Wakali hawa na mabinti damdamu

Monday April 05 2021
WAKALIII PIC
By Kelvin Kagambo

MWAKA 2002 rapa mwenye asili ya jiji la mapenzi Tanga, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ aliachia ngoma ya kuitwa Mabinti.

Humo ndani FA alinata na biti kwa dakika tano akieleza jinsi anavyowapenda na kuwahusudu wanawake na kuheshimu uwepo wao duniani.

Sio peke yake, miaka zaidi ya 15 mbele wasanii wengine wa kiume wa Bongo wameibuka na kuonyesha jinsi wanavyowakubali wanawake huku utofauti wao na Mwana FA ukiwa ni wenyewe wameonyesha kwa vitendo na sio kupitia wimbo.

Wapo waliofanya shoo kwa ajili ya wanawake tupu, wapo waliokuwa na walinzi wa kike na zaidi, na katika makala haya tunachambua wakali hao na namna walivyoonyesha mahaba yao kwa wanawake kwa njia ambazo pengine hazikuwahi kufanyika kabla.


SHOO YA WANAWAKE TUPU

Advertisement

Katikati ya mwaka 2020 mkali wa muziki wa R&B nchini, Juma Mkambala maarufu Jux alifanya shoo maalumu kwa ajili ya wanawake tu, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika kitu kama hiko nchini Tanzania.

Ili uingie kushuhudia shoo hiyo iliyopewa jina la King of Hearts na kufanyika kwa masaa sita katika moja ya hoteli kubwa jijini Dar es Salaam ilikuwa ni lazima uwe mwanamke. Na humo ndani, karibu kila kitu kilifanywa na wanawake, kuanzia wahudumu mpaka maDJ.

Jux aliliambia gazeti hili kuwa aliamua kufanya hivyo kwa sababu anawapenda wanawake na wamekuwa mashabiki wake wakubwa kwa muda mrefu hivyo aliona kuna umuhimu wa kuwapa zaidi na kuwaonyesha mapenzi mazito aliyonayo juu ya pisi kali.


BODYGUARD WANAWAKE

Wakati ‘trend’ ya kila msanii nchini kuwa na walinzi inaanza, rapa mshamba kutoka Mwanza, Young Killer Msodoki alikuja na mpya ya kulindwa na ma-bodyguard wa kike. Yaani wakati kina Diamond wanalindwa na ma-bodyguard wa kiume wenye mbavu nene kama Mwarabu Fighter na wengine, Msodoki yeye alikuwa analindwa na pisi fulani hivi za moto ile mbaya.

Kwenye moja ya mahojiano, mkali huyo wa wimbo wa Dear Gambe alifunguka kuwa ameamua kuwa na ma-bodyguard wa kike kwa sababu kubwa mbili, kwanza kwa ajili ya kuwa na utofauti na wasanii wenzie wote ambao wanatumia walinzi wa kiume, na pili anaamini kuwa kila kinachofanywa na mwanaume, mwanamke anaweza kukifanya kwa ubora mara mbili yake.

Kwa sasa Young Killer halindwi tena na ma-bodyguard hao pia haonekani kutembea na walinzi mara kwa mara kama alivyokuwa akifanya kipindi kitambo hiko, mwaka 2019.


DJ NA MENEJA WA KIKE

Staa wa zamani wa bendi ya Yamoto, Mbwana Kilungi maarufu Mbosso alipoanza kazi pale Wasafi alianza na mkwara wa kutaka kupewa DJ mwanamke na Meneja mwanamke pia. Mabosi wake wakamsikiliza na kumpa DJ anayefahamika kwa jina la DJ Zeylee na meneja anayeitwa Sandra Brown.

Akitolea ufafanuzi staa huyo mwenye albamu mpya ya The Definition of Love aliwahi kusema anaamini uwezo mkubwa wa kufanya kazi walionao wanawake na ndiyo maana alitaka kufanya kazi na meneja mwanamke na Dj wa kike tofuati na wasanii wengine ambao huwapa nafasi hizo wanaume.

Hata hivyo, mpaka sasa Mbosso amebakiwa na DJ mwanamke tu, kwani alishaacha kufanya kazi na aliyekuwa meneja wake.


KUSINDIKIZWA NA WANAWAKE

Kwenye tamasha la Wasafi Tumewasha na Tigo mwaka jana Diamond alikuwa akisindikizwa na wanawake kila anapokwenda. Yaani ndani ya gari aliyokuwa akiingia nayo uwanjani (kwenye shoo) ilikuwa inambeba yeye na wanawake wakali wakali takribani sita hivi waliovaa sare sare.

Wanawake hao walikuwa wanamfuata Diamond au unaweza kusema walikuwa wakimsindikiza kila mahali isipokuwa jukwaani tu. Kwa mfano, kwa kawaida kabla ya msanii kupanda jukwaani huwekwa kwenye eneo maalamu la wasanii kusubiri, basi ilikuwa ukimkuta Diamond kwenye eneo hilo basi ujue atakuwa yupo katikati ya watoto fulani wakali amezungukwa.

Alipoulizwa kwanini aliamua kuja na staili hiyo alisema hapendi kutabirika, anapenda kuja na vitu vipya ili mashabiki zake wasimzoee na kumchoka, lakisni ukweli tunaujua kwamba Simba na mabinti ni damu damu, anapenda kuwa karibu nao muda wote.


Advertisement