Waimbaji 2, 000 kufundwa tamasha la uimbaji

Muktasari:

  • Tamasha la uimbaji wa nyimbo za injili limewakutanisha waimbaji 2,000 kutoka Uganda, Kenya na Tanzania jijini Dodoma.

Dodoma. Zaidi ya waimbaji 2,000 wa kanisa la Anglikana kutoka nchi za Tanzania, Kenya na Uganda wamekutana jijini Dodoma kwa ajili ya tamasha kubwa la uimbaji lenye lengo la kuwafundisha waimbaji hao namna ya kuimba kwa ufasaha nyimbo za Zaburi.

Tamasha hilo ambalo ni la tisa tangu kuanzishwa kwake litajumuisha kwaya

40 ambapo kwaya itakayofanya vizuri itaondoka na tuzo.

Akizungumza wakati wa kufungua tamasha hilo leo Alhamisi Oktoba 26, 2023 Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT), Dk Dickson Chilongani amesema tamasha hilo ni chachu ya kujifunza namna bora ya kumwimbia Mungu kwa kutumia kitabu cha Zaburi.

Dk Chilongani amesema hivi sasa kumekuwa na uimbaji ambao haufuati utaratibu unaotakiwa na ndiyo maana wameianzisha tamasha hilo kwa ajili ya kuwafundisha watu namna ya kuimba ili na wao wakawafundishe watu wengine.

"Siku hizi watu hawaimbi kwa utaratibu unaotakiwa wanaimba tofauti kabisa, tamasha hili litawasaidia wanakwaya hawa kujua jinsi ya kuimba na wao wakijua watawafundisha wengine na mwisho wa siku tutaimba wote kwa sauti moja na ndiyo lengo la tamasha hili," amesema Askofu Chilongani.

Amesema uimbaji wa kwenye tamasha hilo utatumia noten na solfa ambazo ni njia ngumu za uimbaji ambao unatakiwa kufuata mpangilio uliowekwa kwa ajili ya kuimba wimbo husika hasa za kitabu cha Zaburi na nyimbo za kwenye vitabu.

Amesema kwa siku za hivi karibuni watu wengi hawajui kuimba nyimbo za Zaburi na za kwenye vitabu hivyo kanisa limeona lilete tamasha hilo ili kuwakumbusha waumini njia bora ya kumwimbia Mungu kwa kiwango kinachotakiwa.

Askofu huyo amesema waimbaji hao wametoka kwenye makanisa makuu ya Anglikana (Cathedral) kwenye nchi walizotoka ili kumsifu Mungu inavyotakiwa.

Mratibu wa tamasha hilo kutoka nchini Kenya, Daniel Madalanga amesema tamasha hilo la siku tatu lina lengo la kuinua kiwango cha uimbaji kwenye makanisa ya Anglikana ukanda wa Afrika Mashariki.

Amesema waumini wengi hawajui kuimba na huwa wanawaachia wanakwaya peke yake lakini wakifundishwa wote wataimba kwa sauti moja kwa ajili ya kumsifu Mungu.

Mshiriki wa tamasha hilo Catherine Akechi amesema tamasha hilo ni la muhimu kwa kanisa la Anglikana ambalo kwa sasa linataka kuinua viwango vya waimbaji wake pamoja na kuimarisha umoja wao katika nchi za Afrika Mashariki.

Amesema tamasha hilo litawawezesha waumini wa kanisa la Anglikana katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda kuimba kwa ufasaha nyimbo za Zaburi na za kwenye vitabu.