Wakali wa muziki Afrika Mashariki watumbuiza Oktobafest

Muktasari:
- Tamasha hilo limetumika kama daraja la kuunganisha tamaduni na watu mbalimbali wa Afrika Mashariki kwa lugha ya muziki.
Dar es Salaam. Wasanii wanaotamba Afrika Mashariki, wakiwamo Watanzania, Bill Nas, Chino na G Nako ni miongoni mwa waliotumbuiza kwenye tamasha la Serengeti Lite Oktobafest.
Wengine ni Nyanshiski wa Kenya, Jose Chameleon wa Uganda, Ali Kiba wa Tanzania sanjari na wabunifu kama vile Makeke International kutoka Tanzania, wote wakishirikiana kwenye jukwaa moja kugusa mioyo ya maelfu ya Waafrika Mashariki katika tamasha hilo lililofanyika kwenye fukwe ya Coco, Dar es Salaam.
Meneja wa Chapa ya Serengeti Lite na Serengeti Premium Lager, Esther Raphael akizungumza leo Jumapili Oktoba 22, 2023 jijini hapa, amesema tamasha hilo si tu lilijikita kwenye maadhimisho ya muziki na utamaduni, vilevile liliwawezesha vijana wa Afrika Mashariki kupata fursa za biashara.
Amesema pia tamasha hilo limetumika kama daraja, kuunganisha tamaduni na watu mbalimbali wa Afrika Mashariki kwa lugha ya muziki.
"Serengeti Lite Oktobafest pia lilijikita kutunza mazingira kuhakikisha taka zote zinakusanywa, mazingira yalipewa kipaumbele, lakini usalama nao ulikuwa ni kipaumbele cha juu.
"Waandaji walishirikiana na Uber ambao walitoa punguzo la asilimia 40 kwa watu kuja kwenye tamasha Coco Beach na kurudi, hatua hii ililenga kuzuia hatari zinazohusiana na uendeshaji wa magari wakiwa wamelewa, kuhakikisha kuwa washiriki wote walikuwa na njia salama na ya kuaminika ya usafiri," amesema Raphael.
Akizungumza baada ya tamasha hilo, mfanyabiashara mdogo, Mariam Mohammed amesema;
“Nitoe pongeze za kipekee kwa waandaaji, tukio kama hili limelenga kusherehekea tamaduni mbalimbali za Tanzania. Sisi wafanyabiashara wadogo tumepewa fursa ya kuja kuonyesha bidhaa zetu na uwezo tulionao kwa ajili ya watu watakaokuja kupata burudani huku wakipata bidhaa za asili kabisa kutoka kwa wazalishaji wazawa. Nimevutiwa na maandalizi na idadi kubwa ya watu waliojitokeza.”
Naye shabiki wa muziki aliyejitambulisha kwa jina la ‘Queen T’ amesema hiyo ikuwa fursa adhimu kwa wananchi kuwaona wasanii wakubwa wakipanda kwenye jukwaa moja kutumbuiza.
“Mimi nilenda Coco kwa ajili ya kumuona Ali Kiba akitumbuiza, huwa ninamfutailia sana muziki wake, lakini nilimuona ‘live’, tumezoea matukio kama haya mengi yanafanywa na wanasiasa wanapokuwa kwenye mikutano yao, nawapongeza sana Serngeti kwa uamuzi huu,” amesema shabiki huyo.