Verckys, mwamba wa muziki wa Congo

Muktasari:

Georges Kiamuangana Mateta, maarufu kwa jina la Verckys alizaliwa Kisantu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Mei 19,1944.

Georges Kiamuangana Mateta, maarufu kwa jina la Verckys alizaliwa Kisantu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Mei 19,1944.

Alijipa jina la Verckys kimakosa kwani alitaka kujiita jina la mpiga saksafon maarufu wa Marekani wakati ule aliyeitwa King Curtis. Kwa bahati mbaya alisikia jina “Curtis” kama “Verckys.” Na wote mpaka leo tunamfahamu kama Verckys.

Baba yake Verckys alikuwa mfanyabiashara tajiri, hivyo Verckys alipata elimu nzuri kabisa. Mapema kabisa alionyesha umahiri wa kipaji chake cha muziki kwani alikuwa akifahamu kupiga vyombo kadhaa vya kupuliza kama vile filimbi na clarinet, hatimaye alianza kujifunza saksafon alipokuwa kwenye kikundi cha madhehebu yaliyokuwa chini ya mchungaji maarufu wa Kikongo aliyeitwa Nabii Simon Kimbangu.

Mwaka 1962 alijiunga na bendi iliyoitwa Los Cantina, baadaye akahamia Jamel Jazz na mwaka huo huo safari yake ikamfikisha kwenye kundi la Conga Jazz lililokuwa chini ya mkongwe mwingine maarufu katika muziki wa Congo aliyeitwa Paul Ebengo, maarufu zaidi kwa jina la Dewayon.

Mwaka 1963 akahamia TP O.K. Jazz in 1963, kundi lililokuja kumtambulisha rasmi katika ulimwengu wa muziki. Alikuwa mpuliza saksafon mzuri sana kiasi cha kupewa sifa ya kuwa ‘Mtu mwenye mapafu ya chuma’, akawa mtu wa karibu sana na Luambo Luanzo Franco kiongozi wa TP OK Jazz.

Mwaka 1968, Franco akapata ziara ya kwenda Ulaya, akachukua baadhi ya wanamuziki na kwenda nao, huku nyuma Verckys na mwimbaji Youlou Mabiala wakakusanya wenzao na kufanya mazoezi ya haraka na kuingia studio na kurekodi nyimbo nne. Kasheshe kubwa lilizuka baada ya Franco kurudi kutoka ziara yake na hatimaye Aprili 5, 1969, Verckys alilazimika kuacha TP OK Jazz na kuanzisha kundi lake mwenyewe aliloliita Orchestre Veve.

Kundi hili lilikuwa na waimbaji vijana machachari wakiwamo Matadidi Mabele, maarufu Mario, Marcel Loko, maarufu Djeskain, na Bonghat “Sinatra” Tshekabu, maarufu kwa Saak Saakul. Vijana hawa baadaye walikuja kumkimbia Verckys na kuanzisha kundi lao lililokuja kutikisa mpaka bendi kongwe za wakati huo, kundi hili liliitwa Orchestra Sosoliso na umoja wao walijipa jina la Trio Madjesi .

Turudi kwa Verckys, yeye na kundi lake la Orchestre Veve lilikuja kurekodi nyimbo nyingi maarufu kama ‘Mfumbwa’, ‘Bankonko Baboyi’ na uliotungwa na Saak Saakul ulioitwa ‘Fifi Solange’. Mafanikio makubwa aliyokuja kuyapata Verckys yalimuwezesha kuingia rasmi katika biashara ya muziki kwa kuanzisha lebo yake na kuingia mikataba na bendi mbalimbali maarufu wakati ule. Baadhi ya bendi zilizotoa nyimbo kwa lebo hiyo na kutikiza Afrika nzima zilikuwa, Les Grand maquisards, Orchestra Kiam ambayo jina lake Kiam lilikuwa ni ufupisho wa jina Verckys la Kiamuangana, Orchestra Bella Bella ya wale ndugu wawili waimbaji, Soki Vangu na Soki Dianzenza, Orchestra Lipua lipua, Les Kamale, na Empire Bakuba ya Pepe Kalle.

Mwaka 1972 Verckys alifungua studio yake katika kituo alichokiita Veve Center. Alianza kufanya mambo mengi makubwa katika muziki, hili liliwezesha mwaka 1978 achaguliwe kuwa rais wa wanamuziki wa Zaire, baada ya Franco Makiadi kumaliza muda wake.

Historia ya Verckys kwa kifupi imejaa mafanikio makubwa kimuziki. Akiwa na miaka 18 alijiunga na kundi kongwe la TP OK Jazz, alipofikia umri wa miaka 25 alifungua studio yake ya kurekodi muziki. Mwaka 1972 alimshirikisha

Pepe Kalle kuimba kwenye nyimbo kali kama ‘Sola’, ‘Mbuta’ wakishirikiana na Bella Bella, na kumshirikisha na Nyboma Mwandido kwenye wimbo ‘Kamale’ uliopigwa na Orchestra Lipua Lipua .Verckys ndiye chanzo cha Orchestres Baya Baya, Lipua Lipua na Kiam, matokeo yake ni nyimbo tamu maarufu kama ‘Amba’, ‘Mombasa’, ‘Niki bue’, ‘Mbale’, ‘Kamiki’, ‘Bomoto’ na nyingine nyingi sana. Huwezi kumuweka pembeni Verckys utakapotaja mafanikio ya mtindo wa Cavasha ulioishika Afrika nzima miaka ya sabini.

Mwaka 1976 Verckys alibadili jina la lebo yake kutoka Editions Veve kuwa Zadis, ambayo ilikuwa kifupi cha Zaire disc. Kwa lebo hii mpya Orchestra Veve ikatoa nyimbo mbili zilizogusa nyoyo za wapenzi wa muziki wake mpaka leo, zikiwamo ‘Papy Baluti’ na ‘Muana Mburu’. Wakati huo Orchestra Veve ilikuwa na wanamuziki wafuatao; Tino Muinkwa, Djo Roy, Nejos Tusevo, Pepitho Fukiau kwenye uimbaji, Lambion akiwa anapiga gitaa la solo, Aladji Baba kwenye gitaa la rhythm, Ndolo na Celi Bitsou wakiwa wapiga bezi. Kwenye drums alikuweko Bayard, Ponta Vickys kwenye congas, yeye mwenyewe Verckys, Dibuidi na Sax Matalanza wakipuliza Saksafon, Makamba akiwa anapuliza trombone. Ni kiasi cha kusikiliza nyimbo hizo mbili ujue umahiri wa wanamuziki waliotajwa.

Mwaka1978 alimrekodi kijana mdogo aliyeitwa Koffi Olomide, hadithi ya Koffi kwa sasa kila mtu anaijua.