Utamu wa saa 2:30 za Rais Samia, Sugu

Friday June 03 2022
utamupiic

Dar es Salaam. “Haijawahi kutokea!” Ilikuwa moja ya kauli za wageni mbalimbali walioungana na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye The Dream Concert, tamasha maalumu la mwanamuziki Joseph ‘Sugu’ Mbilinyi, aliyeadhimisha miaka 30 ya muziki juzi usiku.

Tamasha hilo ambalo Rais Samia alikuwa mgeni rasmi, pia limewaunganisha viongozi vyama vya siasa, akiwemo Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Abdulrahman Kinana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, mabalozi, wakuu wa taasisi mbalimbali pamoja na wasanii wa Bongo Flava, wakiwa meza moja kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.

Rais Samia katika hotuba yake alimtaja Sugu ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini kupitia Chadema kuwa “ni mtu na yuko tofauti”, akimuelezea kuwa ni mwenye nidhamu na mpambanaji aliyepitia changamoto hadi kutimiza ndoto zake.

“Safari ya Joseph haikuwa rahisi, mimi nitamuita Joseph japo ana majina mengi kama Taita, Mr II na Sugu ingawa sasa amenyooka, lakini mimi kama mama na huyu ni mwanangu nitamuita Joseph,” alisema Rais Samia.

Alisema wengi huwa hawapendi kuweka historia ya maisha yao, hasa zile zenye mwanzo mbaya, lakini amevutiwa na wazo la Sugu kuweka histori yake kitabuni. Kitabu hicho kinakwenda kwa jina la Maisha na Muziki.

“Nakumbuka siku Joseph ‘Sugu’ alipomuudhi Spika akaamuru atolewe nje (wakati huo alikuwa mbunge wa Mbeya Mjini), alivyokuwa ameshikwa mkono na mguu, lile tukio huwa nalikumbuka, lakini huyu ni mpambanaji,” alisema Samia huku akitabasamu.

Advertisement

Ukumbini mambo yalikuwa hivi

Rais Samia aliwasili ukumbini saa 1:14 na kupiga picha na familia ya Sugu, mkewe na watoto kisha wasanii ambao walijitokeza kumsapoti Taita kabla ya kuingia ndani ya ukumbi dakika tatu baadaye.

Saa 1:45 Sugu alipanda jukwaani na jambo la kwanza alilomweleza Rais Samia ni kwamba, yeye na wenzake wametengeneza historia baada ya safari ndefu na mapambano ambayo yalihitaji nidhamu, subira, uvumilivu na kuamua kuishi katika ndoto.

“Pamoja na yote, ila sija ‘lost’ mimi bado Taita, hivyo nikiona vijana wanapiga hela kwenye muziki sina chuki. Utaona leo vijana (wasanii) wanakodi ndege kwenda kupiga shoo Afrika Kusini, wakati ule mimi nilitembea kwa miguu kwenda studio,” alisema Sugu huku mamia ya mashabiki na Rais Samia wakiangua kicheko.

Alisema wengi wa waasisi wa muziki wa Hip Hop hawajafaidika, lakini aliwafananisha na wakandarasi ambao wanajenga barabara lakini wanaweza wasipite kwenye barabara hizo, hivyo ndivyo imekuwa kwa waasisi wa muziki ambao baadhi wameshatangulia mbele za haki.

Picha za wasanii hao zilionyeshwa kwenye runinga kubwa ukumbini hapo sambamba na kumpigia Joseph Haule (Profesa J) makofi ya uponyaji wakati huu anapokabiliana na maradhi hospitalini.

Saa 1:52 usiku, Sugu alimaliza hotuba yake na kutoa burudani akianza na wimbo wake wa kwanza ukiwa wa ‘Ana miaka chini ya 18’ ambao alisema aliutunga baada ya kukutana na binti aliyekuwa akifanya biashara za usiku aliyekuwa na miaka 17 na historia yake ilikuwa inasikitisha.

Muda wote wakati Sugu akiimba Rais Samia alikuwa akitabasamu kwenye kiti chake na alifanya hivyo hata pale Sugu alipowaita jukwaani kundi la Weusi, Nikki wa II, Lord Eyez, G-nako na Joh Makini, AY, Mwana FA na Jide ambao waliimba wimbo wa pamoja wa Kilimanjaro.

“Rais amenipa heshima, leo hii familia yangu imekaa jirani na meza ya Rais, hii ni historia kubwa kwangu lakini pia ameupa heshima muziki wetu kwa kukubali kuungana nasi hapa,” alisema Sugu kwa hisia na utulivu wa hali ya juu.

Rais Samia apanda jukwaani

Saa 2:40 usiku, Rais alipanda jukwaani na kuitaja siku hiyo ni maalumu na anaungana na Sugu katika safari ya miaka 30 ya muziki.

“Nimewaona wabunge (Mwana FA) na wakuu wa wilaya (Nikki wa II), nikajiuliza wanafanya kazi saa ngapi? Lakini najua wanajigawa kwenye muziki na majukumu mengine, hivyo siwavunji moyo waendelee tu,” alisema Rais Samia aliyetoa hotuba yake hadi saa 3:07 usiku alipozindua kitabu cha Maisha na Muziki cha Sugu.

Baada ya uzinduzi huo, Rais Samia alirejea kwenye meza yake, lakini wimbo maalumu wa Mama Kiongozi Simama ulioimbwa na Lady JayDee ulimnyanyua kwenye kiti kwa sekunde chache na kucheza kidogo kabla ya kuondoka kuendelea na majukumu mengine na kuwaacha wengine wakiendelea na burudani.

Wanasiasa meza moja

Tamasha hilo liliwakutanisha wengi, wakiwemo wanasiasa ambao baadhi yao walikaa meza moja na kufurahi.

Kinana na Mbowe usiku huo walikaa meza moja wakifurahi kila mmoja akitabasamu kwa wakati wake kabla ya Rais Samia kumuita Mbowe na wengine jukwaani ili kushiriki kwenye uzinduzi wa kitabu cha Sugu.

Mbali na wanasiasa hao, pia Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mohammed Mchengerwa, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye nao walikuwepo.

Wengine ni aliyekuwa mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika.

Advertisement