Thamani gauni la Lulu unanunua IST mbili

Wednesday February 17 2021
Lulu pic
By Kelvin Kagambo

Dar es Salaam. Kama ni mfuatiliaji wa mitandao ya kijamii hakika utakuwa umeliona gauni alilovaa mwigizaji Elizabeth Michael maarufu Lulu jana Jumanne Februari 16, 2021 wakati akifunga ndoa na mkurugenzi wa televisheni ya TVE na redio EFM, Francis Ciza.

Gauni hilo lililotengenezwa na mbunifu, Valdrin Sahiti huuzwa kuanzia Dola12,000 za Marekani (Sh25 milioni), fedha ambayo unaweza kuitumia kununua magari mawili aina ya Toyota IST kwa kuwa moja huuzwa kati ya Sh10 milioni hadi Sh13 milioni.

Katika mtandao wa kuuza na kukodisha magauni ya harusi wa Borrowing Magnolia, magauni ya Sahiti yanauza kiasi hicho cha fedha.

Ndoa ya wawili hao waliodumu kwenye uchumba kwa takribani miaka miwili ilifungwa katika kanisa la St Gasper lililopo Mbezi  Beach jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Februari 17, 2021 Kenneth Francis  ambaye ni mbunifu wa mavazi aliyeliweka sawa gauni la Lulu lililotumwa nchini na Sahiti anayeishi nchini Cosovo, “mimi nililifanyia marekebisho madogo ili limkae vyema bibi harusi.

“Kulikuwa na magauni mawili moja alilivaa wakati akipambwa na jingine akiwa kanisani. Mimi nilitengeneza hilo la kwanza ila lile la pili (lililotoka kwa Sahiti) ndio nililiweka sawa ili limkae vizuri Lulu. Hilo gauni jina lake maarufu ni Cinderella.”

Advertisement

Mastaa wengine waliowahi kuvalishwa na mbunifu huyo ni mwanamuziki wa Marekani, Beyonce na rapa Cardi B.

Naye  Magreth Shirima aliyeshughulika na uwekaji wa maua katika sherehe ya harusi hiyo amesema ua aliloshika Lulu gharama yake ni Sh300,000.

“Ule ni mchanganyiko wa maua zaidi ya sita na nilifanya hivyo kwa maelekezo ya Lulu aliyetaka yawe maua  yenye kuashiria ndoa hiyo itakuwa na mwisho mwema,“ amesema Magreth, ambaye ni   mmiliki  wa kampuni ya  Meggy Flower.

Clemence  Eliah kutoka kampuni ya upigaji picha ya CP studio, amesema kazi yake siku hiyo ilikuwa nyepesi tofauti na umaarufu  wa Lulu kwa sababu hakukuwa na watu wengi.

“Nimewahi kufanya kazi ya kupiga picha harusi za mastaa wengi, mara nyingi huwa na purukushani, lakini hii ilikuwa rahisi kwa sababu watu walikuwa wachache, ilikuwa rahisi kupata picha yoyote uitakayo,” amesema.

Advertisement