Udhamini watishia uhai wa tamasha la Sauti za Busara

Monday September 05 2022
sauti pic

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Blue Amber Zanzibar, Grant Anderson akibadilishana nyaraka za udhamini na Mkurugenzi wa Sauti za Busara festival, Yusuf Mahmoud (kulia) mwishoni mwa Machi visiwani Zanzibar. Picha ya Maktaba

By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Uwezekano wa tamasha la Sauti za Busara kufanyika kwa awamu ya 20 upo njiapanda kutokana na kusitishwa kwa mkataba wa ufadhili na wadhamini.

Tamasha hilo lenye hadhi ya kimataifa linalofanyika kila mwaka katika ukumbi wa Ngome Kongwe, Mji Mkongwe visiwani Zanzibar linaaminika kuwa miongoni mwa matamasha 10 bora barani Afrika, likivileta pamoja zaidi ya vikundi 40 na wageni kutoka mataifa tofauti duniani.

Taarifa iliyotolewa juzi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Busara Promotions, Yusuf Mahmoud ilisema maandalizi ya tamasha la mwaka 2023 yamepata pigo baada ya wadhamini, Blue Amber kusitisha mkataba waliousaini Machi 2022.

“Agosti 30, Busara Promotions ilipokea taarifa rasmi kwamba udhamini wake na Blue Amber ulikuwa umesitishwa mara moja. Kwa mara nyingine tena, mustakabali wetu haujulikani kwa sababu hakuna fedha za kuendesha ofisi zaidi ya Septemba,” alisema Mahmoud.

Kwa mujibu wa maelezo yake, wafadhili wao, Pennyroyal, watengenezaji wa Blue Amber walifikia uamuzi huo ambao haukutarajiwa baada ya ardhi waliyoikodi kwa miaka 99 kusitishwa na Wizara ya Ardhi, hivyo kufutiliwa kibali cha ujenzi.

Tamasha hilo, hata hivyo, limeahidi kuwa wote walionunua tiketi mapema watafidiwa baada ya mkutano wa bodi utakaofanyika Septemba 15.

Advertisement

Huku ikiwa ni takriban miongo miwili ya burudani, kwa kawaida idadi ya watalii wanaokuja Zanzibar huongezeka kwa kiasi kikubwa kila Februari, huku vyombo vya habari vya kimataifa navyo vikiitaja Sauti za Busara kama moja ya matukio 10 bora.

Ripoti inaonyesha hata mwaka 2020, watalii walioenda Zanzibar, Februari waliongezeka kwa asilimia 0.5 na kufika 61,752 ambapo Februari 2021 walikuwa 51,574 ikilinganishwa na 49,868 Januari mwaka huohuo.

Hii ilikuwa kinyume kabisa na mwenendo wa kimataifa ambapo nchi nyingi zilikuwa zimefunga anga zao na nyingine zilikuwa bado zimefunga mipaka yake.

Kwa mujibu wa Mahmoud, mapato ya tamasha la Sauti za Busara kutokana na mauzo ya tiketi huwa chini ya asilimia 30 ya gharama zote ambazo ni mamia ya maelfu ya dola za Marekani.

“Pengine ingeingia mara mbili zaidi kama ingelingana na madhumuni ya kibiashara,” alisema Mahmoud.

Jitihada za kuwatafuta Blue Amber ili kupata maoni yao hazikuzaa matunda jana, kwani simu za watendaji wake hazikupokelewa wala ujumbe mfupi wa maneno haukujibiwa.

Habari ambazo hazijathibitishwa zinadai kuwa kampuni ya Blue Amber imesitisha udhamini wa tamasha hilo kutokana na mradi wao wa maendeleo kusitishwa na Serikali katika mgogoro wa ardhi unaoelekea kutikisa soko la majengo ya kupangisha visiwani Zanzibar.

Mwaka 2017, eneo hilo lenye mgogoro lilitakiwa kujengwa mradi mkubwa ambao ungekuwa na uwanja wa gofu mkubwa zaidi kwa Afrika Mashariki na hoteli tano za kifahari, ulishindikana kutokana na kutoelewana kati ya Serikali na mwekezaji aliyekuwapo.

Mradi huo pia ulitarajiwa kujengwa hoteli ya chini ya maji, klabu ya usiku, kituo cha farasi na kituo cha boti za starehe (yacht).

Tangazo hilo, ambalo bado halijathibitishwa kwamba ukodishaji wake umekatishwa bila shaka litaleta mshtuko kote Afrika Mashariki na kwingineko duniani.

Ingawa hii inashangaza, uchunguzi wa hivi karibuni wa Mwananchi juu ya uendelezaji na uwekezaji katika eneo hilo umebaini sekta ya majengo Zanzibar inakabiliwa na changamoto ya ushawishi mdogo.

Kama kivutio kikuu barani Afrika, Zanzibar inafukuzana na wenzake kama vile Dubai, Shelisheli na Mauritius kuvutia uwekezaji wa majengo.

Miundombinu iliyokamilika na mingine ambayo bado haijakamilika ni pumzi ya hewa safi katika kisiwa kinachojulikana kama Kisiwa cha Marashi.

Utafiti wa gazeti hili uliofanywa hivi karibuni unaonyesha baadhi ya waendelezaji wa majengo katika visiwa hivyo wamekwama na majengo ambayo ujenzi wake ulimalizika miaka kadhaa iliyopita na baadhi ya wanunuzi hawawezi kupata motisha ambayo iliwekwa kama masharti na mamlaka za usimamizi.

Advertisement