaa ya muziki ya kimatraifa,” amesema Abeneko.

tamasha pcc


Katika tamasha hilo alisema watawafundisha wanamuziki ya jinsi ya kuandaa wasifu kwa kuweka safu ya kazi zao, picha mnato na za video na anwani zao, ili iwe rahidi kutafutwa hasa katika matamasha ya nje ya nchi.

Advertisement


Akifafanua zaidi, Abeneko amesema malengo ya tamasha hilo ni pamoja na kuwawezesha wanawake kufanikiwa kimuziki na pamoja wanamuziki wengine wanaotafuta kufika mbali.


“Kwa dhana ya kidemokrasia, muziki hutoka kwa watu wenyewe na pia Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema, ‘Taifa lisilokuwa na utamaduni, limekufa.” Alisema
Mwakilishi wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Ibrahim Ibengwe amewataka wadau kujitokeza kudhamini matamasha hayo ili kukuza utamaduni wa Mwafrika.


Naye mwakilishi wa Ubalozi wa Ufaransa wanaodhamini tamasha hilo, Sumaiya Jaffar alisema wametoa udhamini kwa kuwa linawaleta watu karibu kwa ajili ya kujenga fikra chanya.

Advertisement