UPO NYONYO... HII NCHI UHURU UMEPITILIZA SANA!

Sunday July 24 2022
nyonyopic
By Dk Levy

Ananiuliza kama nina demu, namwambia sina! Anahisi alishawahi kuniona sehemu, tatizo kanisahau jina. Unaitwa nani? Fid Q! Unaishi wapi? Ghetto! Kazi yako nini? Muziki! (Au sio). Hili pini la mapenzi lakini limeanza kibabe sana, kama movi la ‘Saibogi’.

Mdomo unakuwa mzito, niongee kipi cha maana. Kivipi nimkazie jicho, wakati binti kasimama. Au nijikombee maujiko, Fid sitaki kujuana. Bange usinizingue kihivyo, mimi simuachi huyu kimwana. Fid Q kadata na totozi mpaka anaikoromea bange yenyewe.

Anaonyesha hana maringo lakini ashawahi kupima. Ashazimika kimtindo, mchizi kipingamizi sina. Yupo shkopa, yupo shalo tina tina, yupo full, Oi! Kama wasemavyo watu wazima. Yes! Heshimu pisi ambayo imepima iko poa na wala hairingi. ‘Ndo waifu matirio’ hiyo.

Sasa nami naanza kutoa onyo langu kibabe. Kwa wanaotaka sifa kibwege tu kwa wake zetu. Wakijifanya wao ndio wanajua mapenzi au kufundisha ‘ishu’ za ndoa na kulea. Tunawasihi waache fasta kutafuta sifa za kijinga kupitia shida zetu. Tunamaanisha!

Kwa niaba ya walalahoi, wasotaji, wabangaizaji na wazee wa kusikilizia michongo. Na kwa wote wanaopata pesa za kula kwa jasho na tabu sana. Tunaoishi ‘laifu’ la nguvu za macho, tukiondoka ‘homu’ bila kitu na kurudi ‘homu’ bila kitu. Nasema hivi, sisi ndio sisi!

Tunataka hao washauri wa ndoa za watu, wachunge midomo na vidole vyao. Wengine hutumia nyumba za ibada kuhubiri makosa na shida zetu tu. Wakiwatia ndimu na chumvi wake zetu, kuwa hatujali wala kuziheshimu ndoa. Hao pia nawaonya kwa karipio kali.

Advertisement

Mtu unajiuliza huyu kaolewa na mchungaji au na mimi? Hata maandiko hayasemi hivyo. Wapo wanaolala zaidi ya wiki kwenye maombezi, hawajui cha mume wala watoto. Jamani msiwafanye waume zenu wasake ‘vismolo hausi’, kwa kutotekeleza majukumu yenu. Vitabu vinasema, mke atavunja ndoa kwa mikono yake mwenyewe. Upo titi?

Na vitabu vya wachungaji hao hao. Husema, watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa. Ndio maana yake! Unakesha kwenye maombi na kusahau familia. Hapo unafukuza au unakaribisha hilo pepo? Tuwe ‘siriazi’ kidogo.

Yaani imefika wakati washua hupata ahueni kwa mahaba ya ‘baba shopu’ na ‘masaji hausi’. Ndiyo! Baadhi ya nyumba za ‘masaji’ ukiingia tu kuna mambo ya giza haswa. Yale ambayo ‘mawaifu’ hawawezi siyo tu kutenda, hata kuyawaza.

Mtazame mtoto wa leo, kisha jiulize miaka ijayo tutakuwa na vijana wa aina gani? Mtazame kijana wa leo, kisha jiulize kesho tutakuwa na vizee wa aina gani? Kuna kizazi cha ovyo ovyo kinakuja.

Kinachokera ni vijana hawa wa kiume kujiremba kama mama zao. Na wale wa kike kutenda na kuishi kama baba zao. Ifike wakati tuache kuigaiga hizi mambo za wazungu wa Ulaya huko. Tunakopi kila kitu kwao nasi tunapita mulemule. Wakati tuna utajiri wa vitu ambavyo havifanani na vyao kabisa. Na ukitaka dunia iwe salama zaidi, nasi tutumie akili zetu kama wazungu. Yes!

Ili wakija washangae tunafanya kile wasichokiweza. Mtu ana usafiri wake wa kufika fasta popote bila kutumia mafuta usiku. Ajabu tunapiga kelele za “Pepo tokaa, shindwa na ulegee.” Wakati kupaa na ungo ni sayansi ya pekee. Ila sisi tunaita ushetani.

Kila kitu chao tutaona ni bora sana kuliko chetu. Tukoje?

Ukiongea Kiingereza unaonekana wa maana kuliko Kinyalukolo. Hili kosa hata Mungu atatuhukumu sana kwa undezi wetu. Alipotutenganisha kwa rangi, nywele na macho alikuwa na maana, kama angetaka tufanane asingeshindwa.

Bongo hii kuna joto mzungu kazoea baridi ni rahisi kuvaa kimini mchana. Sasa wewe dada wa Mufindi huko unaiga mzungu kuvaa kimini cha nini?

