VIDEO: Kizimkazi yakumbusha viongozi kuenzi utamaduni

Kizimkazi yakumbusha viongozi kuenzi utamaduni

Muktasari:

Viongozi mbalimbali waliohudhuria katika tamasha la Kizimkazi linalohitimishwa leo katika wilaya ya Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar wametaja umuhimu wa matamasha ya kuenzi utamaduni wakisema ndiyo njia pekee ya kurithisha tamaduni kwa vizazi vya leo.

Dar es Salaam. Viongozi mbalimbali wamesema Tamasha la Kizimkazi limewakumbusha umuhimu wa jamii husika kuenzi utamaduni na kwamba ndiyo nguzo muhimu ya kurithisha vizazi.

Hayo yamesemwa na viongozi mbalimbali wakiwamo Wakuu wa Mikoa leo Jumamosi, Septemba 3, 2022 waliposhiriki kilele cha maadhimisho ya siku ya Kizimkazi yanayofanyika katika wilaya ya Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar, yenye kaulimbiu isemayo ‘Royal Tour na Uchumi wa Buluu ni chachu ya maendeleo’.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Hadid Rashid amesema eneo hilo ndilo alikozaliwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na tamasha hilo limekuwepo kuenzi tamaduni za jamii hiyo.

“Tangu tumeanza tamasha hili tumefanikiwa kuutangaza mkoa kiutalii, tumejenga miundombinu mingi, maji katika miji ya Kizimkazi na miradi mbalimbali ambayo Rais Samia uliizindua jana,” amesema Rashid.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amesema kupitia tamasha hilo viongozi wanajifunza namna ambavyo Rais Samia anakaa na wananchi wa jamii yake bila kujali itikadi wala rika lao, “Kwa sisi viongozi wadogo tunapaswa kujifunza namna ya kuenzi utamaduni wetu asilia.”

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema tamasha hilo limekuwa ni funzo kwa viongozi wengine kuenzi tamaduni za jamii zao.

“Limekuwa kama funzo kwetu tumejifunza mambo mengi namna unavyoishi na jamii yako, tumeshuhudia watoto kwa wakubwa na wazee wote wakishuhudia tukio hili, kama wasaidizi wako hili ni funzo na sisi katika mikoa yetu tutahamasishana kuona namna ya kuendelea kufanya matamasha ya utamaduni katika maeneo yetu ili kufunza vizazi vyetu,” amesema.

Katibu wa kamati ya maandalizi ya tamasha la Kizimkazi, Hamlid Abdul Hamlid amesema Kizimkazi imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kimaendeleo iliyochangiwa na Uchumi wa Bluu.

“Tumefanikiwa kukamilisha miundombinu ikiwemo ujenzi wa maabara shule ya Kizimkazi, wajasiriamali kupatiwa mikopo nafuu kutoka CRDB, maji safi na salama kwa kasi ya usambazaji mabomba, kukamilika kwa ujenzi wa sekondari, tumejipangia malengo yafuatayo kutatua changamoto zinazotukabili kiuchumi, maendeleo na kijamii,” amesema Hamlid.