Utamaduni wa Afrika Mashariki kuoneshwa Serengeti

Muktasari:
- Sasa tamaduni za Afrika Mashariki kukutanishwa jukwaa moja la Serengeti Oktoba Fest katika fukwe za Coco beach.
Dar es Salaam. Utamaduni wa Afrika Mashariki utaonyeshwa siku ya Serengeti Oktoba Fest itakayofanyika Oktoba 21,2023.
Akitambulisha baadhi ya mambo yatakayokuwepo siku hiyo Mkurugenzi wa Masoko na Ubunifu wa Serengeti Breweries Anitha Msangi amesema siku hiyo kutakuwa na matukio tofauti ambayo yatakwenda kutambulisha Uafrika Mashariki.
"Hiyo siku tutaonyesha vitu tofauti ambavyo havijawahi kufanywa katika matamasha yote yaliyofanyika ndani na nje ya Tanzania kwani tunakwenda kuhamasisha utamaduni wetu,"amesema Anita.
Pia Anita amesema kutakuwa na burudani za nchi za Afrika Mashariki kwani tukio hilo ufunguzi wake utafanyika Tanzania na kuzunguka katika nchi nyingine ambazo ni Kenya,Uganda na Sudan Kusini.
Amesema kikubwa kitakachofanyika kwa Tanzania ni kuonyesha vyakula,matumizi ya usafiri wa bajaj kwa wale wote watakaopenda kutumia, kucheza michezo mbalimbali ikiwemo rede na kuonyesha mavazi.
Mbali na hilo pia amesema kwa kuwa tanasha hilo litafanyika kwenye fukwe za bahari wamekuja na vikombe vya bati vitakavyotumika kutia vinywaji ili kusaidia utunzaji wa mazingira ambayo yatasababishwa na matumizi ya vitu vya plastiki.
"Tunataka kuwafundisha wengine ni namna gani tunaweza kutumia matamasha haya kuhamasisha mambo mbalimbali kwa jamii wengi wanajua kuwa ni kunywa na kucheza muziki lakini sisi tumekuja kivingine,"amesema.
Anita amesema tamasha hilo linatarajia kuwapatia ajira watu zaidi ya 500 katika fani tofauti ambayo yanawapa vijana fursa za kujiajiri ikiwepo mitindo ya mavazi na mapishi ya kitamaduni.
Kwa Upande wake Meneja wa Chapa za Serengeti Ester Raphael amesema ubunifu wa kitamaduni utakwenda kuwavutia watu kwani wamejipanga kwa ajili ya kuonyesha vivutio vya kitamaduni.
"Mwaka jana tulizunguka Tanzania nzima kuonyesha vipawa vya Watanzania hususani kwenye muziki safari hii tumekuja na mtazamo mwengine,"amesema Ester.