Hii nchi uhuru umezidi toka enzi na enzi. Yaani kuna ndezi tu aliamua chumba cha ‘gesti’ mwisho saa nne asubuhi. Baadaye mazuzu ya hoteli yakaiga kwa watu wa ‘gesti hausi’. Na Wabongo kwa unyonge wao wa kiboya, wanatii bila shuruti.

Sasa leo natoa tamko rasmi kama mkuu wa matamko Tanzania nzima. Na kama mbia mkuu wa watumiaji wazoefu wa ‘gesti’ nchini. Kwamba tunakerwa kugongewa milango saa nne, na tunatangaza rasmi ni wizi kama wizi mwingine.

Mtu mwenyewe gia za ‘fiati’, ‘steringi’ ya ‘bedifodi’. Usiku kucha unapanda mlima bila mafanikio. ‘Fiati’ linaanza kuchanganya na ‘hangover’ zako ile asubuhi. Eti unasikia sauti ya kadada kanagonga na kuuliza, ‘unaendelea?’ Nyambafu!

Kifupi gesti ni saa 24, ukiingia saa 10 alfajiri utatoka saa 10 alfajiri. Upuuzi wa kuamshana saa 4 ni Bongo tu na vile wanyonge tunakubali. Nenda Kenya au Uganda hapo, ukiingia saa 6 usiku utatoka saa 6 usiku. Ndio manaake!

Bongo unatoka klabu saa 10 alfajiri unaingia gesti, saa tatu unagongewa. Kuna siku wahudumu watakutana na kitu kizito, ndio watajua sheria halisi zinasemaje. Narudia, ‘gesti’ kwa siku kulala ni saa 24 kamili na si vinginevyo. Uhuru usivuke mipaka.

Haya yote wazungu walitakiwa waje kuiga. Mfano matrafiki wa Mwenge wana roho mtakatifu wao. Kwanza hujazana kwa wingi kuliko daladala. Roho mtakatifu wao kawapa ufunuo wa kujua jina la dereva na konda, kuliko namba za gari.

Daladala ikisimamishwa anashuka konda, gari inapaki mbali. Baada ya dakika moja utaona konda anarudi na kuruhusu gari iendelee na safari. Roho mtakatifu wa matrafiki kawapa uwezo wa kuona kosa la gari kupitia mwili, uso, na sauti ya kondakta tu.

Wakiitazama sura ya konda na zile sare zao. Wanajua gari ina vibali, ina taa, breki, bima na shokapu imara. Ndio maana hawana muda mchafu wa kukagua zaidi ya kuongea na konda. Tena roho mtakatifu wao alielekeza wakamate daladala tu. Upo nyonyo!

Tena wana muda wa kuwepo eneo la kazi ni alfajiri na kuondoka saa nne asubuhi, siyo zaidi ya hapo. Bila shaka roho mtakatifu anakuwa kawaelekeza wakanywe supu haraka. Jambo hili ni la kipekee sana, inafaa wazungu waje kuiga. Tuna vitu vingi mno ambavyo hupati popote. Mfano, kitabu cha Kiswahili utasoma siku moja unamaliza. Cha Kiingereza utatumia wiki na zaidi na usimalize wala kuelewa. Kiingereza huumiza kichwa na akili kwa pamoja na kuleta kigugumizi.

Hata totozi ikiwa na viingereza vingi masela hupunguza kujiamini. Lakini tumeamua kutumia Kiingereza hicho kigumu, kama lugha ya kuelimishia watoto wetu mashuleni. Hata wanaokomaa hufeli kama siyo kukariri bila kuelimika. Utamaduni wa lugha ngeni kuelimishia watoto wetu. Haupo popote zaidi ya hapa kwetu kivyetu vyetu. Wazungu waje kuiga hili.

Hatutumii Kiswahili kujifunzia ngazi zote za elimu. Na tukijimwambafai kwamba Kiswahili ni lugha yetu ya Taifa. Nenda ofisi za umma, asilimia kubwa zina majina ya ngeri tu. Hata kwenye ajira usaili wake ni kwa ngeri tu. Nchi ya ‘kiswanglishi’. Taasisi nyingi ukisikia zinatamkwa kwa kifu, ujue kirefu cha ni Kiingereza.Hata serikalini wanapeana vyeo kwa swaga za ung’eng’e tupu mwanzo mwisho.

Sasa unashangaa ya Malkia Karen, kuzaa bila ‘kolabo’ ya msela? Siku hizi kama kuku za kisasa, unauziwa mbegu za kiume kama mbaazi au uwele. Unawekewa kama ‘waini’ kwa glasi na unatotoleshwa mtoto. Utajua mwenyewe!

Kama jamii tungedumisha vitu vyetu. Tingevikweza na kuvihusudu saana. Tusingeona kina Karen wakiiga vitu. Wangekomaa kama bibi na babu zao walivyoishi. Tatizo siyo raia tu, hata viongozi, taasisi za Serikali na wote tunaiga wenzetu. Sasa unategemea nini?

Ukimuuliza Karen sababu ya mtoto bila baba. Anakuambia hajaona wa kumzalia hii Bongo. Hii nchi uhuru umepitiliza sana... upo nyonyo!

Advertisement